Safari ya mwisho ya Mabera ilianzia hapa

WAKATI mashabiki wa muziki wa dansi bado wanaendelea kuugulia maumivu ya kuondokewa na mpiga gitaa la solo mahiri nchini, Saidi Mabera, familia ya marehemu imeanika safari nzima ya mwisho ya mkali huyo aliyedumu na Msondo Ngoma kwa miaka 47 mfululizo.

Mabera alimaliza mwendo duniani Septemba 28 na kuzikwa siku inayofuata, huku mashabiki wakiwa bado wapo njia panda kushindwa kujua kitu gani kiliochomuondoa mkali huyo aliyejiunga Msondo mwaka 1973 na kudumu naye kwa muda wote hadi alipofariki dunia.

Mwanaspoti ilifika msibani nyumbani kwake Goba, jijini Dar es Salaam na lilipata nafasi ya kuzungumza na familia ya Mabera, wakiwamo watoto, ndugu na hata majirani pamoja na wafanyakazi wenzak

TATIZO LILIANZIA HAPA

Kwa mujibu wa mtoto mkubwa wa mzee Mabera anayeitwa, Saidi Mabera Junior alisema Jumatatu jioni iliyopita baba yake alizidiwa ghafla, wakambiza hospitali ya Masana iliyopo Mbezi.

“Mara zote huwa anatibiwa hapo na sana sana huwa anasumbuliwa na miguu, sukari na presha. Lakini siku hiyo (Jumatatu) alivyozidiwa usiku tulimpeleka na alivyochekiwa daktari akasema ni presha. Akapatiwa matibabu kidogo, tukarudi naye nyumbani,” alisema Mabera Junior ambaye pia ni mwanamuziki, japo kwa sasa amepumzika kidogo.

Mabera Junior alisimulia walivyorudi nyumbani, mzee alikuwa anaendelea vizuri, anazungumza na kucheka kabisa lakini baadae, mida ya saa 3 za usiku hali yake ilikuwa mbaya ghafla na ikabidi wamkimbize Hospitali ya Muhimbili ambapo umauti ulimfika huko usiku huo huo.

Mtoto mwingine wa Mabera, Shaaban Mabera, aliyekuwa karibu na mzee siku zote, amebainisha tatizo la mzee wao sio geni kwani takribani miezi miwili iliyopita alianguka kwenye shoo wakati bendi yao ikitumbuiza eneo la Buza, Dar es Salaam kwenye ukumbi unaoitwa Dar Safari.

“Tuliambiwa alikuwa anapiga muziki, lakini mara akatoka kwenda msalani na baadae wakamkuta amenguka huko akiwa ameishiwa nguvu,” alisema Shaaban, huku akilia.

 MSIKIE MENEJA

Hata hivyo, kwenye hili la kuanguka kwenye shoo, linasimuliwa vizuri zaidi na Meneja wa Bendi ya Msondo, Saidi Kibiriti kwa sababu yeye alikuwa eneo la tukio.

“Ilikuwa ni kama mwezi na wiki tatu hivi zilizopita, tulikuwa tunapiga shoo ukumbi mmoja uko Buza unaitwa Dar Safari.

Tukiwa pale mzee akatoka kwenda msalani, akachelewa kurudi na tulipomfuata tukamkuta amenguka huko huko msalani, akiwa ameishiwa nguvu na hawezi kunyanyuka,” alisema Kibiriti na kuongeza;

“Baada ya kumtoa kule msalani, walimchukua na kumuwahisha hospitali ya karibu na eneo la tukio na daktari aliyempima akaambiwa kuwa miguu ilikuwa inamsumbua pamoja na presha.”

“Nadhani kwa sababu ya umri, alikuwa hawezi kusimama muda mrefu, huenda hilo lilichangia. Na baada ya hapo sisi kama uongozi tukaona tumzuie mzee asiwe anakuja ofisini,” aliongeza Kibiriti.

 ALIPENDA KAZI

“Kwa sababu afya ni bora kuliko kitu chochote, lakini tatizo mzee alikuwa anapenda muziki, anapenda kujumuika nasi muda wote, kwa kweli tulikuwa tunapenda kuwa naye mara zote,” alisema Kibiriti.

Meneja huyo aliongeza, licha ya kwamba kwa kipindi chote hicho alikuwa haendi ofisini, lakini bado bendi ilikuwa inampatia stahiki zake zote kama kawaida.

“Kila kitu alikuwa anapata kama ilivyokuwa mwanzo. Ratiba yetu ni tunapiga Jumatano hadi Jumapili. Hivyo kila Ijumaa na Jumatatu tulikuwa tunamtumia pesa. Tena mara ya mwisho ni Jumatatu jioni, niliongea nae kwa ajili ya kumtumia pesa na alikuwa mzima kabisa, lakini usiku tukapewa hii taarifa yenye kuumiza.”

 NENO LAKE LA MWISHO

Kwa mujibu wa familia yake, marehemu Mabera alikuwa na jumla ya watoto 13 kutoka kwa wake watatu aliowahi kuwa nao, (mmoja alifariki wamebaki 12), lakini pia alikuwa na wajukuu 16.

“Kabla ya kufa, aliniambia Shaaban mtunze mama yako. Na mpendane wewe na ndugu zako bila kujali mtoto yupi ni wa mama yupi,” alisema Shaaban lakini akashindwa kuzungumza zaidi, akatoa leso na kuanza kulia.

 HISTORIA YAKE

Said Mabera alizaliwa Ujiji Kigoma, mwaka 1949 na Elimu ya Msingi aliipata Shule ya Government mwaka 1958 kabla ya kutumbukia kwenye muziki miaka ya 1960 akipita bendi mbalimbali ikiwamo Lake Jazz, Musoma Jazz, Tabora Jazz na Orchestra International ya Arusha kabla ya kujiunga Msondo Ngoma (enzi za Nuta Jazz) na kudumu naye hadi mauti yalipomkuta.

Akiwa na Msondo licha ya kupiga gita la kuongoza yaani solo, pia alikuwa ni mtunzi na mpangaji wa muziki na moja ya ngoma zake matata ni Mwana Acha Wizi, Faulata, Uzuri Si Shani, Kifo cha Baba, Huna Shukrani na nyinginezo.