MKOJANI - 4: Hata Joketi ananijua, nililia ndani ya ndege

Monday February 22 2021
mkojani pic
By Kelvin Kagambo
By Olipa Assa

KATIKA kuhitimisha makala iliyotokana na mahojiano maalumu na Mwanaspoti, leo Mkojani anafichua ishu yake ya kumwaga chozi ndani ya ndege mbele ya meneja wake. Kitu gani kilichomliza? Endelea na mchekeshaji huyo aliyedai eti hadi Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo anamjua... Tiririka naye wakati wa maswali aliyopigwa na Mwanaspoti naye alivyojibu!

MWANASPOTI: Ni jambo gani la kudhalilisha liliwahi kukutokea kwa sababu ya ushamba?

MKOJANI: (Anacheka sana kabla ya kuanza kujibu). Kuna siku nilienda kwenye hoteli moja iko Posta kule karibu na Ikulu. Ni hoteli kubwa sana na ilikuwa ndiyo mara yangu ya kwanza kuingia kwenye hoteli kama hiyo.

Sasa hiyo hoteli ilikuwa na ngazi zile za kuslaidi (escalator) na nilikuwa sijawahi kuzipanda katika maisha yangu. Kilichonipata nashukuru Mungu hakuna mtu aliyenirekodi video.

Ilikuwa hivi, nilipanda ile ngazi ikaanza kunitelezesha taratibu kwenda juu, sasa unajua ukitaka kushika ile ngazi lazima uifanyie taimingi kama unaruka, mimi nilikuwa sijui hilo, kilichotokea nilikula mwereka, nikaanguka, sendo zangu nilizokuwa nimevaa zikaruka huko. Nikaangalia huku na kule, kisha nikajikung’uta na kuanza kuondoka, ile siku sitaisahau na bado hizo ngazi naziogopa kusema ukweli.

MWANASPOTI: Je siku yako ya kwanza kupanda ndege ilikuwaje?

Advertisement

MKOJANI: Kheeeee mamamamaaaa, yaani hilo limetokea hivi karibuni nilikuwa naenda mkoani Mwanza kwenye shoo na meneja wangu BenQ Johnson, hiyo ndio ilikuwa mara ya kwanza kupanda ndege, niliangua kilio nakwambia.

Sasa meneja akawa ananiuliza una shida gani, nikamwambia nalia kwa furaha kwa sababu kupanda ndege ilikuwa ni ndoto yangu tangu utotoni. Na nadhani ni ndoto ya kila mtoto aliyezaliwa uswahilini, ndiyo maana tukiulizwa ukiwa mkubwa unataka kuwa nani tunasema rubani.

Meneja akanitazama akaniuliza wewe Mkojani upo sawa kweli, nikamwambia ndio, akaniambia hujui kwamba unatia aibu ona sasa watu wanatuangalia sisi.

Kiukweli meneja alichefukwa sana, usione sasa anacheka, haikuwa hivyo siku ile maana hata baada ya kushuka akaniambia ukirudia tena kuleta aibu zile utakuwa unasafiri mwenyewe.

MWANASPOTI: Ulisema wakati unachekesha barabarani na matumbo na masizi usoni kuna wanawake waliwahi kukutaa kwa sababu ya kazi yako. Kuna yeyote kati ya hao ambaye anakutafuta baada ya kuwa maarufu?

MKOMAJI: Hapana, hawajawahi na tena wasithubutu. Kama huko walipo wananisoma nawatahadharisha wasinijaribu kwa sababu nitawatolea nje. Kwanza ninaweza kuwa na maswali mengi kwamba walisahau nini au nimebadilika nini?

Halafu isitoshe mimi sio mtu wa mademu kwenye maisha yangu halisi, nikiwa na mpenzi mmoja basi ni huyo huyo na natulia kweli kweli. Sasa wakija sasa hivi siwezi hata kuwapa nafasi hata ya kugonga hodi.

MWANASPOTI: Kuna wakati umewahi kuujutia ustaa?

MKOJANI: Sana, haswa ninapokuwa sina pesa. Kwa sababu kabla sijawa maarufu ilikuwa nikiwa na Sh500 naweza kununua maandazi yangu matatu na maji kandoro nikapitisha siku. Lakini ukishakuwa staa huwezi kufanya hivyo, watakwambia umefulia mbaya.

Kwa sasa hivi nina kagari, lakini siku nikikosa pesa ya mafuta siwezi kupanda daladala kwani nahofia macho ya watu, najua kila mtu atakuwa ananingalia, wengine watanipost watasema nimefulia. Inatesa kuwa mtu maarufu ukiwa huna hela.

Pia unajua mimi sio mtu wa kuvaa kibishoo, lakini kuna wakati nalazimika kunyoa viduku, kuvaa hereni, kuvaa pamba kali za kibishoo kwa sababu natoka naenda kukutana na watu na inabidi nionekane kistaa ili nitunze brand. Inatesa lakini pia nafurahia kuwa maarufu na kuingiza kipato kwa kufanya kitu ninachokipenda ambacho ni uchekeshaji.

MWANASPOTI: Kiongozi gani wa kiserikali upo karibu naye?

MKOJANI: Nipo karibu na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mheshimiwa, Joketi Mwangelo na amenialika kwenye tamasha lililopewa jina la Ushoroba, litakalofanyika Februali 19 (juzi), katika viwanja vya Chanzige.

Joketi anazikubali kazi zangu na kuziunga mkono, jambo linalonipa moyo kwamba kumbe hata viongozi wanapata muda wa kututazama tunachokifanya.

MWISHO

Advertisement