Abdalla Hemba; Nyota wa Sikinde anayepitia safari ya maumivu, matumaini
Muktasari:
- MSANII wa muziki wa dansi kutoka bendi ya Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde Ngoma ya Ukaye’, Abdalla Hemba amefunguka kwa kina kuhusu changamoto kubwa ya kiafya inayomkabili na namna alivyoanza kuugua ghafla na safari ndefu ya matibabu aliyopitia hadi sasa.
MSANII wa muziki wa dansi kutoka bendi ya Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde Ngoma ya Ukaye’, Abdalla Hemba amefunguka kwa kina kuhusu changamoto kubwa ya kiafya inayomkabili na namna alivyoanza kuugua ghafla na safari ndefu ya matibabu aliyopitia hadi sasa.
Katika mahojiano maalum na Mwanaspoti, msanii huyo anasimulia maumivu, matumaini na mapambano yake ya kurejea katika hali ya kawaida.
Alivyoanza kuugua
Anasema safari ya ugonjwa wake ilianza Machi 22, 2026 alipopimwa na kugundulika ana maradhi ya malaria na UTI.
Anasema ilibidi alazwe Hospitali ya Malawi iliyopo Kiwalani, jijini Dar es salaam, kwa siku moja kabla ya kuruhusiwa kurejea nyumbani kwa masharti ya kufuatilia matibabu kwa siku mbili, hata hivyo, hali yake haikuimarika.
“Nilianza kuumwa ghafla, wakagundua ni malaria na UTI. Nikalazwa hospitali ya Malawi siku moja, nikarudi nyumbani lakini hali ikazidi kuwa mbaya zaidi mchana wake, ilibidi wanipeleke tena hospitali,” anasimulia.
Baada ya hali yake kuwa mbaya zaidi, alipelekwa Hospitali ya Temeke, jijini Dar es Salaam, ambako alilazwa kwa siku tatu mfululizo mwezi huu Aprili, hata hivyo, licha ya juhudi za madaktari, hali yake iliendelea kuwa tete na kuzua hofu kwa ndugu na jamaa waliokuwa wakimzunguka.
“Nilipofika Temeke walinilaza siku tatu, kwa kweli hali ilikuwa si nzuri, nguvu zilikuwa zimepungua kabisa na nilihisi mwili unazidi kudhoofika kila siku,” anasema.
Magonjwa mengine yaibuka
Katika hali isiyotarajiwa, msanii huyo aligundulika pia kuwa na magonjwa mengine ikiwemo kisukari, presha (BP) na nimonia, jambo lililoongeza ugumu wa matibabu yake.
Anasema alipelekwa hospitali ambako aliwekewa dripu kwa muda kabla ya kuruhusiwa kurejea nyumbani kuendelea na matibabu.
“Nilipimwa zaidi wakagundua nina kisukari, BP, nimonia pamoja na TB, Niliwekewa dripu hospitali hadi jioni, kisha nikarudi nyumbani, kwa sasa naendelea kutumia dawa za BP na kisukari pamoja na TB na ugonjwa huu unakuja na kuondoka kila nikipima,” anafafanua kwa huzuni.
Kupoteza nguvu na kurejea taratibu
Athari za magonjwa hayo zilimwacha akiwa hana nguvu kabisa, hasa miguuni, hali iliyomfanya ashindwe kutembea kwa muda.
Hata hivyo, kuna mwanga wa matumaini baada ya kuanza kupata nafuu taratibu.
“Miguu yangu ilikuwa haina nguvu kabisa, sikuweza hata kutembea. Lakini jana tarehe 16, 2026 nimeanza kutembea kidogo, japo bado si kwa nguvu ile ya zamani,” anasema kwa sauti ya matumaini.
Changamoto ya kula, kwikwi isiyokoma
licha ya dalili nyingine kupungua, bado anakumbwa na changamoto kubwa ya kula na kila anapokula hutapika, hali inayomdhoofisha zaidi.
Pia alikuwa akisumbuliwa na kwikwi kwa muda mrefu tangu ahamie kwa kaka yake mkubwa, Ramadhani Hemba, anayeishi Kiwalani, eneo la Dingu Bita.
“Kula ndiyo changamoto kubwa, nikila tu natapika. Pia nilikuwa na kwikwi muda mrefu tangu nimehamia kwa kaka yangu, lakini kuanzia jana imeanza kupungua japokuwa bado inakuja na kuondoka,” anasema.
Matumaini mapya na ratiba ya matibabu
kwa sasa, msanii huyo anaishi kwa kaka yake akiendelea kupata matibabu na uangalizi wa karibu, ameweka wazi anapaswa kwenda hospitali ya Malawi kila Jumanne kwa kipindi cha miezi sita kwa ufuatiliaji wa afya yake.
Licha ya hali ngumu aliyopitia, bado ana matumaini ya kupona na kurejea tena jukwaani kuwaburudisha mashabiki wake.
“Najua si safari rahisi, lakini naamini nitapona, naendelea na matibabu kila Jumanne hospitali ya Malawi kwa miezi sita. Ninachohitaji sasa ni dua na sapoti ya mashabiki wangu,” anahitimisha kwa matumaini makubwa.