Alichozingua Said Said ni kufanikiwa

Muktasari:
- Nasema nafasi nyingine kwa sababu hii ni mara yake ya pili. Mara ya kwanza alifanya hivyo wakati wa utoaji wa tuzo kwa wachekeshaji Tanzania na alitoka akiwa ‘man of the match’ mpaka akapata picha ya pamoja na Mama Samia.
JUZI kati mchekeshaji Said Said alipata nafasi nyingine ya kuchekesha mbele ya kiongozi mkuu wa serikali ya Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan.
Nasema nafasi nyingine kwa sababu hii ni mara yake ya pili. Mara ya kwanza alifanya hivyo wakati wa utoaji wa tuzo kwa wachekeshaji Tanzania na alitoka akiwa ‘man of the match’ mpaka akapata picha ya pamoja na Mama Samia.
Watu walimsifia sana siku ile. Wachekeshaji wengi walipanda kwenye lile jukwaa kuchekesha, lakini Said Said ndiye aliyezungumziwa na kusifiwa zaidi. Sasa majuzi alipopanda tena matokeo yalikuwa tofauti, badala ya kusifiwa.
Said Said ndiye msanii aliyepondwa zaidi huku watu wengi wakisema vichekesho vyake vilizingua kinoma. Kwamba havikuwa na adabu mbele ya hadhira ya siku ile ambayo ilikuwa imejaa viongozi na vigogo serikalini.
Nimetazama ile video ya Said Said dakika zote tisa - tena sio mara moja, sio mara mbili, mara nyingi kwa kurudia rudia, lakini sioni shida ilikuwa wapi.
Sioni kichekesho gani kilikuwa kinazingua na ubaya ni kwamba watu wote wanaomshambulia wanasema tu “dogo umezingua, dogo umezingua”, lakini hawasemi amezingua sehemu gani wala hawataji kichekesho ambacho kinawafanya waseme hakuwa na heshima.
Watu wangesema hakuchekesha ningewaelewa kwa sababu kila mtu ana vichekesho ambavyo humchekesha na ndiyo maana kwa wingine, mchekeshaji wao bora ni Eliud wakati wengine hawamuelewi hata kidogo wanajiuliza huyu anachekesha nini.
Nachotaka kumwambia tu Said Said ni kwamba sasa anaweza kuanza kujiita msanii mkubwa. Kwanini? Kwa sababu tayari Watanzania wameshaanza kumuonyesha tabia wanazofanyiwa wasanii wakubwa wanaofanya vizuri.
Watanzania tuna kasumba ya kutopenda kuona wasanii wetu wakifanya vizuri. Kila anapotokea msanii akafanya vizuri lazima tulazimishe kumtafutia makosa au kumtengeneza mtu mwingine na kujaribu kumpa nafasi ya mtu anayefanya vizuri.
Kama ambavyo kwa miaka nenda rudi tumemsema Diamond hamna kitu, na tukaleta wasanii kibao wa kumshindanisha naye ili kumshusha - wasanii wa ndani na wa nje. Kina Alikiba, Burna Boy, Wizkid na Davido. Kina Marioo, Harmonize na zaidi.
Hassan Mwakwinyo ambaye naye amepitia changamoto ya kupondwa kwa sababu tu ya kuwa mwanamasumbwi bora wa Tanzania aliwahi kusema hiki kitu ukiona Watanzania wanakusifia tu, basi jua hakuna kitu cha maana unafanya. Watanzania wanachukia watu wanaofanya vizuri.
Zuchu anapitia changamoto hii. Nandy amewahi kupitia kasumba ya kuchukiwa kwa sababu ya mafanikio. Ruby amewahi kupitia hii hali. Orodha ni ndefu na inanifurahisha kwa sababu ni kama vile Watanzania wanatumia moyo, roho na akili moja. Wakikuchukia, wanachukia kwa pamoja na wakikupenda wanakupenda kwa pamoja.
Kimsingi wanapokupenda unatakiwa kuwa makini sana kwa sababu inawezekana hawakupendi kwa mapenzi, bali inawezekana wanakupenda kwa sababu wanataka kukutumia kumshusha msanii mwenzako mkubwa.
Ningekuwa Said Said ningewasikiliza Watanzania na kupembua yenye ukweli, lakini nikizingatia kwamba ni watu wenye tabia ya kupenda kushusha wasanii wakubwa. Kisha ningerudisha umakini kwenye mambo yangu na kujiandaa kwa ajili ya shoo nyingine nikitambua kwamba tayari nimeshakuwa msanii mkubwa.