Boifrendi wa shosti yangu anataka kunioa

Muktasari:

13. ANKO Lao, kijana miaka 20 kuna rafiki yangu anatembea na mpenzi wangu. Naomba ushauri wako cha kumfanya.
Clever Nyimbo, Kigoma

1. ANKO Lao, mimi ni binti wa miaka 20, nina mpenzi ananipenda sana ila shida alikuwa ni boifrendi wa rafiki yangu na anataka kunioa. Nifanyeje?
Grecious, Dar
Jibu
: Hujisikii noma kukubali kuchanganywa na shoga'ko? Uko tayari kuvunja urafiki na shosti wako? Vipi Shosti wako anafahamu kuwa unataka kumpindua na kuumiliki jumla jumla utamu wake? Sina hakika kabisa na huyo jamaa kama kweli anataka kukuoa, ila nadhani amekuingia na gia hiyo ili akunase kirahisi baada ya kupita na shoga'ako. Kuwa makini, aibu ya kumpindua mwenzako itaweza kukurudia, kwani jasiri haachi asili.

2. ANKO Lao, mimi ni kijana wa miaka 20 nina mpenzi tunayependana ila tulipotezana kwa miezi saba, cha ajabu tulipoonana akanikaushia kama hanijui. Nifanyeje?
MHD Zahor, Zanzibar
Jibu
: Kama kusoma hujui, basi picha nayo unashindwa kuielewa, hiyo ndo imeshatoka... unaambiwa ukiona manyoya ujue kaliwa, mwenzio keshajiongeza, kazi kwako...hakuna namna tena! Ninachokushauri acha kusema "nina mpenzi tunayependana" bali sema wewe ndo unampenda. Mngekuwa mnapendana asingekukaushia.  

3. ANKO Lao, mimi ni kijana wa miaka 26. Shida kubwa niliyonayo ni kusumbuliwa na wamama na wadada. Naomba ushauri wako.
Osuman Jr, Tanga
Jibu
: Nashindwa kujua unasumbuliwa nao kivipi kidume mzima kama wewee? Ungefunguka iwe rahisi kujibiwa, hata hivyo nahisi kama unajipepelea tu, kuonyesha eti unapapatikiwa wakati dalili zinaonyesha unahaha kinoma kusaka ving'asti. Ushauri wangu, pambana kutafuta pesa kwanza!

4. ANKO Lao, nimekuwa nikisumbuliwa na kupiga sana puchu kiasi nimeshindwa kabisa kuacha kwa haraka. Nifanyeje?
Steven Edgar, Ubungo Dar
Jibu
: Kama ulivyoanza kujifunza kufanya upuuzi huo ndivyo unavyotakiwa kupambana kuachana nao. Ila kwa ushauri kiduchu ili usitoke patupu, fanya hivi. Kwa kuwa uraibu ni tatizo sugu ambalo sio rahisi kuacha mara moja, weka mkakati kuacha ngazi kwa ngazi, anza na dhamira ya kuacha wiki nzima. Kisha utaongeza wiki nyingine, kisha mwezi kisha, miezi mitatu hadi utafika mwaka mzima bila ya kujichua. Tena uache kuangalia na picha chafu. Juhudi zako ndio uzima wako. Kwa taarifa yako ukizubaa huko mbele ya safari utakuwa mpenzi mtazamaji tu ukiwa na baby pale uwanja wa fundi seremala. Shauri yako we jiendekeze tu!

5. ANKO Lao, kijana miaka 20 nina mpenzi ila shida anapenda sana tupige shoo yaani kila wakati. Nifanyeje?
Yunus Omar, Pwani
Jibu:
Kwa umri ulionao kutoa malalamiko kama haya ni kujichoresha, kwani wenzako wazee wa hizi kazi wanazitafuta mechi za hivyo hawazipati. Ushauri wangu kama shamba limekushinda kulima waachie wenzako, ila ni muhimu kutambua unapaswa kujiweka fiti kwa vile hata katika soka zipo mechi za dakika 90 na zile za 120 ukiwa na pumzi kisoda utaaibika. Shauri yako.

6. ANKO Lao, binti miaka 18 kuna jamaa simpendi ila ananilazimisha kuwa naye. Nifanyaje?
Amina Ally, Tanga
Jibu:
Sijajua analazimisha vipi, ila ni vyema ukamueleza hisia zako zilivyo kwake ili ajiongeze, lakini kama ulishamlia vyake jiandae kuvitapika, kwani vidume vingine hawaliwi vyao kiboya. Hivyo tu!

7. ANKO Lao, binti miaka 20 na kuna mpenzi tunapendana sana ila anataka kumjua mpenzi wangu wa mwanzoni sasa naogopa kumwambia maana sijui anataka kumfanya nini? Naomba ushauri.
Zuleah wa Dar
Jibu:
Huyo jama'ako ni wale vijana wasiojiamini, anataka kumjua zilipendwa wako wa kazi gani? Mwambie ashughulike na yake na mpashe kabisa akiendekeza uduwanzi wa hivyo utampiga chini, kwani hata yeye huenda ana makoloni kibao aliyowahi kuyamiliki na pia mapenzi si kuchunguzana!

8. ANKO Lao, kijana miaka 24, nina mwanamke nipo naye katika uhusiano kwa miaka minne ila bado hajanizalia mtoto japo alishazaa na mtu aliyekuwa naye mwanzo na anasema ananipenda. Nifanyeje?
Hussein Nuru, Handeni Tanga
Jibu:
Umeniangusha sana jombaa, yaani miaka minne huna maajabu yoyote kwa bibie na umetulia tu?! Ebu fanya chapu uende hospitali ukajicheki, usije ukawa joka la kibisa lisilong'ata... Pia huenda bibie anakubania kwa vile hujamuoa maana miaka minne ni muda mrefu ungekuwa upo siriazi naye ungeshaoa kabisa kwa sasa, hivyo anaogopa kubebeshwa mzigo kienyeji. Kazi kwako!

9. ANKO Lao, kijana miaka 25 nina mwanamke ninayepiga deiwaka tu, lakini anataka mtoto na bado sijajipata. Nifanyaje?
Godson Kikoti, Iringa
Jibu
: Kama unajua bado hujajipata, ungetuliza boli kushobokea malavidavi kwani unaweza kupigwa shoti bila kujua. Halafu ni vyema ungeoa kwani umri unakuruhusu kuliko kutambaa na chaki kisela.

10. ANKO Lao, binti miaka 18 kuna mwanaume anasema ananipenda na kanizidi umri mfano wa baba yangu na simtaki, ila anafosi. Naomba ushauri wako.
Janeth Ngulyati
Jibu:
Umri ni namba tu, kama sio mume wa mtu na anayeeleweka ni wewee tu na roho yako, ila iwapo huna mahaba naye mjulishe ajue na acha kumshobokea na kupokea zawadi zake. Fanya hivyo!

11. ANKO Lao, kijana miaka 30 kuna msichana nampenda ila nikimuona nashindwa kumwambia. Nifanyeje?
Shaaban Ally, Morogoro
Jibu:
Kwa umri ulionao ni wazi wewe ni wale vijana wenye midomo zege isiyoweza kuimbisha na pia huna ujasiri wa kumtokea mtu...sasa kwa taarifa yako usipokomaa utaishia kula kwa macho na siku utakaposhtuka wajanja watakuwa wameshapita na bibie na kuishia kiujisonya tu. Changamka!

12. ANKO Lao, kuna msichana nimemuelewa sana ila kila nikimuita tuongee anaona aibu, hivyo nashindwa kumuelewa. Nifanyeje?
David Kimaro, Kilimanjaro
Jibu
: Wewee ebu jiongeze...kama umemzimikia mfikishie ujumbe ujue moja, maana huenda tayari kuna mtu ameshajiweka kwake, hivyo anaona gozigozi kwako...halafu kwa dunia ya sasa hupaswi kutumia njia za kizamani za kuitana sijui mpige stori, wakati unaweza kumtokea hata kwa kwa simu we vipi?

13. ANKO Lao, kijana miaka 20 kuna rafiki yangu anatembea na mpenzi wangu. Naomba ushauri wako cha kumfanya.
Clever Nyimbo, Kigoma
Jibu
: Mayanki wa zama hizi hivi mmekumbwa na mdudu gani? Sasa kama umeshajua umezungukwa, unataka nikupe ushauri gani, yaani unashindwa kujiongeza hapo kama hilo unalosema una uhakika nalo?

14. ANKO Lao, kuna msichana nampenda sana ila nashindwa kumwambia kwa sababu tumezoeana mno. Nifanyaje?
David,  Igoma Mwanza
Jibu:
Usizuge weweee, si useme tu unasumbuliwa na domo zege, kwani kuzoeana na mtu kunazuia nini kuimbisha kama umemuelewa? Sasa chelewa chelewa ukute mwana si wako...kama una hakika jimbo lipo wazi tangaza nia kieleweke!

15. ANKO Lao, kijana miaka 18 kuna msichana nampenda na nimeshamwambia ila anasema muda utaongea. Nifanyaje?
Simon Samwel, Mwanza
Jibu:
Kwa umri ulionao, ni vyema ungepambana kujitengenezea kesho yako, kuliko kushobokea malavidavi, kwani huenda huyo bibie ameshakusoma na kuona huna ishu ndo maana anakupotezea!

16. ANKO Lao, kuna boy tuliyepata naye mtoto ila nikimwambia kuhusu suala la kufunga ndoa anakuwa mkali sana. Nifanyaje?
Neema, Morogoro
Jibu
: Ukiona hivyo ujue, umeingia kwenye mtumbwi wa vibwengo, huyo jama'ako hakuwa na mipango nawe licha ya wewe kujilengesha na kuzaa naye. Hutakiwi kupaniki kwani uliyataka mwenyewe...ungejituliza kwenu wala usingebebeshwa mzigo kienyeji. Kaa kwa kutulia ulee mwanae na siku ikifika utaolewa. Usilazimishe!

17. ANKO Lao, kuna mwanamke nimetokea kumpenda na nimemtolea barua, ila hataki kunipeleka kwao kunitambulisha kwa wazazi. Nifanyeje?
Richard John, Moro
Jibu
: Aisee wee unachekesha kweli, yaani umtolee mtu barua kisha usipajue kwao? Hiyo barua ulipeleka kwa mjumbe au ofisi ya Serikali za Mitaa..? Acha mizinguo, ni wazi inaonekana hujui hata taratibu za kuposa! Jipange tena!

18. ANKO Lao, nina mke na ninaishi na familia, ila kuna binamu yangu ananitega sana kimapenzi, kiasi naanza kumtamani. Nifanyeje?
Barakael Steve, Moshi
Jibu:
Huna lolote wee tamaa nyingi! Kama una mke, binamu hata akutege vipi si umkaushie au unataka kwenda na ule usemi kuwa binamu kinyama cha hamu? Si unajua tamaa zilimponza fisi...utaharibu. Shauri yako!

19. ANKO Lao, kijana miaka 19 nipo chuoni kwa sasa, nina ndoto za kuja kuwa mtangazaji mkubwa hapa nchini. Nifanyeje?
Jerome Mwakipesile, Mbeya
Jibu:
Sijajua huko chuoni kwa sasa unasoma nini...ila kama una sauti na kipaji, sioni tatizo, muhimu komalia masomo ya taaluma hiyo ya habari na utangazaji, vinginevyo kama utalazimisha kazi isiyoendana nawe utazingua. Fanya mazoezi mengi ya kutangaza, fungua akaunti yako ya YouTube, posti sauti yako ukisoma taarifa mbalimbali au fanya masimulizi ya sauti. Utazidi kujiamini kiutangazaji.

20. ANKO Lao, kijana miaka 21, tatizo langu kubwa ni ulevi kupindukia kiasi nashindwa kufanya mambo ya maendeleo. Najaribu kuacha lakini nashindwa. Nifanyeje?
Micky Kimario, Arusha
Jibu:
Kama umeshajua kugida ulabu hakuna faida, ni suala la wewe kukata shauri tu. Unajua kabisa we hukuzaliwa mlevi, ila kilaji umejifunza...kama umeshaona haina faida kwako unapaswa kukomaa kuachana nao, kwani hakuna atakayekuja kukusaidia ila ni wewe mwenyewe uamue. Ila unaweza kuanza kuacha hatua kwa hatua. Acha kwa wiki nzima, mwezi mzima, miezi mitatu, sita hadi utafika mwaka bila ya kuonja. Kazi kwako!

Nawe una jambo linakutatiza kwenye malavidavi au maisha ya kawaida? Usisite uliza kupitia namba 0773-732271 na Anko Lao atakujibu freshi tu!