MTAA WA KATI : Ubingwa wa hivi Ligi Kuu hauwezi kuwa mtamu

Tuesday March 17 2020

Ubingwa wa hivi Ligi Kuu hauwezi kuwa mtamu,Ligi Kuu England ,Liverpool ,hofu ya maambuzi ya virusi vya Corona,

 

By Said Pendeza

HAKUNA ubishi. Hakuna anayepinga. Hakuna asiyekubali ubora ulionyeshwa na Liverpool kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Walikuwa na msimu bora kabisa. Pengo la pointi 25 kileleni, pointi sita pungufu ya kunyakua taji hilo, ni jitihada kubwa zilizofanywa na wachezaji wa timu hiyo pamoja na benchi la ufundi katika kuhakikisha wanamaliza ukame uliowakabili kwa miaka 30 kubeba ubingwa wa ligi ya ndani.

Pointi sita tu zimebaki kwa Liverpool kubeba ubingwa huo. Wamebakiza mechi tisa. Lakini kwa wachezaji wa Liverpool hakuna namna ni kusubiri tu.

Kuna mjadala wa kuhusu hatima ya ligi hiyo baada ya kusimama kwa sasa kutokana na hofu ya maambuzi ya virusi vya Corona.

Mjadala ni mzito, kipi kifanyike, kipi kitatokea kama madhara ya Corona yatakuwa makubwa kiasi cha kufanya ligi ishindwe kuendelea hadi hiyo mapema Aprili ilipopangwa baada ya kusimamishwa.

Je, Liverpool wapewe ubingwa? Kama wakitajwa kuwa mabingwa, vipi hatima ya timu nyingine kama hilo litafanyika kabla ya ligi yenyewe kumaliIka?

Advertisement

Liverpool wao wamebakiza mechi tisa, lakini kuna baadhi ya timu wakiwamo Aston Villa wao wamebakiza mechi 10 ambazo hakika kwao ni msingi mkubwa katika vita yao ya kukwepa kushuka daraja.

Kama ligi itamaliza sasa, basi wanufaika watakuwa Liverpool peke yao. Lakini, hilo litaingia kwenye historia isiyovutia sana kwa Liverpool, kwamba itasomeka, Liverpool walichukua taji lao la kwanza la Ligi Kuu wakiwa na pointi ambazo hazikutosha kuwapa taji hilo.

Sawa, Liverpool wameweka pengo la pointi 25, lakini bado hawajafikisha pointi zinazotosha kubeba ubingwa. Wanahitaji pointi sita zilizobaki kuwapa hadhi ya kubeba taji lao la kwanza.

Kinyume cha hilo, kama watapewa ubingwa kwa sasa, basi jambo hilo litawapa nguvu wapinzani wao kuwasakama, kwamba wamepewa ubingwa wa mezani.

Jambo hilo litakwenda hadi kwa wachezaji wake, hawatakuwa na ile furaha ya utamu wa kubeba ubingwa kwa kucheza hadi mwisho kwa kuwazidi wengine pointi za jumla.

Lakini, kuwapa ubingwa kwa sasa kuna maana ya kukubali ligi iwe imekwisha jambo litakalozigusa timu nyingi, wakiwamo Man City, Man United, Chelsea, Tottenham, Arsenal, Leicester City, timu zinazopigania kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao na zile zinazosaka nafasi ya kubaki Ligi Kuu.

Hivyo mjadala wa kumaliza ligi kwa hapa ilipofika kwa sasa itakuwa na hasara kwa timu nyingi kuliko faida.

Hata Liverpool hawatafurahia hilo la ubingwa wa kupewa. Kwa hivyo njia pekee iliyobora ni kucheza hadi mwisho wa ligi, kila mmoja afahamu alichovuna baada ya kucheza mechi zake zote 38 kwa msimu.

Kinyume cha hapo basi kusiwepo na washindi wala walioshindwa, kitu kianze upya.

Kwenye kijiwe cha Mtaa wa Kati, wanakijiji wanasema Liverpool wanapaswa kujitazama, bila shaka watakuwa na gundu la ubingwa wa ligi.

Kuna ukweli? Hilo sijui. Ila kiwango cha Liverpool ya msimu huu, kumaliza bila taji itakuwa kitu cha kikatili zaidi kuwahi kutokea kwenye mchezo wa soka.

Taji lililobaki kwenye himaya yao kwa sasa ni la Ligi Kuu England pekee.

Ndoto yao ya kubeba mataji matatu makubwa imeyeyuka ndani ya wiki chache tu, wakatupwa nje kwenye Kombe la FA, kisha kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na kufanya Liverpool inayoonekana kuwa timu bora zaidi kuwahi kutokea kwenye muongo huu kuwa kwenye hatari ya kumaliza ligi bila ya taji.

Chelsea imewavuruga kwenye Kombe la FA, Atletico Madrid kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na Corona inataka kuwavurugia kwenye Ligi Kuu England.

Kuna mkono wa mtu si bure.

Advertisement