Wasanii wa Bongo Fleva wakali wa muziki wa Sauzi

WAKATI muziki wa Amapiano ukitamba Bongo kwa sasa, jikumbushe kuwa muziki huo wenye asili ya Afrika Kusini sio wa kwanza kuvuma Tanzania. Kabla ya Amapiano, miziki mingine kutoka bondeni kwa Madiba kama vile Kwaito ilikuwa gumzo kiasi kwamba hata wasanii wetu waliichangamkia na kuimba sana kama walivyouchangamkia muziki wa Amapiano kwa sasa.

Hata hivyo, licha ya kwamba kila miziki ya namna hiyo ‘inapotrendi’ nchini wasanii wa Bongo Fleva hukimbilia studio kuiimba. Bado ni wasanii wachache tu wameonekana kuimudu zaidi kwani kila wakitoa ngoma inakuwa jiwe la uhakika.

Katika makala haya, Mwanaspoti linakuchambulia wasanii wachache wa Tanzania ambao wamefanikiwa kuikamata mitaa kwa kuimba muziki wenye asili ya Afrika Kusini.


SUMA LEE

Mwishoni mwa miaka ya 2000 gemu ilimkataa staa huyo kutoka mji wa Tanga. Ilikuwa kila ngoma anayoachia haitambi kama ilivyokuwa enzi zake wakati anatoa nyimbo kama Chungwa au enzi yupo na Hayati Cpwaa kwenye kundi la Parklane.

Hali ikaendelea hivyo na ikafikia hatua Suma Lee akawa kama amefulia, akapotea kwenye gemu, akakaa kwa zaidi ya miaka mitatu bila kutoa ngoma. Mpaka 2011 aliporudi mjini kwa nguvu ya ajabu kwa wimbo wa Hakunaga ambao uliimbwa kwa mtindo wa Kwaito.

Wimbo wa Hakunaga ulikuwa ni mkubwa, ukamjengea Suma Lee madaraja yaliyovunjika awali na kumrudisha kwenye chati. Baada ya hapo, karibu ngoma zote za Suma Lee ambaye jina lake kamili ni Ismail Thabit aliziimba kwa mtindo wa Kwaito.

Hata licha ya kukubalika sana na Kwaito zake, 2016 staa huyo alitangaza kuachana na Bongofleva kwa kile alichoeleza kuwa ameamua kujikita katika masuala ya imani. Kwa sasa anaimba Kaswida.


MADEE

‘Rais huyu wa Manzese’ ni staa mwingine aliyeutawala muziki wa Kwaito kipindi unabamba. Mwaka 2013 aliachia wimbo wa kwanza unaoitwa Pombe Yangu ambao uliikamata mitaa vibaya mno na kumfanya kuwa mfalme wa kwaito Bongo.

Mafanikio makubwa aliyoyapata Madee kupitia wimbo huo yalimzuia kubadilisha aina ya muziki kwani karibu ngoma zake zote zilizofuata baada ya Pombe Yangu aliziimba kwa mtindo huo. Wimbo kama vile Tema Mate Tuwachape, Ni Sheeda. Inaonyesha Madee bado ana mapenzi mkubwa na miziki ya Afrika Kusini kwani 2018, kabla hata muziki wa Kwaito haujaanza kuwa maarufu sana Tanzania, yeye tayari alishaachia wimbo unaoitwa Joka la Kibisa.


HARMONIZE

Wasanii wengi wanafanya Amapiano kwa sasa, lakini msanii na bosi wa lebo ya Konde Gang, Harmonize anaonekana kunogewa zaidi na muziki huo mpaka amefikia hatua ya kujipa jina la Mfalme wa Amapiano.

Hadi sasa Harmonize anashikilia rekodi ya kuwa msanii wa Bongofleva aliyeachia nyimbo nyingi za Amapiano akiwa na zaidi ya ngoma tano alizoimba kwa mtindo huo ikiwemo Sadakale, Anajikosha, Ticha, Mang’dakiwe Remix na Kilofeshe. Kinachompa jeuri Harmonize kuendelea kukomalia muziki huo ni ukweli kwamba ngoma zake hizo zimekuwa zikifanya vizuri mtaani na kwenye majukwaa ya kuuza na kusikiliza muziki mtandaoni.


MARIOO

Mkali huyu wa ngoma za kulalamika ni mmoja wa wasanii wa Bongofleva walioichangamkia Amapiano mwanzoni kabisa. Wimbo wa kwanza wa Amapiano wa Marioo unaitwa Anyinya na aliuachia 2019.

Tangu aachie Anyinya, Marioo ameonekana kunogewa na muziki huo lakini pia kuumudu vizuri kwani nusu ya nyimbo zote alizotoa baada ya Anyinya ameziimba kwa mtindo wa Kwaito. Novemba mwaka jana aliachia Mama Amina aliomshirikisha Shoo Madjozi na Bontle Smith kutoka Afrika Kusini wakati wiki tatu zilizopita aliachia ngoma inayoitwa Beer Tamu.


WENGINE

Kuna wasanii wengine wakubwa ambao wamejaribu aina hii ya muziki na ngoma zao zikabamba ingawa wenyewe hawajaufanya kwa sana kama wasanii tajwa hapo juu. Ngoma kama vile Iyo ya Diamond, Chawa ya Whozu, Mapopo ya Damian Soul, Amapiano ya Baba Levo zingine.