‘Sanaa Feel Free’ imebadilisha taswira muziki wa singeli

Mkurugenzi wa Uswazi born Talent (UBT), Masoud Kandoro maarufu ‘Meneja Kandoro’ amesema Mradi wa ‘Sanaa Feel Free’ umewasaidia wasanii wa Muziki wa singeli na kubadilisha taswira kuwa muziki huo sio wa kihuni .
Kandoro ambaye ni mmoja wa wanufaika wa mradi huo, ameyasema hayo katika tafrija ya kuonyesha kazi mbalimbali zilizofanywa na wasanii ambazo zimefadhiliwa na mradi huo ambapo yeye alikuja na mradi alioupa jina la ‘Sauti za Kumoyo’.
"Mradi huu wa Sanaa Feel free umeweza kuwaongezea uwezo wa wasanii wa singeli katika namna ya kukuza na kuongeza ufanisi kwenye muziki wao ili kuweza kuongeza mashabiki na kupanua wigo wa wasikilizaji wa muziki wa singeli nje na ndani ya nchi,”amesema.
Akizungumzia kuhusu mradi wake wa ‘sauti za kumoyo’, Meneja Kandoro amesema ni muziki ambao umechanganywa wa zamani na wa kisasa na kupatikana sauti hizo za kumoyo na kuwataja wasanii aliowashirikisha kuwa Kinata Mc, Seneta, Manfongo pamoja na Moto music ambapo kazi zao wametia vionjo kutoka kwenye makabila tofauti tofauti.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa "Sanaa Feel Free" kutoka Taasisi ya Nafasi Arts Space, Rhoda Kabenga, amesema mradi huo umefadhiliwa na ubalozi wa Norway na Uswiss,ambapo awamu hii umeweza kuwapika miezi minane vijana wanne wenye vipaji vya Sanaa ya ufundi ngoma na Sanaa za uoni.
Kutokana na shuhuda mbalimbali zilioolewa na wanufaika, Rhoda ametoa wito kwa wasanii kuwa wabunifu ili waweze kupata wafadhili, kujitangaza na kukuza sanaa kwa ujumla nchini.
Katika Mradi huo, zaidi ya sh3 bilioni zimetolewa na nchi ya Switzerland na Norway kwa ajili ya kusaidia kuendeleza na kukuza vipaji vya wasanii Tanzania na kati ya fedha hizo Switzerland wametoa Sh2.1 bilioni huku Norway wakitoa Sh1 bilioni.
Mkurugenzi huyo amesema fedha hizo zitakuwa zikitolewa kwa makundi au msanii mmojammoja atakayeandika andiko zuri la kufanya katika sanaa yake lengo likiwa kuieleimisha jamii kupitia vipaji vyao na watakaofanikiwa kushinda watapatiwa fedha kati ya Sh10 milioni hadi Sh50 milioni kutegemea na ukubwa wa mradi husika.