Alichosema Waziri Sonyo kabla ya kuisha mechi ya Simba Vs Al Ahly

Sanit Sonyo ambaye ni kaka wa mwanamuziki Waziri Sonyo, ameeleza alichozungumza na Waziri muda mfupi kabla ya kuisha kwa mechi ya Simba na Al Ahly ya nchini Misri.
Sonyo ambaye alikuwa shabiki wa Yanga kindakindaki, alifikwa na umauti akiwa  kwao Kibaha, mkoani Pwani muda mfupi baada ya kutoka kutazama mpira wakati timu hizo zikikipiga pale uwanja wa Mkapa.
Chanzo cha kifo chake kinaelezwa kuwa ni ugonjwa wa moyo na shinikizo la damu, magonjwa yaliyokuwa yakimsumbua kwa muda mrefu.
Akizungumza na Mwanaspoti kaka huyo alisema muda mfupi kabla Sonyo hajafikwa na umauti, alimpigia simu kipindi cha mapumziko wakati wa mechi hiyo iliyokuwa inachezwa uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam huku Simba ikiongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Luis Miquissone dakika ya 30 , na kumueleza kwamba anaona kila  dalili za Simba kuibuka washindi katika Mtanange huo.


“Mara ya mwisho kuzungumza na mdogo wangu ilikuwa jana wakati Simba na Al Ahly zilipokuwa zinacheza na ilikuwa kipindi cha mapumziko baada ya dakika 45 za mwanzo kuisha tena simu hiyo alinipigia mwenyewe na kuniambia kaka hapa naona kila dalili za Simba kuibuka washindi kwa namna wanavyocheza mpira mzuri.
“Pia aliahidi kwamba angenipigia baadaye lakini ndio hivyo sikupata bahati ya kuzungumza naye tena mpaka alipofikwa na umauti, imeniuma sana,”alisema kaka huyo.
Akizungumzia dakika za mwisho za msanii huyo zilivyokuwa alidondoka mlangoni baada ya kulalamika kuishiwa pumzi nah ii ilikuwa baada ya kutoka kutazama mpira wa simba na Al Ahly kupitia runinga maeneo ya jirani na nyumba. majira ya saa 2;30.
 “Baada ya tukio hilo aliwaomba wadogo zangu wampatie dawa zake, na wakati dada yetu mmoja anaenda kumchukulia alivyorudi ndio akamkuta kalala moja kwa moja na kutonyanyuka tena,” alisema Sanit.
Alisema baadaye waliamua kuuepeleka mwili wa msanii huyo kwenda kuihifadhi hospitali ya Tumbi na amezikwa jana  katika makaburi ya Air Msae wilayani humo Kibaha.
Waziri Sonyo Aliyewahi kufanya kazi katika bendi mbalimbali ikiwemo Tanzania One Theatre, Tamtam na Chuchu Sound na moja ya kibao ambacho aliwahi kukitunga na kuwika ni ‘Masimango’ akiwa TOT na mpaka anafariki alikuwa akifanya kazi na bendi ya Kiteshe yenye makazi yake Kibaha Mailimoja.
Chama cha Muziki wa dansi kupitia katibu wake, Hassan Msumari, alisema watamkumbuka Waziri Sonyo kama moja ya wasanii wa kizazi kipya katika muziki wa dansi walioleta mapinduzi na kuufanya muziki huo kuwa wa kisasa