Bingo, Walitesti zali kisha wakanogewa

KATIKATI ya zaidi ya aina 1000 za muziki duniani kila msanii amechagua kujikita kwenye aina yake ya muziki. Wapo wanaofanya Singeli, K Pop, Jazz, Hip Hop, Blues, Gengetone, Dancehall, Japanoise na mingine huku kila mmoja akiwa na sababu za kuchagua kufanya anachofanya.

Hata hivyo, kwa kawaida wasanii wengi hufanya zaidi ya aina moja ya muziki, lakini bado karibu kila msanii duniani anakuwa na uwanja wake wa nyumbni, aina ya muziki ambayo ndio inayomtambulisha, kwahiyo hata akijaribu kufanya muziki mwingine mwisho wa yote atarudi tu kwenye muziki wake aliozoeleka kuufanya.

Kwa mfano Diamond, anafanya muziki aina ya Afro Pop, huo ndio uwanja wake wa nyumbani, lakini pia mara kadhaa amewahi kujaribu aina nyingine za muziki, amewahi kuimba Mchiriku, Mduara, Zouk, Hip Hop na zaidi lakini mwisho wa yote hurejea kwenye Afro Pop yake.

Lakini pia, kuna wasanii wachache ambao walipata umaarufu kupitia aina fulani ya muziki, lakini baadaye wakajaribu muziki mwingine na walipoona wamepokewa vizuri, wakagoma kurudi kwenye muziki waliokuwa wakiufanya awali — na leo ndo tunawaongelea hao washikaji.

Kumbuka: tunaongelea wasanii ambao walibadilisha aina ya muziki au namna ya uimbaji wakiwa tayari wameshapata ustaa kupitia aina ya muziki au staili ya kuimba waliyokuwa wakiifanya awali.

MBOSSO

Umaarufu wake umeanzia Yamoto Band, na akiwa hapo Maromboso alikuwa akiimba kwenye ‘punch’ ya juu kama ambavyo wasanii wote wa bendi hiyo walivyokuwa wakiimba.

Mwaka 2017 bendi ikavunjika, kila mtu akala kona, na Maromboso akaibukia Wasafi akiwa na jina jipya, ila uimbaji ule ule aliokuwa akiimba Yamoto Band. Nyimbo kama Nimekuzoea, Picha Yako na Watakubali ni kati ya ushahidi wa hiki tunachokisema.

Hata hivyo, ngoma hizo ni kama hazikumpa ‘boost’ sokoni ukizingatia kwa kipindi hicho, mwanabendi mwenzake wa zamani Aslay alikuwa kwenye chati ile mbaya. Ndipo baada ya muda Mbosso akaachia wimbo wake wa kwanza wa tofauti unaoitwa Nadekezwa akiimba kwa ‘pitch’ ya chini na tangu hapo mpaka leo hajawahi kurudi alipotoka, kwenye pitch ya juu.

Mbosso ambaye jina lake halisi ni Mbwana Kilungi amekiri aliyemshauri kufanya mabadiliko hayo ni Cassim Mganga.

“Cassim ndo aliniambia nibadilishe muziki, aliniambia, mdogo wangu ushaimba sana, ushapiga sana kelele, sasa imba chini, wabembeleze watu,” Mbosso ameeleza.

DARASSA

Mwaka 2010 Darassa hakuwa Mr. Burudani kama anavyojiita leo, alikuwa akiimba Hip Hop ngumu ya kuiongelea mitaa kama wanayofanya kina Nikki Mbishi na Fid Q na akafanikiwa kuachia hit song mbili, Sikati Tamaa aliyomshirikisha baba Anelisa, Ben Pol na Nishike Mkono aliofanya na Winnie.

Alikuwa maarufu, lakini umaarufu wa kawaida, akachoka na hali hiyo, mwaka 2016 akaamua kubadilika, akaachia ngoma inayoitwa Kama Utanipenda akimshirikisha Mavoko, wimbo ambao ndani yake alirap lakini kwa staili ya tofauti sana, ya kama anaongea, kama kulainisha hivi — kilichotokea ni mitaa ikakubali staili hiyo, naye akanogewa, akaachia Too Much, kisha mwishoni mwa 2016 akaachia ngoma ya kihistoria ya kuitwa Muziki ambayo ili hit kuliko namna tunavyoweza kuiongelea na tangu kitambo hicho, mpaka leo hajawahi kurudi kwenye ile aina yake ya muziki, ya Hip Hop ya kuingolea mitaa au ‘Boom Bap’ kitaalamu.

Kuna kipindi alikumbana na kupondwa kwamba amepoteza muelekeo kwenye muziki wake kwa kuanza kuimba Hip Hop laini, alijibu kwamba; “Ukiwa Mtanzania hustahili kutetea utamaduni wa Hip Hop, unatetea wewe kama nani wakati Hip Hop ni utamaduni wa Wamerakani Weusi? Sisi (Watanzania) tunatakiwa kutetea muziki wa kina Saida Karoli tukiona unaharibiwa. Huo ndio utamaduni wetu.”

DOGO JANJA

Alipokutana na Madee na kuomba msaada alimwambia yeye anafanya muziki wa Hip Hop. Na hata Madee alimpoleta mbele ya Watanzania Janjaro alithibitisha kwamba yeye ni mtu ‘mbad’ kwenye kuchana.

Kwa kipindi chote Dogo Janja amekuwa akifanya Hip Hop mpaka ulipotokea mgogoro kati yake na Madee na kumfanya akahamia menejimenti nyingine ya Ostazi Juma Na Musoma. Akiwa kwenye menejimenti hiyo mambo hayakuwa shwari, napo akatibuana napo na kupotoea kwenye gemu kwa muda fulani.

Aliporudi aliibukia kwa Madee tena, na safari hii aliibuka akiwa na staili mpya ya muziki ambayo ni Dancehall na ndio muziki anaofanya mpaka sasa huku akionyesha hana dalili yoyote ya kurudi kwenye Hip Hop. Hata hivyo, mara kadhaa amekuwa akirap kwenye nyimbo hizo pia.

CHRISTIAN BELLA

Alikuwa kwenye bendi, alikuwa anaimba muziki wa dansi. Baadaye akachomoka kwenye bendi na kuanza kujichanganya na wasanii wa Bongofleva, matokeo yake naye akaanza kuimba muziki mpya, muziki ambao ilikuwa ni mchanganyiko wa kama muziki wa dansi na Bongofleva na mpaka leo bado anafanya hivyo.

Hata hivyo, bado anagusia gusia muziki wa dansi katika bendi yake ya Malaika ambayo kwa sasa ni kama imekufa fulani hivi. Jamaa anaonekana anaipenda sana bongofleva na kuwa solo artist (msanii wa kujitegemea).

LAVALAVA

Alipotoa wimbo wake wa kwanza mpaka Alikiba akamvulia Kofia. Kumbuka wimbo wake wa kwanza ulikuwa ni Bora Tuachane na aliutoa akiwa Wasafi, lebo ambayo inamilikiwa na mpinzini namba moja wa Kiba, Diamond Platnumz, lakini Kiba hakujali hilo, alikiri kwamba kwenye sekta ya kuimba ngoma za kulalamika Lavalava ni noma mpaka chenji inabaki.

Lakini baadaye Lavalava akaona ni kama muziki wa aina hiyo haumpeleki mahali, ndipo akaamua kubadilika rasmi mwaka 2019 na kuachia wimbo wa Afro Pop wa Go Gaga na tangu hapo hajaonesha dalili za kutaka kurudi alipotoka au kama amerudi basi ni katika nyimbo chache sana.