#WC2018: Mechi ya Ubelgiji vs Ufaransa yawavuruga wafanyabiashara

Tuesday July 10 2018

 

Mashabiki wa Ubelgiji matumaini yao ni ushindi tu katika mechi yao ya leo Jumanne dhidi ya Ufaransa saa tatu usiku.

Wabelgiji wamekuwa wakikatiza mitaa mbalimbali ya Moscow wakiwa na bendera zao kuashiria kuwa leo haponi mtu.

Jambo la ajabu ni kwa mashabiki wasiokuwa na timu, wamekuwa na wakati mgumu kujua siku ya leo washabikie timu gani kutokana na ubora wa kila timu.

Mfanyabiashara mmoja anayemiliki baa amesema inamuwia ugumu hasa mashabiki wanaofika hapo, jambo ambalo limemlazimu kupamba baa yake nusu kwa nusu.

Upande mmoja wa baa hiyo imewekwa bendera za Ubelgiji, na mwingine umewekwa bendera za Ufaransa.

Alisema lengo la kufanya hivyo nio kuendana na mazingira ya mashabiki

wao wanaofika kupata huduma hapo.

Aliongeza kuwa kila jambo wanalofanya lazima liwe na muonekano wa pande mbili yaani Ufaransa na Ubelgiji hasa katika mapambo ndani ya baa hiyo.

Mfanyabiashara mwingine alisema vyovyote itakapokuwa baada ya timu hizo kupata matokeo leo usiku kwake ni jambo gumu katika uendeshaji wa shughuli zake.

Hata yeye amejikuta akizishabikia timu zote kwa sasa licha ya kuwa ni shabiki damu wa Ufaransa.

Mkazi wa Quievrain alisema matokeo yoyote yatamfanya ajisikie vibaya licha ya upande mmoja utaibuka kidedea tu.