MTU WA PWANI : Kagera na Prisons haziwezi kuwa Leicester City

Friday November 15 2019

MTU - PWANI- Kagera - Prisons -haziwezi - Leicester City- Ligi Kuu -Tanzania- Bara -Mwanasport-MwanaspotiSoka-MwanaspotiGazeti-

 

By Charles Abel

MAFANDE wa Tanzania Prisons na ‘Wakata Miwa’ wa Kagera Sugar wamekuwa moto wa kuotea mbali katika Ligi Kuu Tanzania Bara tangu msimu ulipoanza hadi sasa.

Kagera Sugar inayonolewa na Mecky Mexime inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa imekusanya pointi 20 baada ya kupata ushindi katika mechi sita, kutoka sare mbili na kupoteza michezo miwili.

Habari ya kufurahisha zaidi kwa Kagera Sugar imekuwa ndio timu tishio zaidi ugenini kwani haijapoteza mchezo wowote ugenini na ndiko imevuna idadi kubwa ya pointi kuliko katika uwanja wake wa nyumbani.

Ikumbukwe ni msimu uliopita tu, iliponea chupuchupu kushuka daraja na ilijikuta ikilazimika kucheza mechi za hatua ya mchujo dhidi ya Pamba ya Ligi Daraja la Kwanza na kuibuka na ushindi wa jumla wa mabao 2-0 ambao uliihakikishia kubaki Ligi Kuu.

Upande mwingine, Tanzania Prisons imekuwa mwiba kwa timu pinzani kutokana na kiwango bora inachokionyesha katika mechi ambazo imekuwa ikicheza msimu huu na hadi sasa ipo nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi kutokana na idadi ya pointi 16 ilizokusanya.

Inaweza kuwa ndio timu inayoumiza vichwa vya timu pinzani kwani hadi sasa haijapoteza mechi yoyote ya Ligi Kuu ikiwa imepata ushindi katika jumla ya michezo mitatu na michezo saba iliyobakia, Maafande hao wametoka sare.

Advertisement

Prisons una hadithi inayokaribia kufanana kidogo na Kagera Sugar kwani msimu uliopita ilikuwa na hali mbaya katika Ligi Kuu na ilisubiria hadi dakika za lala salama ili iweze kubakia vinginevyo leo hii ingekuwa Ligi Daraja la Kwanza.

Kwa wafuatiliaji wa soka, hapana shaka wanakitafsiri kile kinachofanywa na Prisons na Kagera Sugar kwa muono uleule wa kinachofanywa na timu ya Leicester City ya Ligi Kuu ya England msimu huu.

Leicester hadi sasa inashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa imekusanya jumla ya pointi 26 ikipata ushindi katika michezo minane, kutoka sare mara mbili na kupoteza michezo miwili na imefumania nyavu mara 29 wakati huo nyavu zake zikiwa zimefumaniwa mara nane (8) tu ikiwa ndio timu iliyoruhusu idadi ndogo zaidi ya mabao.

Wakati timu vigogo kama Manchester United, Arsenal na Tottenham wakiwa wanataabika katika ligi hiyo, Leicester inazidi kuchanja mbuga na kwa kiwango inachokionyesha kwa sasa imeanza kutajwa kama mshindani halisi wa Liverpool katika mbio za ubingwa kama ilivyo kwa Manchester City.

Na kama Liverpool na Manchster City zitashindwa kujipanga vizuri, zinaweza kujikuta zikiliacha taji hilo kwa Leicester ambayo iliwahi kutwaa ubingwa kwa staili kama hiyo katika msimu wa 2015/2016.

Hata hivyo, wakati timu hizo tatu zikifanya kitu kinachofanana katika ligi zao msimu huu, haionekani ni rahisi na wala hakuna matarajio ya watu kwamba Prisons na Kagera Sugar zinaweza kutwaa ubingwa au kuleta ushindani hadi mwisho katika kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kama wanavyoitazama Leicester City pale England.

Kuna sababu kadhaa ambazo zinachangia kwamba ni vigumu kwa Prisons na Kagera Sugar kuwa mabingwa wa Ligi Kuu msimu huu tofauti na wanavyoitazama Leicester. Kwanza ni miundombinu ambayo inatumika na timu hizo katika programu zao. Wenzetu Leicester City wana miundombinu bora na ya kisasa kuanzia ile ya kuwaandaa kiufundi kama viwanja, kumbi za mazoezi na huduma za kuweka sawa miili wachezaji baada ya mchezo au mazoezi na hata ya usafiri tofauti.

Kagera Sugar na Prisons hazina miundominu ya kisasa katika ufanyaji wa programu zake za kiufundi lakini kana kwamba haitoshi, wachezaji wa timu hizo wanalazimika kusafiri umbali mrefu kwa njia ya barabara jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linachangia kuwachosha na kupoteza ubora wao kadri ligi inavyozidi kupiga hatua.

Upo uwezekano wa nyota muhimu wa Kagera Sugar na Prisons kuondoka katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo ambacho kitaanza Desemba 15 hadi Januari 15 jambo ambalo litawalazimu kuanza kusuka upya timu baada ya dirisha hilo kufungwa. Haya yote yapo chini ya sababu moja kubwa ambayo ni idadi kubwa ya timu zetu kutokuwa na nguvu ya kiuchumi kumudu kujiendesha kisasa kama Leicester City.

Kama Prisons na Kagera zingeshiriki Ligi Kuu ya England, ingeweza kuwa rahisi kuzitazama kama washindani halisi wa ubingwa lakini ukitafakari mazingira ambayo yamezizunguka, inatafakarisha kuzivalisha viatu vya Leicester City.

Advertisement