TIMUA VUMBI : Mzigo wa madaraka TBF utamwangusha Magesa

Thursday January 23 2020

 Mzigo wa madaraka TBF utamwangusha Magesa-timu ya Taifa ya kikapu -benchi la ufundi wanne-

 

By Mwanahiba Richard

HIVI karibu timu ya Taifa ya kikapu ilishiriki michuano ya kimataifa iliyochezwa jijini Nairobi, Kenya. Timu hiyo iliyoiwakilisha nchi ilikuwa na nyota saba pekee na ilishinda mechi moja tu dhidi ya Ertrea. Mashindano hayo ya AfroBal ni kwa ajili ya kufuzu michuano ya Afrika itakayofanyika mwakani.

Awali Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu nchini (TBF), Phares Magesa alitangaza kikosi cha watu nane kushiriki mashindano hayo na baada ya kuhojiwa alikaririwa akisema wengine wanne wataungana na wenzao huko huko, hivyo huenda jumla yao wangekuwa wachezaji 12 kama ambavyo mara nyingi ndiyo wanajumuishwa kwenye timu yoyote iwe ya mkoa, klabu ama taifa.

Kwenye mchezo huo wachezaji wanaonza kucheza ni watano ambapo wachezaji saba wa akiba wanapaswa kukaa benchi na ikitokea mmoja kati ya wachezaji 12 akaumia basi hubaki wachezaji 11 ingawa kanuni za FIBA zinawaruhusu kuomba endapo watahitaji kupata mbadala wa mchezaji aliyeumia ingawa mara nyingi huwa hawakubaliwi.

Sheria za mchezo wa kikapu huruhusu kufanya mabadiliko ya mchezaji hata kama mchezo unaanza tu, hauna muda maalumu wa kufanya mabadiliko hayo.

Kwa kawaida FIBA hutoa fomu ya usajili wa wachezaji 15 kwenye michuano ya kimataifa ambayo ipo chini yao badala ya wachezaji 12 wanaotakiwa pamoja na watu wa benchi la ufundi wanne.

Kwenye mashindano hayo yaliyofanyika Nairobi, timu ya taifa Tanzania iliyoundwa na wachezaji saba lakini waliokwenda huko walikuwa wachezaji sita baada ya mmoja, Isaya Aswile kutoka timu ya mkoa wa Mbeya kushindwa kukamilisha usajili wake.

Advertisement

Kwa mujibu wa Katiba ya TBF majukumu ya usajili wa mashindano yote yaliyo chini ya shirikisho hilo husimamiwa na Katibu Mkuu Msaidizi, Mwenze Kabinda ambaye huenda alichelewa kufanya usajili wa Aswile ikiwamo kutimiza idadi ya wachezaji wanaotakiwa kwa mujibu wa mwongozo wa FIBA.

Hapa Mwenze alijikoroga kidogo maana haya mashindano TBF ilikuwa inayatambua hivyo taratibu nyingine zilipaswa kufanyika mapema ikiwamo kuteua timu imara yenye mchanganyiko mzuri wa pande zote mbili, Bara na Visiwani

Magesa yeye anaingia kwenye mkumbo huu kwa kujitakia kwasababu anabeba majukumu yote ya shirikisho hilo kwa kufuata Katiba yao inayompa nguvu kusimamia kila jambo na ndiyo maana makosa ama upungufu wa watendaji wengine hauonekani kabisa huku akibaki kupokea lawama za watu wengine.

Watendaji wake wanafahamu wazi nini wanapaswa kukifanya na kwa wakati gani lakini hawafanyi jitihada zozote kwasababu tu wanafahamu kwamba Rais wao ndiye mwenye mamlaka makubwa ya kuendesha mchezo huo hata kama wanaoona anachokifanya kitawaangusha siku zijazo.

Mwenze na Katibu wake Michale Mwita wamecheza mchezo huo, naamini huu ni wakati wa kupambana kuhakikisha mchezo wa kikapu unakuwa na si kudodora kama ilivyo sasa na hii ni kutokana tu na udhaifu wa viongozi wachache ambao huenda hawana uchungu na mchezo wenyewe. Mwita hebu msaidie Mwenze basi ili mambo kama hayo yasijirudie. Okoeni kikapu na kiwe kama mlivyocheza nyie.

Na ni wakati sasa wa Magesa kukubali kwamba TBF imekuwa kubwa zaidi kwako na kinachoonekana ni mchezo huu kwenda kuzikwa kaburini. Amua moja kuachia kila kamati ifanye kazi yake wewe upokee taarifa tu ya utekelezaji na yule ambaye hafanyi kazi yake unapaswa kumuwajibisha.

Naamini ndani ya shirikisho hilo hakuna kiongozi ambaye amewajibishwa kwa uzembe ama kosa lolote na ndiyo maana hata timu inaposafiri bendera ya Taifa inakabidhiwa tu kiholela bila hata kuwepo mwakilishi kutoka serikalini. jambo ambalo si rahisi kwa serikali kushindwa kutuma hata mwakilishi kuikabidhi timu ya taifa bendera.

Kama kuishirikisha serikali kwenye jambo kama hili tu inakuwa shida, je mtakapopeleka kilio chenu cha msaada mtasikilizwa? Haya ni mambo ambayo yatamwangusha Magesa pamoja na jitihada zake ambazo baadhi zinaonekana kuwa nzuri.

Magesa ana nguvu ndani ya TBF kwa mujibu wa Katiba lakini anazidiwa sana, mtu mmoja huwezi kusimamia kila kitu, wengi wapo kama vivuli tu kwasababu Magesa amejitwisha kila kitu mwenyewe pasipo kujionea huruma hata kama anaona jahazi linazama.

Timu ya Taifa imerudi, Magesa amesema kushiriki na kushinda mechi moja ni moja ya kupiga hatua, binafsi sidhani kama huko ni kupiga hatua, bali ni kufeli kabisa.

Magesa una kila kitu kwa maana ya macho, masikio na ufahamu iweje ujirundikie mzigo wote huo na baadaye uje ubebe lawama?

Advertisement