Miss Tanzania wa 27 huyu hapa

Miss Tanzania wa 27 huyu hapa

PISI kali 20(pichani) kesho zitapanda jukwaani kusaka mrembo wa Miss Tanzania 2020 ambaye atakuwa ni mrembo wa 27 katika historia ya shindano hilo.

Warembo hao kutoka kanda ya Kaskazini, Mashariki, kanda ya kati, kanda ya ziwa na Dar es Salaam watachuana katika fainali itakayofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam.

Mshindi kwenye fainali za kesho atakuwa Miss Tanzania wa 27 tangu kuanzishwa shindano hilo 1967 kabla ya kusitishwa na kurejea tena mwaka 1994 hadi sasa ambapo warembo 20 watapanda jukwaani.

Jana warembo hao walitembelea ofisi za makao makuu ya kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL), Tabata Relini, Dar es Salaam ili kujionea jinsi Mwanaspoti inavyotengezwa.

“Niko vizuri, nimejipanga kuwa Miss Tanzania na kuiwakilisa chi kwenye Miss World,” alisema Zenitha Deodatus wa kanda ya Mashariki.

Magreth Mwambi anayeiwakilisha kanda ya Dar es Salaam alisema anatarajia ushindi kwenye fainali hiyo.

“Mchuano ni mkali, kila mrembo ana sifa za kuwa Miss Tanzania, ndiyo sababu wote tumeingia fainali, nimejiandaa na ninaamini nitashinda na kuwa Miss Tanzania 2020,” alisema.

Razia Abraham anayeiwakilisha kanda ya Dar es Salaam alisema anatarajia ndoto yake ya kuwa Miss Tanzania 2020 itatimia Jumamosi.

Mratibu wa fainali hizo, Basilla Mwanukuzi na Miss Tanzania wa 1998 alisema mshindi wa mwaka huu atazawadiwa gari mpya aina ya Subaru Impreza na mshindi wa pili atapewa kiwanja eneo la Kigamboni.

“Washiriki wote wataondoka na zawadi mbalimbali kwenye fainali hiyo,” alisema Basilla.

Jana warembo hao walitembelea ofisi za MCL na kujionea uzalishaji wa kampuni hiyo.

Katika ziara hiyo, warembo hao walitembelea chumba cha habari cha MCL, kitengo cha Mwananchi Digital, Sport Unit, Studio za Mwananchi Digital na vitengo vingine ndani ya ofisi hiyo.

Mhariri mtendaji wa gazeti Mwananchi, Angetile Osiah aliwambia wote ni washindi na ndio sababu wameingia kwenye fainali akiwapongeza kwa hatua hiyo.

“Hadi kuingia fainali maana yake wote ni washindi ingawa taji la Miss Tanzania liko moja, lakini uwepo wenu kwenye fainali ni fursa ya kufika mbali zaidi bila kujali umeshinda taji au la,” alisema.

BY IMANI MAKONGORO