MZEE WA UPUPU : Mkude na tatizo la ‘mentality’ kwa wachezaji wetu

Tuesday March 24 2020

Mkude na tatizo la ‘mentality’ kwa wachezaji wetu,Azam FC ,Crystal Palace,Ruvu Shooting ,

 

NILIWAHI kuongea na kocha fulani wa zamani wa Azam FC kuhusu kukwama kwa kwa timu hiyo.

Akasema kuna mambo mengi sana, lakini kikubwa na cha kwanza ni namna ya kufikiri na kuyapima mambo (mentality) ya wachezaji wa klabu hiyo.

Kocha huyo anasema hakuwahi kutumia muda mwingi kufundisha mpira klabuni hapo, bali kuwajenga wachezaji kisaikolojia.

Anasema wachezaji wa Azam ni kama watoto wa shule ya msingi ambao wanasubiri kengele ilie warudi nyumbani. Watoto ambao akili yao haipo darasani. “Siku moja nilikuwa naongea nao, kila ninayemwangalia naona akili yake haipo katika mazungumzo yetu. Nikanyamaza kama dakika moja hivi...hayupo aliyegundua kama nimenyamaza.

“Baadaye nikasema kwa nguvu wote wakashtuka kama watu ambao walikuwa usingizini. Ikabidi nianze kuongea na mmojammoja kwa wakati wake, maana kwa pamoja hakuna aliyekuwa akinisikiliza”.

Kocha huyo akamalizia kwa kusema, “wachezaji wa Azam ni kama watu wenye kinyongo fulani. Wanapata kila kitu lakini saikolojia yao imekaa kana kwamba kuna kitu wanakosa, hivyo hawana furaha. Ukiifundisha Azam inabidi utumie muda mwingi sana kuwatengeneza wachezaji kiakili kabla ya mbinu na ufundi.”

Advertisement

Oktoba 27, mwaka jana, Azam ilifungwa 1-0 na Ruvu Shooting kule Mlandizi. Wakati wa kurudi, basi lao lilipata hitilafu kidogo. Cha kushangaza wengi wao walikuwa wanalalamikia matokeo ya Arsenal siku hiyohiyo, kukubali kupoteza uongozi wa 2-0 hadi sare ya 2-2 dhidi ya Crystal Palace, badala ya kuumia na matokeo yao.

Hapo ndipo nikaamini kauli ya kocha yule, kwamba wachezaji wa Azam akili yao haipo kwenye klabu yao ipo sehemu nyingine kabisa.

‘Mentality’ hii ya wachezaji wa Azam ndiyo inayolitafuna soka letu. Jonas Mkude, kiungo mkabaji wa klabu ya Simba na timu ya taifa amezua jambo kubwa sana hivi karibuni kuhusu kuripoti kwenye kambi ya timu ya taifa.

Mkude ambaye ameitumikia Simba tangu ajiunge nayo 2010 katika timu ya vijana, hakuwahi kuwa tegemeo kwenye timu ya taifa hadi ujio wa Etienne Ndayiragije kama kocha mkuu.

Mrundi huyu ambaye Mungu amemjalia karama ya kuongea na watu, amejitahidi sana kumfanya Mkude ‘ajisikie yuko nyumbani’ akiwa kwenye timu ya taifa. Nilipata simulizi moja ya kiuandamamizi kutoka kambi ya timu ya taifa ilipokuwa Kenya kwenye mchezo wa marudiano kufuzu Chan.

Kocha alifanya mazungumzo maalumu na Mkude wakiwa peke yao.

Inasemekana huo ndio ugonjwa wa Mkude....damu yake haiwezi kutiririka kwenye mishipa bila ‘kuchangamshwa’.

Hivyo Ndayiragije akamuweka sawa halafu akakaa naye akimueleza kile anachohitaji kutoka kwake kwenye huo mchez Mkude akatikisa kichwa na kusema, “Mwalimu, hilo limeisha.”

Na kweli, Stars ikafuzu kwa kuwaondoa Kenya kwa mikwaju ya penalt baada ya Mkude kuziba njia za mianya kuelekea kwenye safu yake ya ulinzi kwa dakika zote 90.

Lakini ni bahati mbaya sana inadaiwa kwamba ilipoitwa kambi nyingine Novemba 2019 kujiandaa na mechi mbili za kufuzu Afcon 2021 dhidi ya Guinea ya Ikweta na Libya. Mkude hakufika kambini na wala hakukuwa na taarifa yoyote huku akiwa hapatikani kwenye simu.

Baada ya siku mbili ndiyo akaripoti kambini na kusema alikuwa na matatizo ya kifamilia, akidai mwanaye alikuwa anaumwa.

Mrundi wa watu masikini, Ndayiragije, akamwambia, “kama una mwanao anaumwa, nenda kaendelee kumuuguza sisi sote hapa ni wazazi na tunajua uchungu wa mtoto”.

Lakini kumbe inadaiwa Mkude hakuwa na mtoto anayeumwa wala matatizo yoyote ya kifamilia, ni kwamba mambo yake ya ujana yalimzidi akajikuta amechelewa kuripoti kambin, hivyo akajificha kwenye kichaka cha matatizo ya kifamilia.

Alipoambiwa arudi kwenda kuendelea kuyatatua kijasho kikamtoka kwa sababu ukweli ni kwamba hakuwa na matatizo.

Basi aliendelea kushinda kambini hadi jioni inadaiwa watu wakawa wanaulizana, “huyu si ana matatizo ya kifamilia sasa anangoja nini muda wote hapa?”

Safari hii tena, kambi imeitwa Mkude hayupo na hakuna taarifa kuhusu uwepo wake. Mkude anawakilisha kundi kubwa la wachezaji wetu na matatizo yao ya ‘mentality’.

Wakati kocha wa Stars akiwa Salum Mayanga, inadaiwa Ibrahim Ajibu aliwahi kutoonekana kambini.

Mayanga na busara zake hakutaka kulisema hilo hadharani. Akaongea naye na akamwambia nakuacha kama adhabu. Na kweli hakwenda naye kwenye Cosafa ya 2017. Mentality.

Advertisement