‘Mtasubiri’ ya Diamond na Zuchu yapigwa marufuku

‘Mtasubiri’ ya Diamond na Zuchu yapigwa marufuku

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA), imepiga marufuku vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kutoonyesha wimbo wa ‘Mtasubiri’ ulioimbwa na msanii Diamond Platnumz akimshirikisha Zuchu.

Video hiyo iliyotoka mwezi mmoja uliopita mpaka sasa imeshatazamwa zaidi ya mara milioni kumi kwenye mtandao wa Youtube na ni moja kati ya nyimbo zilizoko katika EP yake First of All (FOA) ukiwa wimbo namba  nne.
Kuzuiwa kwa video hiyo kumetangazwa kupitia taarifa ya TCRA na kuthibitishwa na Meneja wake wa huduma za utangazaji, Mhandisi Andrew Kisaka,alipozungumza na Mwananchi Digital ambaye hata hivyo alitaka kwa maelezo zaidi watafutwe Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).
“Ni kweli hiyo ni taarifa yetu, lakini kwa maelezo zaidi watafute Basata kwani wao kiutaratibu ndio wanaleta maombi na sisi tunachofanya ni utekelezaji kama wasimamizi wa vyombo vya utangazaji,” amesema Mhandisi Kisaka.
Katika tangazo hilo linaloonyesha limetolewa Aprili 29, 2022 ikiwa na kichwa cha habari ’Vyombo vya utangazaji kutopiga wimbo wa msanii Nasib Abdul (Diamond Platnumz) kwa kushirikiana na Zuhura Othuman Soud (Zuchu), uitwao ‘Mtasubiri Sana’.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa TCRA imepokea taarifa kutoka Basata ya kuzuia usambazaji wa video ya wimbo wa wasanii hao unaopigwa katika mitandao ya kijamii na vyombo vya utangazaji.
Imesema sababu za kuzuia video hiyo ni kutokana na kuwa na kipande kinaonyesha wahusika wapo kanisani wanaimba kwaya lakini baadae wakaacha na kuelekea kwingine.
“Kipande hicho cha video kimeleta ukakasi miongoni mwa waumini wa madhehebu ya dini na kuleta hisia kwamba ni dharau juu ya dini/madhehebu fulani.
“Hivyo kwa baru hii, TCRA inaagiza vyombo vyote vya utangazaji na mitandao ya kijamii hapa nchini kutorusha video ya wimbo uitwao huo ’Mtasubiri’ hadi hapo msanii tajwa atakaporekebisha sehemu hiyo ya video,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Mwananchi Digital iliutafuta uogozi wa WCB, ambapo Meneja wa lebo hiyo, Hamis Tale, alijibu kwa ujumbe mfupi ’’sijui mie’.
Basata walipotafutwa kupata maelezo zaidi simu ya Katibu Mkuu wake, Mniko Mtiko iliita bila ya kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi kupitia whatsApp ili kupata ufafanuzi kuhusu jambo hilo hakujibu, bado tunaendelea kuwatafuta.
TCRA inatangaza kufungia video hiyo ikiwa imepita miaka minne tangu ilipofungia nyimbo 15 na kati ya hizo mbili zilikuwa za Diamond ikiwemo Wakawaka na Hallelujah.
Nyingine ilikuwa ni Kibamia (Roma Mkatoliki), Pale Kati patamu na Maku Makuz (Ney wa Mitego), Hainaga Ushemeji (Manifongo), I am Sorry JK (Nikki Mbishi.

Pia ilikuwepo  Chura na Nimevurugwa (Snura), Tema mate tumchape (Madee), Uzuri wako (Jux), Nampa papa (Gigy Money) na  Nampaga (Baranaba).