#WC2018: Mbappe amfunika Messi kinoma

Muktasari:

  • Mbappe mwenye miaka 19, amelipandisha jina lake na kuyafunika majina ya Lionel Messi na  Cristiano Ronaldo, baada ya jana kufunga bao la mwisho kwenye dimba la Luzhniki, kuipa Ufaransa Kombe la Dunia kwa ushindi wa 4-2 dhidi ya Croatia.

Moscow, Russia. Mshambuliaji chipukizi wa Ufaransa, Kylian Mbappe, amepaishwa na fainali za mwaka huu za Kombe la Duinia.

Mbappe mwenye miaka 19, amelipandisha jina lake na kuyafunika majina ya Lionel Messi na  Cristiano Ronaldo, baada ya jana kufunga bao la mwisho kwenye dimba la Luzhniki, kuipa Ufaransa Kombe la Dunia kwa ushindi wa 4-2 dhidi ya Croatia.

Mchezaji huyo aliyetwaa tuzo ya mchezaji bora chipukizi wa fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia, amekuwa gumzo kutokana na umahiri aliouonyesha.

Mbape aliyezianza fainali za mwaka huu akiwa hana umaarufu wowote miongoni mwa wachezaji wa Ufaransa, amezimaliza fainali hizo kwa kishindo, bao lake katika mchezo wa fainali dhidi ya Croatia, limemfanya atabiriwe kufanya makubwa katika ulimwengu wa soka hapo baadaye.

Anaonekana kufuata nyayo za magwiji wa soka Pele na Diego Maradona ambao walianza kung’ara tangu fainali zao za kwanza za Dunia hadi wanastaafu.

Kushindwa kufika fainali kwa Ureno inayoongozwa na Ronaldo na Argentina inayoongozwa na Messi, kumempa nafasi chipukizi huyu wa Paris Saint-Germain, kujitangazia jina.