MTU WA PWANI : Safari ya Ulaya ianze sasa kwa Shomary Kibwana

Friday February 7 2020

 Safari ya Ulaya ianze sasa kwa Shomary Kibwana,beki wa kulia wa Mtibwa Sugar, Kibwana Ally Shomary ,timu ya African Lyon ,Samatta Aston Villa,

Beki wa kulia wa Mtibwa Sugar, Kibwana Ally Shomary 

By Charles Abel

Pasipoti ya beki wa kulia wa Mtibwa Sugar, Kibwana Ally Shomary inaonyesha kuwa sasa ana umri wa miaka 20.

Taarifa rasmi za umri wake ambazo zipo katika pasipoti anayomiliki, zinaonyesha na kuthibitisha kwamba beki huyo wa kulia alizaliwa mnamo Januari Mosi, 2020.

Katika kipindi cha umri wa miaka 20 kama alionao yeye, nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ anayechezea Aston Villa ya England, Mbwana Samatta alikuwa ameshaondoka nchini na kutua DR Congo na kwa muda huo alikuwa mchezaji tegemeo wa kikosi cha kwanza cha timu hiyo inayomilikiwa na bilionea Moise Katumbi.

Ikumbukwe kuwa Samatta alijiunga na Mazembe akiwa na umri wa miaka 19 wakati huo akichezea Simba ambayo ilimnasa kutoka timu ya African Lyon ambayo awali ilikuwa ikijulikana kama Mbagala Market.

Lakini katika umri huo tayari nyota aliyewahi kutamba katika klabu ya Manchester United, Wayne Rooney alikuwa ameshakuwa staa maarufu katika Ligi Kuu ya England na alikuwa mwiba kwa walinzi wa timu pinzani.

Ipo mifano ya kundi kubwa la wachezaji ambao katika umri wa miaka 20 tayari wamekuwa wakitamba katika ligi mbalimbali na kuwa tegemezi katika vikosi vya timu zao za taifa kutokana na kiwango bora ambacho wamekuwa wakionyesha. Ni kama ilivyo kwa Kibwana Shomary ambaye ni vigumu kwa wafuatiliaji wa soka la Tanzania kushindwa kulitaja jina lake pale wanapokuwa wakijadili mabeki wa pembeni ambao wanafanya vizuri kwa sasa katika mashindano ya ndani kama vile Ligi Kuu na Kombe la Azam Sports Federation.

Advertisement

Kibwana Shomary ana kila kitu ambacho kinahitajika kwa beki wa kulia kuwa nacho mfano uwezo wa kudhibiti washambuliaji wa timu pinzani, kasi, kusaidia mashambulizi na kutengeneza nafasi hasa kupitia mipira ya krosi.

Umri na umbile limemfanya awe mnyumbulifu na mwenye uamuzi wa haraka juu ya wapi apeleke mpira pindi unapokuwa miguuni mwake, anatumia zaidi akili anatumia akili nyingi pindi anapomkabili mahambuliaji wa timu pinzani.

Huyu ni mchezaji ambaye anaweza kuwa hazina na mwenye mchango mkubwa kwa Taifa Stars siku za usoni katika nafasi ya beki wa kulia ambayo katika siku za hivi karibuni imeonekana kutetereka.

Hata hivyo hilo kwa kiasi kikubwa linaweza kutimia ikiwa tu beki huyo ataondoka sasa kwenda nchi za ng’ambo kwa ajili ya kucheza soka la kulipwa huko.

Ni mahali ambako kutamuimarisha na kumfanya awe mchezaji wa daraja la juu kama ambavyo tunaona sasa kwa nahodha wa Stars, Mbwana Samatta na mshambuliaji Saimon Msuva ambaye anacheza soka la kulipwa nchini Morocco katika klabu ya Difaa El Jadida.

Akiwa huko atafundishwa kuishi katika misingi ya weledi kisoka, ataimarishwa kimbinu na kiufundi jambo ambalo litamfanya awe beki mahiri zaidi na mwenye msaada mkubwa kwa Taifa Stars.

Na hii haipaswi kuishia kwa Kibwana Ally Shomary pekee bali hata vijana wengine wanaocheza nafasi ya ulinzi hasa mabeki wa pembeni kama vile Israel Patrick wa Alliance FC, Ally Ramadhan ‘Oviedo’ wa KMC, Dickson Job wa Mtibwa Sugar na Gustaph Saimon wa Yanga.

Kwa nini kundi kubwa la vijana wanaocheza katika nafasi ya ulinzi ndio liwe kipaumbele cha kwenda nje ya nchi kusakata soka la kulipwa kwa sasa? Ni kwa sababu taifa linakosa idadi kubwa ya wachezaji wa daraja la juu ambao wanacheza nafasi ya beki.

Ni idara ambayo mara kwa mara imekuwa ikiiangusha Taifa Stars katika mechi za mashindano mbalimbali ambayo imekuwa ikicheza na sababu kubwa inayopelekea hilo ni makosa ya mara kwa mara ya kimbinu na kiufundi ambayo kaka zao wamekuwa wakiyafanya katika timu hiyo.

Kumekuwa hakuna mwendelezo wa ubora kwa walinzi wa Stars na viwango vyao vimekuwa kama homa za vipindi ambapo kuna wakati wamekuwa wakicheza vizuri na muda mwingine hufanya vibaya na kuigharimu timu hiyo. Hayo ni matokeo ya kukosekana kwa maandalizi ya uhakika wakiwa katika klabu zao ambazo nyingi zinakosa miundombinu bora na wataalam kama vile wa lishe, matibabu na ufiti jambo ambalo limesababishwa na hali duni ya kifedha ambayo klabu hizo zinazo.

Tukifanikiwa kuwapeleka nje mapema hawa akina Kibwana Shomary na wenzake, pengine tutakuwa na uwezekano wa kutibu tatizo hilo la upungufu wa wachezaji wa daraja la juu wanaocheza katika nafasi za ulinzi.

Advertisement