#WC2018: Mashabiki timu zilizotolewa wakomaa Russia

Tuesday July 10 2018

 

Kama ulidhani timu zilizotolewa zitakuwa zimeondoka na mashabiki wake, utakuwa unakosea. Hali ilivyo Russia ni kwamba mashabiki wameendelea kubaki huku wakichagua timu za kuzishangilia na maisha yanaendelea.

Mashabiki wameendelea kumiminika kwa ajili ya kushuhudia mechi za nusu fainali zinazoanza kupigwa leo Jumanne usiku kwa kuwakutanisha Ufaransa dhidi ya Ubelgiji.

Shabiki Paula Ponti alisema ataishuhudia mechi ya nusu fainali na anatumaini itakuwa ya kuvutia.

Anaamini kwamba miamba Ubelgiji na Ufaransa ni kama fainali ambapo ametabiri kwamba bingwa wa Kombe la Dunia atatokea kwenye mechi hii ya leo.

Shabiki mwingine, Stephane Schnopp ambaye ni shabiki wa Uruguay kutoka Marekani alisema bado anafikiria ni timu ipi ataishabikia usiku leo Jumanne.

Hata hivyo anaamini Ufaransa itaibuka na ushindi kwenye mchezo huo.