Jumbe kuzushiwa kifo, nyoka chumbani

Jumbe kuzushiwa kifo, nyoka chumbani

GWIJI wa muziki wa dansi nchini, Hussein Jumbe, amepitia mengi kufikia sasa. Ukiacha tungo zake maarufu katika kazi yake ya sanaa, kubwa linalokumbukwa nje ya muziki ambalo lilitingisha ni tukio la kupakaziwa kifo na mambo kibao.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalum na muimbaji huyu aliyetamba katika bendi kubwa nchini na amefunguka mengi yakiwamo matukio ya kushanagaza yaliyomtokea likiwamo la siku za hivi karibuni la kuvunjika vidole vya mguuni, baada kuota ndoto akipambana na kuku wa ajabu. Hebu tiririka naye pamoja sasa...

“Nilitokea kuupenda muziki wa dansi tangu nikiwa shule ya msingi huku mwanamuziki alinimvutia akiwa ni Marijani Rajabu, ambaye nilikuwa nikienda kuangalia maonyesho yake pale baa ya Prince iliyokuwa maeneo ya Mnazi Mmoja kwa kiingilio cha Sh5,” anasimilia Jumbe.

Anasema kuwa sio kama alikuwa akipewa pesa kwa ajili ya kwenda kwenye burudani bali alikuwa akihifadhi hela ya shule aliyopewa na wazazi wake kwa ajili ya chakula ili Jumapili awe njema tayari kwenda kumuona nguli huyo wa muziki wa dansi nchini aliyeacha alama kubwa.

Jumbe, ambaye baadaye alikuwa mwamuziki mkali, amepata kufanya kazi kwenye bendi mbalimbali ikiwemo Orchestra Siza iliyokuwa mtaani kwao na kuingia hapo kama mpiga ngoma na alipofika Sekondari alichukuliwa na bendi Asilia Jazz iliyokuwa ikimilikiwa na Baraza la Muziki la Taifa (Bamuta).

Ilipofika mwaka 1983, alitimkia mkoani Tabora na huko alijiunga na bendi ya Tabora Jazz kama mpiga ngoma.

Badaye mwanamuziki Shem Kalenga aligundua kipaji chake cha kuimba baada ya kumsikia akiimba nyimbo za Marijani wakiwa safarini kwenda Mpanda, mkoani Rukwa (Sasa Katavi).

Kuanzia hapo kama kiongozi wa bendi, Kalenga alimhamisha kutoka kupiga vyombo na kuimba na kutunga wimbo wa ‘Mwanzo wa Binadamu’ ambapo alimpa sehemu kubwa auimbe.

Ni kutokana na kipaji chake hicho Jumbe, anasema bendi mbalimbali zilianza kumtolea macho na kujikuta anahama kila uchwao.

Bendi alizofanya nazo kazi ni pamoja na Mlimani Park, Mikumi Sound, Mlimani Park, ikwemo Msondo Ngoma, Sikinde, Tabora Jazz, Tanzania One Theatre (TOT) na mwaka 2009 na baada ya kuchoka kuajiriwa alianzisha bendi yake aliyoipa jina la Talent yenye makazi yake Temeke na ndiyo yupo nayo hadi sasa.

Mikasa mbalimbali aliyopitia

kuhusu mikasa ambayo amewahi kuipitia ukiacha ule wa kuzushiwa kifo, Jumbe anasema alishaona nyoka zaidi ya mara moja nyumbani kwake.

Tukio la kwanza alimuona kwenye suruali yake asubuhi alipoamka na siku nyingine majirani walimkuta nyoka mlangoni kwake.

Kama vile haitoshi wiki mbili zilizopita aliona mjusi akipaza sauti akiwa kwenye onyesho maeneo ya Mwembe Yanga. Katika tukio hilo, anasema hazikupita siku nyingi ndipo akapata ajali ya kuvunjika vidole vinne baada ya kuota anampiga kuku mateke.

Akielezea kwa urefu kuhusu tukio hilo, Jumbe anasema ilikuwa siku ya Jumatano akiwa amelala, aliota akiwa anaendesha baiskeli katika moja ya mtaa kijijini kwao.

Hata hivyo, akiwa njiani alikutana na wasichana watatu na alipowakaribia aliwasikia wakisema mtu mwenyewe si ndio huyu na kuamua kupita kushoto ili kuwakwepa.

Wakati akiwa anafanya hivyo alikutana na mtoto akiwa ameshika manati na kumtishia kama anampiga, lakini alimpita na aliposigea mbele kidogo jiwe hilo likagonga katika tairi la nyuma la baiskeli yake.

“Kitendo cha mtoto yule kupiga baiskeli yangu, kilinifanya nimrudie na kumuuliza kulikoni kabla sijamaliza, akageuka kuku ambaye alikuja kuanza kupambana na mimi na ndipo hapa nikawa napambana naye kwa kumpiga mateke.

“Kumbe wakati najiona napigana na kuku, nilikuwa naupiga ukuta mateke jambo lililomshutua mke wangu kwa kuniona nikiwa katika hali ile ambapo, aliniamsha na wakati huo nilikuwa nimetota mwili mzima na ndipo nikamuahadithia ndoto hiyo,” anasema.

Hata hivyo, kulipokucha aliendelea na shughuli zake ikiwemo mazoezini na siku iliyofuata maumivu yalizidi na hapo ndipo mkewe alimlazimisha kwenda hospitali kwa matibabu na kubainika vidole vinne vimevunjika.

KUMILIKI BENDI YAKE AU KUAJIRIWA

Katika hili, Jumbe anasema kuna utofauti mkubwa kwani, kumiliki bendi ni sawa na umetoka kwenye nyumba ya kupanga na kuhamia kwako.

Japokuwa kuna changamoto ya usimamizi kwa wanamuziki kwa kuwa, kuna wengine ni ngumu kuwaongoza.

“Kusimamia wanamuziki ni lazima uwe na roho ya chuma, hawa hata siku ukiwaambia leo hatujaingiza hela kutokana na mvua, hawakuelewi na pia ni wajuaji wa kila kitu. Lakini, kwa kuwa mimi nimefanya kazi katika fani hii muda mrefu nakwenda nao hivyo hivyo,” anasema Jumbe.

Hata hivyo, anafichua kuwa tangu ameanzisha bendi hiyo ambayo kwa sasa inakaribia kutimiza miaka 10, ikiwa na wasanii wanane, mambo yanakwenda vizuri na sasa anajiandaa kuachia albamu yao ya tisa.

VIPI SIKINDE AU MSONDO

Jumbe anaeleza kwamba, bendi hizi zitabaki kuwa mama wa muziki kwani, zimesheheni vipaji vya hali ya juu, na kuwataka wasanii wa sasa kuchota ujuzi kwa wakongwe.

Anasema licha ya muziki wa dansi kushuka lakini, ukienda katika bendi hizi bado kuna wapenzi na kutoboa siri ya hilo kuwa ni ni kutokana na kuwa na tungo zanazoishi.

Lakini, katika kuurudisha muziki wa dansi kama enzi zamani, Jumbe anafichua kuwa zinapaswa kwenda na wakati ikiwemo kutumia mitandao ya kijamii kujitangaza kama ilivyo kwa wasanii wa Bongo Fleva.

Je, unafahamu siri ya wimbo wa Siri ambao Rayvanny wa WCB alikwenda kuufanya tena? Fuatilia kesho IIjumaa kufahamu mengi zaidi ambayo Jumbe amefunguka.

Siri ya nyimbo zake kurudiwa

Jumbe ambaye anasema ana nyimbo zaidi ya 300 katika maisha yake ya muziki, moja ya nyimbo zake zilizorudiwa ni ule wa ‘Mapenzi ya Siri’ ulioimbwa na msanii wa Bongo Fleva, Rayvanny kutoka lebo ya WCB.

Anasema hili lilitokea baada ya mmoja wa viongozi wa lebo hiyo kuuona katika ukurasa wake wa Instagrm, ambapo alimdiem na kuweza kumuunganisha na msanii wao na kufanya kazi.

Jumbe anasema jambo lile lilimpa heshima na kujiona mtu wa pekee, kwani mbali ya kuchukuliwa kwa wimbo wake lakini yeye na mke wake Zakhia walionekana kwenye video ya wimbo huo jambo ambalo ni kumbukumbu isiyofutika kwao.

Vilevile anasema mchongo huo ulimuwezesha kupata mtonyo mrefu kuliko ambayo aliufikiria kwenye kichwa chake awali hali iliyomuwezesha kujenga nyumba maeneo ya Toangoma.

Anaunaje muziki wa Bongo Fleva

Jumbe anasema muziki huo ni mzuri, lakini aliwashauri kuacha kuimba tungo zenye matusi kwani zinakuwa zikileta picha mbaya kwa jamii hususani watoto wanaozaliwa na kuukuta muziki huo.

Katika hili anashauri pia vyombo vya habari zikiwemo televisheni na redip kutowabeba wasanii wenye tungo hizi tata kwa kuwa nao wanachangia ukiukwaji wa maadili na kuonekana kuwa ni maisha ya kawaida jambo ambalo sio sawa.

Tukio lake la furaha na huzuni ni lipi

Katika maisha kila mtu kuna tukio alilowahi kukutana nalo likawa huzuni au la furaha.Kwa Jumbe tukio la furaha ni lile la kumuoa mke Zakhia ambaye awali ndugu zake walikataa kupokea barua yake ya posa kwa kuwa tu yeye ni mwanamuziki.

Jambo hilo alisema lilimsononesha kwa kuwa jamii iliona kama mwanamuziki hastahili kuwa na mke na ni watu wa ovyoovyo.

Katika hili anasema halina ukweli na mfano mzuri ni yeye ambapo mpaka leo amedumu na mke wake katika ndoa kwa miaka 27 sasa na hawajawahi kupelka kesi sehemu yoyote.

Wakati tukio la huzuni, anasema hatakaa akasahau siku aliyozushiwa kifo, ukizingatia kwamba siku hiyo alikuwa yupo kitandaani akiumwa.

Akielezea mkasa huu, anasema ilitokana na moja ya redio nchini katika kipindi chake cha matangazo ya vifo kutangaza jina la msanii linalofanana na lake mwisho la Jumbe kuwa amefariki.

Kwa kuwa watu walikuwa wakijua anaumwa, wakatafsiri moja kwa moja ni yeye na hivyo watu kuanza kwenda nyumbani kwake huku wakilia.

Ni kutokana na hilo, aliamua kutunga wimbo wa’Nachechemea’ ambao ulikuwa gumzo katika vituo mbalimbali vya redio na televisheni.

UHUSIANO NA BITCHUKA

Wakati kukielezwa kuwa yeye na bitchuka hawakuwa wakiiva chungu kimoja, Jumbe anakanusha hilo na kueleza kuwa ni mmoja wa wanamuziki anaowakubali na wamekuwa wakiwasiliana mara kwa mara.

KIAPO CHA MSONDO

Akiwa bendi ya Msondo, Jumbe aliwahi kutunga kibao kinaitwa ’kiapo’ kama moja ya kujiapiza kutoondoka katika bendi hiyo, lakini baadaye aliondoka.

Akilifafanua hili, Jumbe anasema ilitokana na maslahi na kujikuta anaondoka kwenye bendi hiyo na kipande kuhusu maslahi na kwenda na wakati pia ni moja ya shairilililopo kwenye wimbo huo, kipande ambacho alikiimba marehemu Maalim Gurumo.

BENDI BORA

Licha ya kupita bendi mbalimbali katika maisha yake, Jumbe anasema Msondo Ngoma itabaki kuwa bendi bora kwake wakati alipokuwa mwajiriwa.

Katika bendi hiyo aliyodumu muda mrefu kuliko zote kwa kukaa hapo kwa miaka 15 anasema ilikuwa na uongozi makini uliokuwa unajua nini unachokifanya na ndio maana mara ya mwisho baada ya kuachana nayo aliamua kuanzisha yake kutokana na kuchota ujuzi kwao ikiwemo suala zima la uvumilivu.


MRITHI WAKE

Wanasema mtoto wa nyoka ni nyoka, Jumbe ambaye ana watoto nane, anasema kati yao mmoja kamrithi kipaji cha kuimba na mwingine kipaji cha kucheza mpira shughuli ambayo pia alikuwa akiifanya akiwa mdogo ambapo alichezea timu ya watoto ya Simba hadi kufika hatua ya ligi kuu.

Kwa mtoto anayeimba anasema amekuwa hasikiki sana kwa kuwa pia ni mfanyabiashara na amejikita kwa sasa katika shughuli zake huko.

Wakati anayecheza mpira anasema kwa sasa anakipiga katika timu ya Mwadui.