Banana Zoro avutiwa na kazi ya Simba

Monday April 05 2021
BABANA ZORO PIC
By Olipa Assa

MSANII mkongwe wa bongo fleva, Banana  Zoro amesema kiwango kinachoonyeshwa na mastaa wa Simba, kinamwaminisha ubingwa msimu huu unaweza kwenda Msimbazi kwa mara nne mfululizo, licha ya kwamba Yanga ndio inaongoza Ligi Kuu Bara kwa pointi 50.

Yanga hadi sasa imecheza mechi 23, imeshinda 14, imefungwa mmoja dhidi ya Coastal Union na imetoka sare nane, wakati watani wao wa jadi Simba inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi baada ya kucheza mechi 20, imeshinda 14, sare nne na imefungwa michezo miwili, hivyo imejikusanyia pointi 46.

Msanii huyo ambaye ni Simba damu, ameliambia Mwanaspoti Online, leo Jumatatu ya Aprili 5, 2021 kwamba wachezaji wa timu hiyo wapo kwenye kiwango cha juu ambacho, kimewapa imani mashabiki wao kuamini katika ubingwa msimu huu.

Amesema ili kudhihirisha hilo, Simba imeanza kuonyesha makali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika (Caf) ambapo wametinga hatua ya robo fainali, baada ya kuichapa AS Vita ya DR Congo kwa jumla ya mabao 5-1, ugenini ikishinda moja, Uwanja wa Benjamini Mkapa ikifunga mabao 4-1.

"Sizungumzii kishabiki kazi ya Simba inaonekana wazi, ingekuwa ligi ya ndani wengine wangeaanza kujificha kwenye kivuli cha Simba inabebwa, lakini imeshinda nyumbani na ugenini, hilo linathibitisha ubora wao," amesema na ameongeza kuwa;

"Ubora wa Simba umetokana na kikosi kukaa kwa pamoja muda mrefu, baada ya miaka iliopita kupitia changamoto za hapa na pale wakaamua kukaa chini na kujua nini wanapaswa kufanya ili kuwa na timu bora, ndio maana nasema hata kama kuna timu haikubali kiwango cha Simba kwasasa basi itakuwa na lake jambo," amesema.

Advertisement

Mbali na kushangilia mafanikio ya Simba, Banana amewashauri mastaa kutunza heshima wanayopewa na mashabiki wao kwamba imetokana na kazi yao nzuri, hivyo wapambane hadi mwisho wa msimu ili waje wale kwa raha matunda yao.

 "Nipo kwenye muziki najua unapofanya kazi vizuri, ndivyo unavyozidisha ushindani mkali, ndio maana nawashauri wachezaji wa Simba wasibweteke wakijua wanachokifanya kuna timu zinatamani kuwa kama wao,"amesema.

Advertisement