AliKiba, Samatta kusaidia watoto njiti Kibiti na Kigoma

Msanii Ally Saleh maarufu Ali Kiba na mchezaji mpira anayekipiga kimataifa, Samatta Mbwana, wanataraji kukusanya fedha kupitia mechi ya hisani kwa ajili ya kukusanya fedha kwa ajili ya kusaidia matibabu ya watoto waliozaliwa njiti mikoa ya Kibiti na Kigoma
Wawili hao watafanya jambo hilo kupitia taaisi yao ya Samakiba Foundation kwa kushirikiana na taasisi ya Doris Mollel Foundation ambayo kwa miaka saba imekuwa ikijishughilisha na kutoa misaada mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia watoto hao.
Samakiba Foundation, ni taasisi isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa mwaka 2020 na Mbwana Samatta na Alikiba, ikiwa na lengo la kusaidia wale wanaohitaji ndani ya jamii
Akizungumza leo katika kuzindua kampeni hiyo waliyoipa jina la' Nifuate na Upendo wa Zambarau 2023', Ali Kiba amesema hii ni awamu ya sita ya mechi hizo za hisani ambapo kwa mwaka huu wanaungana na Doris Mollel Foundation.
"Taasisi ya Doris Mollel imekuwa ikisaidia Serikali kutoa huduma kwa watoto njiti na pia kusaidia katika utoaji wa vifaa vya afya maalum vinavyotumika kuokoa maisha ya watoto waliozaliwa kabla ya wakati hivyo mwaka tumeona tuungane nao katika kuwasaidia watoto wetu hawa ,"amesema Kiba.
Msanii huyo amebainishaa kuwa katika kuelekea kilele cha kampeni hiyo ya Nifuate, kutakuwa na Bonanza mbili za mitaani, zilizopangwa kufanyika Juni 10 na 11, 2023 maeneo ya Kariakoo na Mbagala huku mechi ya hisani ikiwa imepangwa kufanyika Juni 17,2023 viwanja vya Chamazi Azam Complex.
Kupitia viingilio ambavyo vitakuwa kati ya Sh3000 na Sh5000 ,Ali Kiba amesema yatatoa nafasi kwa wapenzi wa mpira wa miguu kuhudhuria pamoja na kuchangia fedha zitakazo saidia kuokoa maisha ya watoto hao.
Pia katika ukusanyaji fedha huo, kutauzwa jezi za Team Kiba na Team Samatta ambapo kwa wauzaji wa jumla watauziwa kwa Sh40,000 na kwa wale wa mtaani watauziwa Sh45,000.
Kwa upande wake Doris Mollel, amesema katika kampeni hiyo wamechagua mikoa ya Kigoma na Kibiti kwa kuwa ndio ina idadi kubwa ya kuzaliwa kwa watoto hao njiti ukilinganisha na mikoa mingine.
"Moja ya sababu inayochangia mikoa hiii kuw na idadi kubwa ya watoto hao ni elimu duni kuhusu tatizo hilo ambapo kupitia Samata na Kiba watawezesha kuwafikiwa watu wengi zaidi katika utoaji elimu na pia fedha zitakazopatikana zitatumika kununua vifaa na kuanzisha utoaji wa huduma katika vituo vya afya badala ya kufata huduma hiyo hospitali za rufaa.
Rehema Salim ambaye ni meneja mahusiano kampuni ya Bakhresa, amesema katika kuunga mkono kampeni hiyo pamoja na kutoa maji ya kunywa kwa wachezaji pia watajitolea uwanja wa Chamazi kwa ajili ya kuchezwa mechi hiyo.
Rehema amesema wamekuwa wakijitoa katika masuala mbalimbali kama njia ya kurudisha kwa jamii.
"Watoto njiti hawa niwa kwetu wote sote hivyo tumeona tujitoe nasi ikiwepo kushiriki katika harambee ambayo itafanyika hivi karibuni,"amesema Rehema.