#WC2018: Ni Ufaransa

Muktasari:

  • Mechi hiyo ya fainali iliyoshuhudiwa na mashabiki 78,011 na kuamuliwa na mwamuzi, Nestor Pitana wa Argentina, ilikuwa na matukio mengi, ikiwamo bao la kujifunga, maamuzi ya utata ya kuhusu penalti iliyoamuliwa kwa VAR na makosa ya makipa wa timu zote mbili, lakini Ufaransa ndiyo walioibuka mabingwa wakiweka historia ya kunyakua taji hilo kwa mara ya pili katika rekodi zao.

KWISHA, Ufaransa ndio mabingwa wa fainali za Kombe la Dunia 2018 baada ya jana Jumapili kuwachapa Croatia 4-2 katika fainali iliyofanyika kwenye Uwanja wa Luzhniki mjini Moscow huko Russia.

Mechi hiyo ya fainali iliyoshuhudiwa na mashabiki 78,011 na kuamuliwa na mwamuzi, Nestor Pitana wa Argentina, ilikuwa na matukio mengi, ikiwamo bao la kujifunga, maamuzi ya utata ya kuhusu penalti iliyoamuliwa kwa VAR na makosa ya makipa wa timu zote mbili, lakini Ufaransa ndiyo walioibuka mabingwa wakiweka historia ya kunyakua taji hilo kwa mara ya pili katika rekodi zao.

Taji jingine la dunia walilibeba kwenye Kombe la Dunia 1998, ambapo wakati huo, kocha wao wa sasa, Didier Deschamps alikuwa mchezaji.

Hivyo, Deschamps anaweka rekodi ya kunyakua taji la Kombe la Dunia akiwa mchezaji na baadaye akiwa kocha.

Neema ya Ufaransa ilianza mapema tu, baada ya Mario Mandzukic kujifunga wakati alipojaribu kuupiga kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Antoine Griezmann.

Hiyo ilikuwa kwennye dakika ya 18. Lakini, dakika 10 baadaye, Ivan Perisic alisawazishia Croatia kwa bao matata kabisa kabla ya Griezmann kufunga kwa penalti katika dakika 38 baada ya mwamuzi Pitana kutumia muda mrefu kutazama marudio ya picha za video kabla ya kuamua alichokiamua, kwamba ipigwe penalti. Kwenye kipindi cha pili, mambo yalianza kwa kasi, wakati Croatia wakifikiria namna ya kupata bao la kusawazisha, ghafla wakajikuta kwenye wakati mgumu ambao umewafanya waondoke kabisa kwenye mchezo.

Ufaransa ilifunga mabao ya chapchap kwenye dakika ya 59 na 65 kupitia kwa Paul Pogba na Kylian Mbappe kuwafanya Les Bleus kujihakikisha ubingwa huo.

Kwenye dakika ya 69, kipa Hugo Lloris alifanya makosa yaliyoiruhusu Croatia kufunga bao lao la pili kupitia kwa Mandzukic.

Kwa dakika 90 za mchezo huo, Croatia ilimiliki mpira kwa asilimia 61 dhidi ya asilimia 39 za Ufaransa.

Ubingwa huo kwa Ufaransa umekuja kwenye kipindi kizuri kwao baada ya miaka miwili iliyopita kufika fainali kwenye Euro 2016 na kufungwa na Ureno wakati fainali hizo zilipofanyika kwenye ardhi yao ya nyumbani huko Ufaransa.

Fainali ya jana, ilishuhudia makocha wote wakianza na vikosi vilevile vilivyocheza kwenye nusu fainali, huku Croatia wakiingia kwenye mechi hiyo wakiwa timu waliocheza kwa dakika nyingi zaidi kuliko wapinzani wao baada ya kucheza kwa dakika 120 katika mechi tatu mfululizo za hatua zilizopita kabla ya fainali hiyo.

Lakini, mengine yote yatabaki kuwa historia, habari ya mjini ni kwamba Ufaransa ndiyo mabingwa wa Kombe la Dunia 2018 ikiwa ni miaka 20 tangu kutwaa mara ya mwisho.