Awilo, Fuse ODG jukwaa moja Tuzo za CAF 2025
Muktasari:
- Wasanii watatu maarufu, Awilo Longomba, Fuse ODG na Douaa Lahyaoui, kila mmoja akiwakilisha kizazi na uelekeo tofauti wa muziki, watapanda jukwaa moja kutoa burudani.
Shirikisho la Soka Afrika (CAF), limetangaza orodha ya wasanii watakaotumbuiza katika hafla ya utoaji Tuzo za CAF 2025, itakayofanyika kesho Jumatano, Novemba 19, 2025 katika Chuo Kikuu cha Mohammed VI Polytechnic (UM6P) kilichopo Rabat nchini Morocco, kuanzia saa 3:00 usiku kwa majira ya Tanzania.
Wasanii watatu maarufu, Awilo Longomba, Fuse ODG na Douaa Lahyaoui, kila mmoja akiwakilisha kizazi na uelekeo tofauti wa muziki, watapanda jukwaa moja kutoa burudani.
Sherehe hizo zinatarajiwa kupata msisimko wa aina yake kupitia Awilo Longomba, gwiji wa soukous kutoka DR Congo, ambaye nyimbo zake zimekuwa maarufu barani kote.
Kwa kazi yake iliyotambuliwa kimataifa na tuzo lukuki, Awilo ameahidi kutumbuiza kwa nguvu ileile inayomtambulisha ikiwa na mchanganyiko wa midundo, dansi na uchezaji wa kuvutia jukwaani.
Miongoni mwa nyimbo zake maarufu ni Moto Pamba, Coupé Bibamba, Gaté Le Coin, Manon, Karolina, Champion, Mondongo, Fidele na Bundele. Uwepo wake unathibitisha nafasi muhimu ya muziki wa Congo katika urithi wa kitamaduni wa Afrika.
Kwa upande wa Fuse ODG ambaye jina lake halisi ni Nana Richard Abiona, ni moja ya wasanii vinara wa muziki wa kisasa wa Afrobeats. Msanii huyu mwenye asili ya Ghana na Uingereza ambaye ni mshindi wa tuzo za MOBO, amejikita kimataifa kupitia ushirikiano na wasanii mbalimbali na juhudi za kuinua sauti za Afro-urban katika ulimwengu wa muziki.
Akiunganisha kwa urahisi mitaa ya Accra na London, Fuse ODG anawakilisha kizazi chenye ubunifu, uwazi na mizizi imara ya utambulisho wa Kiafrika, anatarajiwa kuongeza shangwe katika utoaji tuzo hizo katika usiku unaotolewa heshima kwa wachezaji bora wa soka barani Afrika.
Nyimbo kama Antenna na Azonto zilizotoka mwaka 2013, zilimtambulisha vilivyo msanii huyo ambaye amekuwa maarufu Afrika.
Pia kuna Douaa Lahyaoui, moja ya vipaji vinavyoinukia kwa kasi nchini Morocco, amewavutia mashabiki katika matamasha makubwa ya utamaduni nchini humo. Ametajwa kwa sauti yake yenye upeo mpana na utambulisho wa kisanii ulio bora, akichanganya ladha za Kimoroko na muziki wa kisasa wenye ushawishi wa kimataifa.
Uwepo wake katika Tuzo za CAF 2025 ni ishara ya kizazi kipya cha Wamorocco kinachobeba kwa kujiamini rangi za taifa lao huku kikiungana na sauti za kisasa katika bara zima.