Barbie Mia nafasi yako ilikuwa inasubiri Bongo

Muktasari:
- Lakini, ukiangalia marapa wengi wa kike wa Tanzania wanafanana kitu kimoja - wengi ni wagumu, wanarap kigumu, wanaongea kigumu, wanavaa kigumu au tuseme kiume. Sio kitu kibaya, lakini kusema ukweli kwa kiasi kikubwa soko lilikuwa linahitaji rapa wa kike mwenye swagga za kidada na hapo ndipo anapoingia Barbie Mia.
TANZANIA haijawahi kuwa na uhaba kivile wa marapa wa kike. Japo sio wengi, lakini wanajaa kwenye orodha. Tumewahi kuwa na Sister P na Zay B kwenye kizazi cha kwanza cha muziki. Tukabarikiwa kina Rah P, tukawa na Chiku Keto. Tunae Rozalia, Frida Amani an Chemical wanakimbiza kwa sasa na wengine kibao ambao sijawataja.
Lakini, ukiangalia marapa wengi wa kike wa Tanzania wanafanana kitu kimoja - wengi ni wagumu, wanarap kigumu, wanaongea kigumu, wanavaa kigumu au tuseme kiume. Sio kitu kibaya, lakini kusema ukweli kwa kiasi kikubwa soko lilikuwa linahitaji rapa wa kike mwenye swagga za kidada na hapo ndipo anapoingia Barbie Mia.
Barbie Mia sio jina jipya ni mtu aliyetrendi na kiki nyingi mjini kwa sababu ni mtu wa kiki. Kuna kipindi alikuwa anavuma na skendo ya kutoka na Simba Dangote. Na hata kwenye muziki sio mgeni amewahi kuachia ngoma zake mbili - tatu ambazo ziliishia Chalinze hazikuingia mjini na hakuna mtu aliyeona kama ana nafasi.
Lakini, hivi majuzi Barbie Mia chini ya lebo ya Iam Music inayoongozwa na rapa Country Boy aliachia EP yake ya kwanza ya kuitwa Life of Barbie na nitakwambia tu ukweli - ngoma nne za EP hiyo zinatosha kutuamsha mashabiki wa rap Tanzania na kutukumbusha kwamba kuna ladha fulani ya rap tulikuwa tunaikosa.
Barbie Mia anarap kilaini, sexy, kama mdada unaweza ukajiuliza hiyo inahusiana nini na muziki, lakini amini nakumbia moja ya kilichowabeba kina Nick Minaj na Card B ni uwezo na urembo wao.
Kukosekana kwa rapa wa kike wa staili za Barbie Mia kwa muda mrefu kunafanya nikiri kwamba tunamhitaji Barbie Mia. Tunamhitaji kwa sababu anaileta rap kwenye kona tofauti kabisa. Barbie Mia alivyojitambulisha siyo rapa wa kukumbatia 'punchlines' kama kina Chemical au Frida Amani, lakini ana kitu kingine — anafanya rap kidada akijishaua, akiringa.
Na hii ni muhimu kwa sababu kwa muda mrefu tumezoea kuona wanawake kwenye rap wakilazimika kujifanya wao ni “wagumu” ili wachukuliwe siriazi. Lakini, Barbie Mia anatuonyesha kwamba unaweza kuwa dada wa kawaida, unapenda kusuka na kupaka lip gloss ya pink na bado ukarapu ukapendelewa.
Na kwa kweli, hayo ni mabadiliko ya namna yake. Ni kama namna ambavyo kina Doja Cat au Cardi B walivyobadili landscape ya rap Marekani - hawakuchagua kuwa wagumu, bali waliamua kuleta rap kutoka kwenye dunia ya kike, na bado wakaipa uzito.
Kwa sasa tunapomwangalia Barbie Mia na Life of Barbie ni wazi kuwa huu ni mwanzo mpya sio tu kwake kama msanii, bali kwa mwelekeo wa rap ya kike Bongo. Na pengine, huu ndio wakati ambao muziki wetu unahitaji Barbie energy zaidi.