TIMUA VUMBI : Ligi hazina haraka kwasasa, afya kwanza

Muktasari:

Juzi Jumanne, Serikali kupitia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa taarifa nyingine ya kuongeza muda wa kusimamishwa kwa shughuli za mikusanyiko na mara hii bila ya kutoa muda maalulm akieleza kwamba kusimama kutaendelea hadi Serikali itakapotangaza vinginevyo.

SERIKALI imejumuika katika mapambano dhidi ya tatizo linaloisumbua dunia la ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona. Mambo mengi yamesimama.

Kuanzia serikalini hadi kwenye taasisi binafsi kote wanapigana kuona ni namna gani janga hili linakwisha.

Hivi karibuni, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema hivi sasa maambukizi ya ugonjwa huo yamekuwa ya ndani na si tena kutoka kwa wageni wanaoingia kutoka nje za nchi.

Alisema hatua hiyo inahitaji kila mmoja wetu kujumuika katika mapambano ya kuona ni namna gani tunaishinda hii vita, kwa sababu vita ya corona si ya serikali pekee bali kila mmoja kwa nafasi yake kwa kufuata masharti na maelekezo yanayowekwa na wataalam wa afya.

Huu sio ugonjwa kwamba unachagua rika, rangi ama watu wa kipato fulani. Kila mmoja yuko hatarini, hivyo kila mtu popote alipo anapaswa kushiriki mapambano dhidi ya corona.

Awali serikali iliagiza kusimama kwa shughuli zote zinazohusu mikusanyiko kwa siku 30 huku ikizifunga shule kuanzia chekechea hadi vyuo. Hii ilimaanisha mìchezo yote na mambo yote yanayosababisha kuwepo na mikusanyiko yalisimamishwa.

Juzi Jumanne, Serikali kupitia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa taarifa nyingine ya kuongeza muda wa kusimamishwa kwa shughuli za mikusanyiko na mara hii bila ya kutoa muda maalulm akieleza kwamba kusimama kutaendelea hadi Serikali itakapotangaza vinginevyo.

Huu ni uthibitisho kwamba mapambano ni lazima yaendelee katika kukabili tatizo hili ambalo limechukua maisha ya maelfu ya watu duniani.

Sio taarifa za kuzipuuza hizi. Kama serikali inapambana kuwajali wananchi wake hivyo hakuna sababu hata michezo kufikiria kuendelea hata bila mashabiki kwani hakuna ulazima wowote wa kufanya hivyo na kuhatarisha maisha ya wachezaji.

Shirikisho la Soka nchini (TFF) lilisema watasubiri serikali inatoa tamko gani na endapo wataruhusu ligi zote kuendelea basi mechi zingechezwa pasipo mashabiki lakini kwa sasa ni wazi jambo hilo halipo.

TFF na Bodi ya Ligi sasa wanapaswa kukaa na kufikiria nini kifanyike juu ya ligi hizo ambazo zilikuwa zinaelekea ukingoni ambapo mwezi ujao Mei ndo ilikuwa mwisho. Nadhani hapa kuna haja ya kuwa na uamuzi mwingine mgumu.

Wenye mpira wenyewe duniani Fifa tayari walisema hawana haraka ya kuendelea na mashindano mbalimbali kwani hali ni mbaya kote hivyo TFF kama mwanachama wa FIFA nao wanapaswa kufikiria mbele zaidi hasa kwa kujali afya za wachezaji wao.

Mbaya zaidi kipindi hiki pia ni cha kuelekea usajili mkubwa ambao kikawaida unaanza Juni lakini kwa hali iliyopo sidhani kama timu nyingi zinaweza kufanya hivyo kwani hatma ya ligi haijulikani.

Fifa imeshasema kwamba wachezaji ambao mikataba yao inatarajiwa kumalizika Juni wataendelea kuzitumikia klabu zao hadi pale msimu huu utakapomalizika, iwapo ligi zitarejea kumaliziwa baada ya janga la corona kumalizika.

Timu nyingi kwa mfano zile ambazo zinatwaa ubingwa kwenye ligi zao zinashiriki michuano ya kimataifa ya Caf lakini ni nani mwenye uhakika wa kwamba michezo ama mikusanyiko itaruhusiwa kwa wakati ili kuiwahi michuano hiyo ambayo huanza Agosti?

Ni jambo la kufikirisha kidogo kuwa mwaka huu michezo hasa soka mwisho wake utakuwaje maana kwa upande wa michezo mingine ratiba zao wamezisogeza hadi mwakani 2021. Je huku itakuwaje ingawa nako mashindano ya Ulaya yamesogezwa mbele.

Bado tubaki pale pale kwamba afya kwanza halafu soka baadaye hadi hali itakapotengamaa kabisa.

Viongozi wa mashirikisho wakubali kwamba mwaka huu ni mgumu kwao na taifa zima kwa ujumla.