TIMUA VUMBI : Ujio wa Sevilla uwe darasa tosha kwa Simba

Muktasari:

Sasa Simba inacheza na Sevilla inayoshiriki Ligi Kuu Hispania (La Liga) inapata nafasi ya kujifunza mambo mbalimbali kupitia mechi hiyo japokuwa itacheza kwa dakika 90 pekee.

WIKI ijayo ya Mei 23, Uwanja wa Taifa, Simba wataikaribisha Sevilla katika mechi ya kirafiki ya kimataifa. Ni mechi kubwa kwani timu zote zinashiriki ligi kuu nchini mwao.

Simba ndiyo mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara na imetoka kushiriki michuano mikubwa ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba iliishia hatua ya robo fainali ambapo ilitolewa na TP Mazembe ikiwa ni mara ya kwanza kufika hatua hiyo tangu kuanza kutumia mfumo mpya ulipobadilishwa mwaka 1997 ingawa hatua ya makundi imeingia mara mbili.

Mfumo wa zamani, Simba iliingia hatua ya robo fainali mwaka 1974 wakati Yanga pia imewahi kufika hatua hiyo ya robo fainali mara mbili mfululizo kabla ya kuanza kutumia mfumo mpya wa michuano hiyo ya CAF.

Kutokana na kiwango cha Simba kwa misimu miwili mfululizo kuwa juu ndiyo maana imekuwa ikimudu vyema kufanya vizuri kwenye mechi zao za ndani na nje ya nchi ambako kwa asilimia kubwa ilipambana na timu ambazo zina wachezaji wengi wazoefu na viwango vya juu.

Sasa Simba inacheza na Sevilla inayoshiriki Ligi Kuu Hispania (La Liga) inapata nafasi ya kujifunza mambo mbalimbali kupitia mechi hiyo japokuwa itacheza kwa dakika 90 pekee.

Dakika hizo ni nyingine kwa mchezaji ama benchi la ufundi kuiba baadhi ya mbinu na ujuzi kutoka kwa Wahispania hao ambao kwenye ligi yao wanashika nafasi ya sita wakiwa na pointi 56 baada ya kucheza mechi 37 wakibakiza mechi moja pekee kumaliza msimu wa ligi hiyo.

Simba yenyewe bado inapambana kutetea ubingwa wao ambapo sasa wanashika nafasi ya pili wakiwa wamekusanya pointi 82 nyuma ya pointi moja ya watani zao Yanga wenye pointi 83 ingawa Wekundu hao wana mechi tano mkononi wakati Yanga wamebaki mbili.

Hii ni nafasi nzuri pia kwa wachezaji wa Simba hasa wale wenye malengo ya kufika mbali kisoka kupata uzoefu wa kucheza na nyota wa timu ambayo kisoka imepiga hatua kubwa ukilinganisha na Ligi hii wanayoshiriki.

Nafasi hii pia si kwa timu na benchi la ufundi pekee bali hata kwa viongozi ambao watajifunza nini cha kufanya kuelekea mafanikio kulingana na malengo yao ya kufika ngazi ya kimataifa, viongozi wataangalia hata aina ya wachezaji ambao wanastahili kuwepo ndani ya Simba.

Hii si kwamba wanaweza kusajili wachezaji kutoka Sevilla ina maana ya kwamba kupitia wachezaji wanaowahitaji basi watachukuwa mfano wa nyota wa Sevilla ambao angalau wanaendana viwango ili angalau wakipata nafasi ya kushiriki tena michuano ya kimataifa basi wafike hata nusu fainali ama fainali zenyewe.

Kwa Simba hii ambayo imebadilisha mfumo wa uendeshaji kutoka klabu ya wanachama kwenda kampuni inaaminika wana uwezo mkubwa wa kusajili nyota wa viwango vya juu ambao wanaweza japo kuzifikia timu kubwa za Afrika.

Uzeofu watakaopata wachezaji wa Simba kwenye mechi hiyo iliyoandaliwa na Kampuni ya michezo ya kubahatisha SportPesa utawasaidia kukuza vipaji vyao.