Diamond kutua Tulia Street Talent Competition

Miss Mwanza awachanganya Ben Pol na Diamond!

Mbeya. Mwanamuziki Diamond Platnumz, anatarajia kuwa miongoni mwa wageni waalikwa katika mashindano ya kusaka vipaji vya muziki yatakayofanyika kesho Jumamosi Desemba 3 mkoani hapa.

Mkurugenzi wa Tulia Trust, Jacklin Boazi amesema huu ni msimu wa tatu kwa mashindano hayo kufanyika ikiwana lengo la kuibua vipaji kwani washindi kwa misimu yote miwili walipelekwa chuo cha sanaa Bagamoyo kwaajili ya kujiendeleza.

Amesema vijana wengi wenye vipaji wameshindwa kujiendeleza kutokana na kukosa sapoti ya kufanya kipaji chake kizidi kukua na kuonekana mbele ya jamii.

"Mwaka huu tumeboresha mambo mengi pamoja na kumleta, Diamond sababu vijana wengi tunaamini wana ndoto ya kufika pale alipo yeye na hii inaweza ikawa fursa kwa vijana wetu.

"Tunaamini maneno yake yanaweza yakawa tiba kwa vijana na kuwafanya wao wasonge mbele na sababu anafanya kazi ya namna hii inawezekana wachache wakabahatika akawachukua," amesema Jacklin.

Ameongeza mwaka jana mashindano haya tulifanya kwa Mkoa wa Mbeya pekee lakini mwaka huu kumekuwa na ongezeko la washiriki kutoka mikoa tofauti kama vile, Songwe, Sumbawanga na Ruvuma.

Amesema lengo ni kuona vijana wanakuwa na ajira na kupata kipato kupitia kipaji alichokuwa nacho kuliko kumwacha abaki nacho mtaani ndio maana washindi wanapelekwa chuo cha Bagamoyo kwa kujiendeleza zaidi.

Baadhi ya vikundi vinavyoshiriki ni pamoja na Mbeya Chocolate, Lily Kings, Wakatili Dancer, Watamu, Waarabu, Kidy Nation, Monster, Swax, Scopion, Oxygen, Winners na Sprit Chidren.