Pedro, Pantev kazi ipo CAF, rekodi zinaongea
Muktasari:
- Yanga itaanza kutupa karata Jumamosi kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco katika mechi ya Kundi B, kabla ya siku inayofuata Simba kushuka Benjamin Mkapa dhidi ya Petro Atletico ya Angola kwa mechi ya Kundi D.
SIMBA na Yanga zipo kambini kwa sasa zikijiandaa na mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku makocha wa timu hizo, Dimitar Pantev na Pedro Goncalves wakikabiliwa na kibarua kizito kulingana na rekodi za makocha waliopita na kuziongoza timu hizo hatua hiyo.
Yanga itaanza kutupa karata Jumamosi kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco katika mechi ya Kundi B, kabla ya siku inayofuata Simba kushuka Benjamin Mkapa dhidi ya Petro Atletico ya Angola kwa mechi ya Kundi D.
Kitu cha kuvutia timu hizo zitashuka uwanjani kuanza kibarua cha mechi hizo za CAF kila moja ikiwa na kocha mpya na zote zinaanzia nyumbani, tofauti na wawakilishi wengine wa Tanzania Azam FC na Singida Black Stars wanaocheza Kombe la Shirikisho wakianzia ugenini.
Katika mechi za raundi ya pili klabu hizo zinabadilishana, Azam na Singida zenyewe zitarudi nyumbani, huku Yanga na Simba zikitaenda ugenini kumalizana na JS Kabylie ya Algeria na Stade Malien ya Mali mtawalia na hapo kuna mziki mnene wanaoenda kukumbana nao makocha hao.
Mechi ya raundi ya tatu, Simba itakuwa Tunisia kucheza dhidi ya Esperance na Yanga ikiwa Misri kuwakabili mabingwa mara 12 wa Afrika, Al Ahly.
Wataalamu wa mambo ya soka, wanaziangalia mechi tatu za makundi kama mwanga wa kutoboa au kufeli kwa timu, hivyo makocha wa Simba na Yanga macho yao yapo hapo.
Yanga inakwenda makundi ikiwa na Pedro, kocha Mreno aliyetambulishwa Oktoba 25, 2025, saa chache baada ya kikosi hicho kufuzu makundi.
Pedro amechukua nafasi ya Romain Folz aliyesitishiwa mkataba pale Yanga baada ya kuiongoza kupitia mechi sita za mashindano msimu huu zikiwamo tatu za Ligi ya Mabingwa Afrika hatua za awali. Kibarua chake kilifikia mwisho Oktoba 18, 2025, Yanga ilipofungwa ugenini na Silver Strikers katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa. Baada ya hapo msaidizi wake, Patrick Mabedi akachukua jukumu la kumalizia mechi ya marudiano na Yanga na kushinda 2-0 na kufuzu makundi.
Kuanzia hapo, Pedro akawa bosi wa benchi la ufundi akiiongoza Yanga kucheza mechi mbili za ligi ambazo zote timu hiyo imeshinda.
Kwa upande wa Simba, Dimitar Pantev akatua kikosini hapo baada ya Fadlu Davids kuachana na timu hiyo alipoiongoza kushinda ugenini bao 1-0 mechi ya kwanza ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Gaborone United.
Tangu Pantev ametua Simba, timu hiyo imecheza mechi tatu za mashindano, ikiwamo moja ya Ligi Kuu na kushinda 2-1 dhidi ya JKT Tanzania.
Pantev amehusika kuivusha Simba kucheza makundi ya Ligi ya Mabingwa alipoiongoza katika mechi mbili, ugenini na nyumbani dhidi ya Nsingizini Hotspurs ya eSwatini. Ilianza na ushindi wa mabao 3-0, kisha kutoka 0-0 Dar.
MTIHANI ULIPO
Msimu huu 2025-2026, inakuwa mara ya pili kwa Yanga na Simba kufuzu pamoja makundi ya Ligi ya Mabingwa. Awali, ilikuwa 2023-2024 na zote ziliishia robo fainali. Pia imeshuhudiwa mara mbili timu hizo zimecheza makundi ya michuano ya CAF kwa msimu mmoja, lakini michuano tofauti. Ilikuwa 2022-2023, Yanga ilishiriki Kombe la Shirikisho na Simba ikiwa Ligi ya Mabingwa, kisha 2024-25, Simba ikawa Kombe la Shirikisho na Yanga Ligi ya Mabingwa.
Rekodi zinaonyesha katika misimu kumi iliyopita ya Yanga na Simba kucheza hatua ya makundi ya michuano ya CAF tangu 2016, hazikuwa na matokeo mazuri kwa mechi tatu za kwanza, hivyo Pedro na Pantev wanapaswa kuvunja rekodi hiyo mbaya.
Simba katika kipindi hicho tayari imecheza makundi mara sita huku msimu huu ikiwa ya saba, imeshuhudiwa ikitoboa hadi robo fainali, kabla ya msimu uliopita 2024-2025 kufika fainali. Haijawahi kuishia makundi. Huu ni mtihani wa kwanza kwa Pantev anapaswa kuushinda.
Kwa upande wa Yanga, hii ni mara ya sita inakwenda kucheza makundi ya CAF, katika mara tano zilizopita, tatu imeishia makundi, huku moja ikikwamia robo fainali na nyingine ikienda hadi fainali.
Simba katika mara saba za kufuzu makundi CAF, mbili Shirikisho na tano Ligi ya Mabingwa. Takwimu zipo hivi kwa Ligi ya Mabingwa ilitinga 2018-2019, 2020-2021, 2022-2023, 2023-2024 na 2025-2026, huku kwa Kombe la Shirikisho ni; 2021-2022 na 2024-2025.
Yanga mara zake sita za kufuzu makundi CAF, tatu Ligi ya Mabingwa na tatu Shirikisho. Hali ipo hivi; Kombe la Shirikisho ilicheza 2016, 2018 na 2022-2023, wakati kwa Ligi ya Mabingwa ni 2023-2024, 2024-2025 na 2025-2026.
MZIKI MSIMU HUU
Msimu huu, Yanga iliyopangwa Kundi B na timu za Al Ahly (Misri), AS FAR (Morocco), JS Kabylie (Algeria), itaanzia nyumbani ambapo imetangaza kuutumia Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Zanzibar. Mechi hiyo itachezwa Jumamosi hii Novemba 22, 2025 dhidi ya AS FAR.
Baada ya hapo, itaifuata JS Kabylie kati ya Novemba 28 na 30, mwaka huu, kisha kutakuwa na mapumziko ya muda mrefu kupisha michuano ya AFCON.
Kati ya Januari 23 na 25, 2025, Yanga itaenda Misri kukabiliana na Al Ahly, kisha itarejea Dar kurudiana na wababe hao wa Afrika, mechi ikipangwa kuchezwa kati ya Januari 30 na Februari 1, 2026. Itasafiri kwenda Morocco kuikabili AS FAR kati ya Februari 6 na 8, 2026. Itamalizia nyumbani hatua ya makundi kwa kuiribisha JS Kabylie kati ya Februari 13 na 15, 2025.
Kwa Simba iliyopo Kundi D, msimu huu inaanzia nyumbani dhidi ya Petro Atletico, mechi ikichezwa Novemba 23, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambapo ndipo ilipo ngome ya Wekundu hao wa Msimbazi.
Kati ya Novemba 28-30 Simba itakuwa Mali kukabiliana na Stade Malien, kisha kati ya Januari 23-25, itaenda Tunisia kukabiliana na Esperance, kisha timu hizo zitarudiana kati ya Januari 30 na Februari 1, 2026 jijini Dar es Salaam.
Kati ya Februari 6-8, 2026, Simba itakuwa Angola kuivaa Petro Atletico, itahitimisha makundi nyumbani kati ya Februari 13-15, 2026 kuikaribisha Stade Malien.
REKODI YANGA MECHI 3 ZA KWANZA
Mwaka 2016 katika Kombe la Shirikisho, Yanga ikifundishwa na Mholanzi Hans van der Pluijm, ilipangwa Kundi A na TP Mazembe ya DR Congo, Mo Bejaia (Algeria) na Medeama (Ghana). Wawakilishi hao wa Tanzania wakamaliza mkiani kwa pointi nne baada ya kushinda mechi moja, sare moja na kupoteza nne.
Katika mechi tatu za kwanza, Yanga ilikusanya pointi moja tu, ilianza kwa kufunga 1-0 na MO Bejaia (ugenini), kisha nyumbani ikapokea kichapo kama hicho kutoka kwa TP Mazembe, kabla ya kuambulia sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Medeama.
Kutoka hapo, ikafungwa 3-1 na Medeama (ugenini), ikashinda 1-0 nyumbani dhidi ya MO Bejaia na kupoteza ugenini 3-1 dhidi ya TP Mazembe.
Mwaka 2018 katika Kombe la Shirikisho, Yanga ilipangwa Kundi D, mechi mbili za kwanza dhidi ya USM Alger iliyowanyoa ugenini 4-0 na ile ya 0-0 nyumbani dhidi ya Rayon Sports, kikosi kiliongozwa na makocha wasaidizi Shadrack Nsajigwa na Noel Mwandila, baada ya kocha mkuu, George Lwandamina kuondoka wakati Yanga ikipambania kucheza makundi.
Ikiwa Kundi D, Yanga ilimaliza mkiani tena kwa pointi nne, ikipata matokeo kama ilivyokuwa mwaka 2016, ikishinda moja, sare moja na kupoteza nne.
Mechi tatu za kwanza iliambulia pointi moja, ilipoanza kufungwa 4-0 na USM Alger, kisha 0-0 na Rayon Sports na kichapo kingine cha 4-0 kwa Gor Mahia. Kumbuka mechi hiyo dhidi ya Gor Mahia, timu iliongozwa na Kocha Mkongomani, Mwinyi Zahera aliyekabidhiwa kukiongoza kikosi akiwa kocha mkuu.
Yanga ikafungwa tena nyumbani 2-3 na Gor Mahia, ikashinda nyumbani 2-1 na USM Alger, ikamalizia na kichapo cha 1-0 kutoka kwa Rayon Sports.
Kutokea hapo, Yanga ikakaa muda mrefu bila ya kucheza makundi ya CAF, ikaja kufanya balaa msimu wa 2022-23 katika Kombe la Shirikisho ilipokwenda hadi fainali na kupoteza kwa kanuni ya bao la ugenini kufuatia matokeo ya jumla kuwa 2-2 dhidi ya USM Alger. Nyumbani ilifungwa 2-1, ugenini ikashinda 1-0.
Msimu huo, Yanga ilianzia Ligi ya Mabingwa Afrika, ilipofeli katika kuwania kufuzu makundi, ikaangukia mtoano Shirikisho na kufuzu makundi kibabe chini ya Kocha Nasreddine Nabi.
Ikapangwa Kundi D, ikamaliza kinara kwa kukusanya pointi 13, hata hivyo, hadithi ilikuwa ileile mechi tatu za kwanza ikapata matokeo ya aina tatu. Ilianza na kichapo ugenini cha mabao 2-0 dhidi ya US Monastir, kisha nyumbani ikashinda 3-1 dhidi ya TP Mazembe, ikaenda ugenini ikaambulia sare ya 1-1 kwa Real Bamako.
Kutoka hapo, ikatembeza dozi kwa wapinzani wake wote ikianzia nyumbani mechi mbili mfululizo ikaichapa Real Bamako (2-0) na US Monastir (2-0), kisha ikamalizia ugenini kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya TP Mazembe.
Msimu wa 2023-2024 katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga iliongozwa na kocha Miguel Gamondi ikiwa ni mara yake ya kwanza kikosini hapo. Gamondi akaiwezesha Yanga kufuzu kwa mara ya kwanza makundi ya Ligi ya Mabingwa baada ya kupita takribani miaka 25. Yanga ilipangwa Kundi D, ikamaliza nafasi ya pili kwa pointi nane ikiwa nyuma ya Al Ahly.
Mechi tatu za kwanza, Yanga ilikusanya pointi tatu, haikupoteza mechi, ikishinda moja na sare mbili. Ilianza na kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa CR Belouizdad, kisha sare za 1-1 mfululizo dhidi ya Al Ahly (nyumbani) na Medeama (ugenini).
Ikashinda nyumbani 3-0 dhidi ya Medeama, pia ikaikaribisha CR Belouizdad na kuipa kichapo cha mabao 4-0, ikamaliza makundi kwa kufungwa 1-0 na Al Ahly.
Msimu uliopita, Gamondi aliiwezesha Yanga kucheza tena makundi Ligi ya Mabingwa, lakini hakwenda na timu hiyo, yakafanyika mabadiliko ya benchi la ufundi, timu ikaongozwa na Mjerumani, Sead Ramovic. Yanga ilipangwa Kundi A, ikamaliza nafasi ya tatu kwa kukusanya pointi nane, huku Al Hilal na MC Alger zikiwa juu yake.
Yanga ilifungwa mechi mbili mfululizo za kwanza kwa kichapo cha 2-0, ilianza nyumbani dhidi ya Al Hilal, kisha ugenini kwa MC Alger. Mechi ya tatu ikatoka 1-1 na TP Mazembe. Katika mechi hizo tatu, ikakusanya pointi moja pekee.
Baada ya hapo ikashinda 3-1 nyumbani dhidi ya TP Mazembe, ikaenda kushinda ugenini 1-0 dhidi ya Al Hilal na kumalizia nyumbani kwa matokeo ya 0-0 dhidi ya MC Alger. Safari ikaishia hapo.
SIMBA HALI IPOJE?
Msimu wa 2018-2019, Mbelgiji Patrick Aussems alikata kiu ya Wanasimba kwa kuifikisha timu hiyo makundi Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya muda mrefu, hakuishia hapo, timu ilikwenda hadi robo fainali.
Hatua ya makundi, Simba ilipangwa Kundi D, ikamaliza nafasi ya pili na pointi tisa nyuma ya vinara Al-Ahly iliyokuwa na kumi. Tofauti ni pointi moja tu.
Licha ya Simba kuanza na ushindi mzuri wa mabao 3-0 nyumbani dhidi ya JS Saoura, lakini ikakumbana na vichapo vikubwa viwili mfululizo vya kufanana mabao 5-0 dhidi ya AS Vita Club na Al-Ahly, zote ikicheza ugenini.
Hata hivyo, msimu huo Aussems alikuwa na mbinu zake kali, zikambeba kwani alihakikisha nyumbani haachi pointi hata moja, akaichapa Al Ahly 1-0, akaenda ugenini kufungwa 2-0 na JS Saoura, mwisho akaiduwaza AS Vita Club kwa mabao 2-1.
Didier Gomes Da Rosa anabaki kuwa kocha bora kitakwimu ndani ya Simba katika hatua ya makundi katika mechi tatu za kwanza kwani aliiongoza timu hiyo msimu wa 2020-21 kushiriki Ligi ya Mabingwa na kumaliza kinara kwa kukusanya pointi 13 katika Kundi A.
Pointi hizo zilitokana na kushinda mechi mbili za kwanza dhidi ya AS Vita Club bao 1-0 ugenini, kisha ushindi kama huo nyumbani dhidi ya Al Ahly. Mechi ya tatu ugenini ikaisha kwa matokeo ya 0-0 dhidi ya Al Merrikh ambayo Simba ilikuja kuikanda nyumbani 3-0. Ikainyanyasa AS Vita Club kwa kichapo cha mabao 4-1. Mechi ya mwisho ndio pekee Simba ilipoteza kwa bao 1-0 mbele ya Al Ahly.
Gomes aliichukua Simba kuanzia makundi ikiwa ni baada ya Sven Vandenbroeck kuondoka alipomaliza kuifikisha hapo kutoka hatua za awali.
Pablo Franco Martin naye alitembelea njia za Gomes kwa kushinda mechi ya kwanza msimu wa 2021-2022 kunako Kombe la Shirikisho alipoichapa ASEC Mimosas mabao 3-1 nyumbani. Hata hivyo, alikuja kutoka sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya US Gendarmerie ugenini na kufungwa ugenini 2-0 dhidi ya RS Berkane. Msimu huo Simba ilimaliza nafasi ya pili katika Kundi D ikikusanya pointi 10 sawa na vinara RS Berkane.
Ukiweka kando mechi hizo tatu za kwanza, Simba ilikuja kulipa kisasi nyumbani kwa kuifunga RS Berkane 1-0, kisha ikafungwa 3-0 na ASEC Mimosas ugenini, ikamalizia nyumbani na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya US Gendarmerie.
Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’ katika msimu wa 2022-23 Simba ikiwa Ligi ya Mabingwa, aliiongoza timu hiyo kumaliza nafasi pili Kundi C na pointi tisa nyuma ya vinara Raja Club Athletic iliyokusanya pointi 16.
Simba ilianza kwa kufungwa mechi mbili mfululizo dhidi ya Horoya 1-0 ugenini, kisha 3-0 nyumbani na Raja CA. Ikaenda ugenini kushinda 1-0 dhidi ya Vipers, pia ziliporudiana, Simba ikashinda tena nyumbani 1-0. Ikaikaribisha tena Horoya na kuipa kichapo kikubwa cha mabao 7-0. Ikamaliza kundi kwa kufungwa 3-1 na Raja.
Msimu wa 2023-2024, Simba ilimaliza nafasi ya pili Kundi B na pointi zake tisa nyuma ya vinara ASEC Mimosas lakini haikuwa na matokeo mazuri mechi tatu za kwanza ikitoka sare mbili mfululizo, kisha ikachapwa.
Kocha Abdelhak Benchikha ndiye aliiongoza timu hiyo katika makundi Ligi ya Mabingwa msimu wa 2023-2024, alitua kikosini hapo Desemba 2, 2023 kuchukua nafasi ya Robertinho, aliyeondoka Aprili 29, 2024, timu ikiishia robo fainali.
Simba ilianza mechi ya makundi dhidi ya ASEC Mimosas kwa sare ya 1-1 nyumbani, kikosi kiliongozwa na Daniel Cadena ambaye alichukua jukumu hilo baada ya Robertinho kuondoka. Kumbuka Cadena alikuwa kocha wa makipa kikosini hapo.
Mechi iliyofuata, Benchikha akakaa benchini na kushuhudia matokeo ya 0-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy, ugenini. Kisha kichapo cha bao 1-0 ugenini kutoka kwa Wydad.
Simba ikaja kulipa kisasi kwa Wydad nyumbani iliposhinda 2-0, ukiwa ni ushindi wa kwanza Benchikha kuupata kimataifa na kufufua matumaini. Kisha ikatoka tena 0-0 na ASEC Mimosas, lakini ikahitimisha makundi kibabe kwa ushindi mnono wa mabao 6-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy.
Msimu uliopita 2024-2025 wa kihistoria kwa Simba kufuatia kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Simba iliyokuwa Kundi A, nyota njema ilianza kuonekana kwa kumaliza kinara wa kundi na pointi zake 13, ikiwapiga bao Waarabu wawili, CS Constantine waliomaliza katika nafasi ya pili na pointi 12. Wengine ni CS Sfaxien waliokuwa mkiani kwa pointi tatu. Pia kulikuwa na Bravos ya Angola ikikamata nafasi ya tatu kwa pointi saba.
Simba ilianza na ushindi wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Bravos, ikaja kufungwa ugenini 2-1 na Constantine, kisha ikashinda 2-1 nyumbani dhidi ya CS Sfaxien. Ikaenda kwa CS Sfaxien na kushinda 1-0, kisha ikatoka 1-1 ugenini dhidi ya Bravos, ikamalizia nyumbani na ushindi wa 2-0 dhidi ya Constantine. Fadlu naye anabaki kuwa miongoni mwa makocha walioanza makundi kwa ushindi.
KISIKI CHA KUKIVUKA
Kwa takwimu hizo, Yanga inaonesha haijawahi kushinda mechi ya kwanza ya makundi katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, wakati Simba ikishinda mara tatu kupitia makocha Didier Gomes Da Rosa, Pablo Franco Martin na Fadlu Davids, hata hivyo, Gomes ameonekana kuwa na takwimu nzuri zaidi kwani mechi tatu za kwanza, alishinda mbili na sare moja.
Hapa Pedro na Pantev wana kisiki cha kukivuka, lakini pia, kuhakikisha mechi tatu za kwanza hawadondoshi pointi yoyote kutokana na watangulizi wao hakuna hata mmoja aliyeweza kufanya hivyo.
Jambo jingine, Pantev ana mtihani wa kuhakikisha Simba haikwami makundi kwani tangu mwaka 2018, imevuka hapo na kucheza robo fainali, huku msimu uliopita Fadlu akiweka rekodi yake kwa kuipeleka Simba fainali ya CAF kwa mara ya kwanza baada ya takribani miaka 30 kupita.
Kwa Pedro, unaweza kufananisha na ilivyokuwa msimu uliopita Yanga ilipokuwa ikinolewa na Ramovic aliyeikuta timu tayari imefuzu makundi, akashindwa kuivusha zaidi. Hakudumu sana, akaondoka. Safari hii, Pedro kibarua cha kwanza kimataifa ni hatua ya makundi. Atafanyaje? Tusubiri tuone.