TUONGEE KISHKAJI: Hatimaye Jay Melody amepata mganga mzuri

TUONGEE KISHKAJI: Hatimaye Jay Melody amepata mganga mzuri

ZAMANI wakati Jay Melody anatoa ngoma zake kama vile Goroka nilikuwa nawaambia wanangu, ‘Huyu dogo anajua kuandika, anajua kuimba, ana sauti ya kuimba, anawajua maprodyuza kiasi kwamba anaweza kuingia studio muda wowote na kurekodi na kama haitoshi ni bishoo.”

Yaani ana kila kitu anachotakiwa kuwa nacho msanii mkali wa muziki wa Bongofleva ili atoboe, lakini mbona hatoboi, mbona hawi maarufu?” Jamaa yangu mmoja akanijibu, “Bado hajapata mganga mzuri.”

Leo hii tunavyozungumza Jay Melody amekuwa moja ya wasanii pendwa sana Bongo, anatrend ile mbaya, ukiingia kwenye mitandao ya kijamii kama Tik Tok utajikuta unalazimishwa kusikiliza wimbo wake wa Nakupenda utake usitake.

Kila mtu anajirekodi akiimba Nakupenda, kila MC anaposti video ya kwenye harusi watu wakicheza Nakupenda. Na hiyo ni sawa na kusema kwamba, hatimaye mdogo wetu kapata mganga mzuri, mambo yanakwenda kiulaini.

Mganga wake alianza kufanya kazi tangu Jay Melody alipotoa Huba Hulu, kuanzia pale, kila wimbo uliofuata Watanzania tunaukubali, tunaona ni mzuri na dogo anazidi kuvun mashabiki.

Ni muhimu mganga wa Jay Melody apongezwe sana, lakini cha muhimu zaidi ni akumbushwe kupunguza ukali wa dawa kidogo kwa sababu amefanya mashabiki wanapenda sana muziki wa Jay Melody kiasi sasa wanaanza kumshindanisha Jay Melody na wasanii wengine ambao tunatambua wana waganga wakakamavu kuliko yeye na hapa ndiyo tatizo linapoanzia.

Hakuna sababu ya kumshindanisha kila msanii mchanga anayeanza kufanya vizuri na wasanii wengine ambao tayari wapo.

Hakuna haja ya kumshindanisha Jay Melody na Mbosso, Diamond, Zuchu wala mtu yeyote wa Wasafi, hakuna haja ya kumshindanisha Jay Melody na Marioo, hakuna haja ya kumshindanisha Jay Melody na Ibrah, Konde Boy wala msanii yeyote wa Konde Gang, wala hakuja haja ya kumpambanisha msanii yeyote anayechipukia na msanii mwingine ambaye tayari yupo kwenye gemu.

Muziki ni biashara, kwa sababu Jay Melody, Marioo, Zuchu, Diamond na Angela wa Konde Gang wote wanafanya biashara moja ‘automatically’ watajikuta wanakuwa washindani bila hata sisi vyombo vya habari na mashabiki kulazimisha kuwashindanisha. Rapcha ana kauli yake inasema; “siku ina masaa 24, masaa 24 yanatosha kabisa kwa shabiki wa muziki kusikiliza muziki wa kila msanii anayemtaka.”

Akimaanisha, hakuja haja ya kumshindanisha Rapcha na Young Lunya, na Dogo Janja au Conboi. Kama shabiki atajisikia kusikiliza ngoma za Dogo Janja atasikiliza, na kama atajisikia kusikiliza za wote atasikiliza.

Ushindani kwenye biashara ni mzuri lakini usilazimishwe kwenye muziki kwa sababu mara nyingi unaishia kuwagawa wasanii badala ya kuwafanya kitu kimoja. Ndo matokeo yake utasikia msanii huyu hachezwi kwenye redio fulani.