Britney Spears: Sina mpango wa kurudi kwenye muziki
Muktasari:
- Britney Spears amepinga uvumi kuwa ana mpango wa kurudi kwenye tasnia ya muziki, akisema kuwa hana mpango huo wala siyo miongoni mwa vitu anavyopanga kuvifanya.
Britney Spears (42), ameapa kutorudi kwenye muziki licha ya timu yake kuzungumza na waandishi mbalimbali wa nyimbo kwa ajili ya kuandaa albamu yake ya 10.
Staa huyo wa muziki na filamu amesisitiza kuwa, "Nimekuwa nikisikia habari nyingi lakini ni takataka, wanasema ninatafuta waandishi waniandikie nyimbo kwa ajili ya kuandaa albamu yangu ya 10, ukweli ni kuwa sitorudi tena kwenye tasnia ya muziki,” amesema Britney kwenye chapisho aliloliandika kwenye mtandao wa Instagram.
Amesema ameandika sana nyimbo. "Ninapoandika, ninaandika kwa kujifurahisha au ninaandikia watu wengine. "Kwa wale ambao mmesoma kitabu changu, kuna mambo mengi ambayo hamjui kunihusu,”amesema.
Licha ya kusisitiza kutokuwa na hamu ya kushika kipaza sauti na kuimba. Mtandao wa Page Six umeeleza Britney aliwaeleza wafuasi wake kuwa ameandika zaidi ya nyimbo 20 kwa watu wengine, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. "Mimi ni mtunzi ila ni mwandishi nisiyejionyesha au kuonekana (ghost) na ninalifurahia hilo " amesisitiza.
Mtandao huo umeripoti kuwa nyota huyo amewaeleza mashabiki zake wasibane pumzi wakitegemea muziki moya kutoka kwake, kwani hana mpango wa kufanya hivyo.
Amesema kutengeneza muziki hakupo kwenye orodha ya mambo yake anayofanya.
Britney pia amekanusha uvumi kuwa kitabu chake cha "The Woman In Me" kilitolewa bila idhini yake.
"Watu pia wanasema kitabu changu kilitolewa bila kibali changu, na hiyo ni mbali na ukweli," ameandika mama huyo wa watoto watatu.
Tamko la Spears linakuja siku chache baada ya mtandao wa Page Six kuripoti taarifa kuwa Charli XCX na Julia Michaels wanataka kuandika nyimbo katika albamu inayofuata ya mshindi huyo wa tuzo moja ya Grammy, huku akitajwa kuiwania mara nane.
Britney alitangaza kuacha muziki mwaka 2019.
Kwenye kitabu cha Britney kulikuwa na siri nyingi za maisha yake, kubwa ikiwa ni kueleza alivyolazimika kutoa mimba baada ya aliyekuwa mpenzi wake Justin Timberlake kumwambia hayupo tayari kuwa baba.
"Kusudi la kitabu changu halikuwa kumkasirisha mtu yeyote kwa njia yoyote. Hiyo ilikuwa mimi wakati uliopita, zamani," Spears aliandika, akizidi kufichua kuwa kufuatwa fuatwa na vyombo vya habari kulimfanya aache biashara ya muziki mnamo 2019.
Kwa mujibu wa tivuti ya Elite Daily staa huyo alisema, "Sipendi vichwa vya habari ninasoma, hiyo ndiyo sababu kwa nini niliacha biashara ya muziki miaka minne iliyopita.