Achana na gari, Harmonize kamnunulia Kajala nyumba

Sunday February 28 2021
harmonizee pic
By Nasra Abdallah

‘Couple’ kati ya msanii wa filamu, Kajala Masanja na mkali wa ngoma ya Uno, Harmonize inazidi kunoga na sasa ni mwendo wa mazawadi kila uchwao.

Wawili hao walianika rasmi mahusiano yao Februari 14, mwaka huu, kwenye sikukuu ya Wapendanao na kuibua gumzo huko mitandoni na kwa wafuatiliaji wa masuala ya burudani kwa ujumla.

Pia katika hafla ya chakula cha usiku iliyoandaliwa na benki ya CRDB hivi karibuni ambapo Harmonize ni balozi wao, alimtambalisha Kajala kama mke wake kwa kumuita jukwaani ili watu wamuone.

Juzi kati wapendano hao tena wakaja na jipya baada ya kusambaa kwa picha zikimuonyesha Harmonize akimkabidhi funguo za gari Kajala ambaye wakati huo alikuwa mazoezini.

Gari hiyo aina ya Crown Athelete inaelezwa kuwa thamani yake ni kati ya Sh12 milioni hadi Sh13 milioni.

Hata hivyo, mtu wa karibu na msani huyo, alisema ukiachana na gari, Kajala tayari amenunuliwa mjengo eneo la uwekezaji wa nyumba za Himidu City zilizopo maeneo ya Kigamboni, Dar es Salaam ambapo nyumba zake zinaelezwa huuzwa kati ya Sh114 milioni hadi Sh260 milioni.

Advertisement

“Hee nyie vipi mnashangaa zawadi ya gari kwa Kajala, jamaa anampenda sana huyu mwanamke, tayari amemnunulia na nyumba na nimeshuhudiwa kwa macho yangu akikabidhiwa hadi hati yenye jina lake,” alisema mtoa taarifa huyo na kuomba jina lake kutotajwa gazetini.

Couple hii imekuwa ikizungumzwa sana kutokana na historia ya mahusiano kati yao kwani Harmonize kabla ya kumuoa Sarah, raia wa Italia na kuachana naye, huko nyuma aliwahi kuwa katika mahusiano na Jacquiline Wolper ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa Kajala.

Pia jingine ni hivi karibuni baada ya kusambaa kwa video ikiwaonyesha msanii Rayvany kutoka lebo ya WCB kuwa katika mahusiano na Paula ambaye ni mtoto wa Kajala, hadi kufika hatua ya kupelekana Polisi, lebo ya WCB hususani mmoja wa kiongozi wake kuonyesha bifu la waziwazi na msanii, Harmonize alijitokeza na kuandika waraka mtandaoni akimuonyaRayvany.

Harmonize mwenyewe amewahi kuandika kuwa huenda yote yanayofanyika kwa sasa dhidi ya Kajala ni kutokana na kuwa na uhusiano naye, hivyo wanatumia kama fimbo kumchapa.

Advertisement