MTAA WA KATI : Klopp, Pep ni vita huko Anfield wikiendi hii

Tuesday November 5 2019

Klopp-Pep-Anfield-Liverpool- Man City-Liverpool-Aston Villa-Michezo blog-Mwanasport-MwanaspotiGazeti-MwanaspotiSoka-

 

By Said Pendeza

POINTI 31 kwa 25. Tofauti ya pointi sita hizo.

Msimu uliopita uliisha kwa pointi 98 kwa 97. Tofauti ya pointi moja.

Hilo linazihusu timu mbili, Liverpool na Man City. Ndio wanaonekana kuwa watalawa wa Ligi Kuu England ndani ya misimu miwili ya karibuni. Msimu uliopita, Man City waliibuka wababe, wakibeba ubingwa kwa tofauti ya pointi hiyo moja dhidi ya Liverpool.

Hakika ulikuwa msimu ambao Liverpool pengine hawakustahili kuukosa ubingwa huo. Walipoteza mechi moja tu, wakati Man City walipoteza mechi nne. Kitu kilichowaponza Liverpool ni sare, walitoka saba, wakati wenzao Man City walitoka sare mbili.

Msimu huu, mambo ni yaleyale, vita ni ya Man City na Liverpool. Lakini, kocha Jurgen Klopp anaonekana kumeza mate ya akili, kumaliza kile kilichomshinda kukimalizia msimu uliopita.

Liverpool sasa imeweka pengo la pointi sita kileleni dhidi ya Man City kwenye nafasi ya pili.

Advertisement

Mechi zao 11 Liverpool walicheza kwenye ligi, wametoka sare moja tu, nyingine zote wameshinda. Walitoka sare na Man United, mechi ambayo wengi walidhani wangepoteza.

Kwa inavyoonekana Liverpool ya msimu huu, wamekuwa wagumu sana kupoteza.

Jumamosi iliyopita ilifunga mabao mawili ndani ya dakika sita za mwisho kuandikisha ushindi dhidi ya Aston Villa. Hicho ndicho kinachomtia homa Pep Guardiola.

Lakini, pengo hilo la pointi litaweza kuzidi kuwa tisa au kufungua kuwa pointi tatu baada ya Jumapili ijayo. Wababe hao wawili watakutana Jumapili huko Anfield.

Liverpool inaamini ushindi utakaowafanya waweke pengo la pointi tisa, basi litakuwa mtihani mzito kwa Guardiola kulifikia kutokana na uchezaji wa kikosi chake kwa msimu huu.

Hadi sasa tayari Man City imeshapoteza mara mbili na kutoka sare moja. Tena mechi ilizopoteza, imefanya hivyo dhidi ya Norwich City na Wolves.

Mechi hiyo ya Anfield inabeba taswira nzima ya ubingwa wa Ligi Kuu England licha ya kwamba inafanyika kwenye mwezi huu wa Novemba. Bado miezi kibao kufika Mei mwakani na chochote kinaweza kutokea hapo kati.

Lakini, kwa mwendo wa Liverpool msimu huu kwa namna wanavyotafuta matokeo uwanjani, unaona wazi kabisa wamedhamiria kumaliza ukame wa kulibeba taji hilo. Inatosha kwa muda waliokaa kusubiri kubeba taji hilo. Kisha wanacheza Anfield, mahali ambapo mechi yao ya mwisho ya ligi kupoteza uwanjani hapo ilikuwa Aprili 2017.

Hiyo ni rekodi tamu inayowafanya Liverpool kuwa na uhakika wa kuweka pengo la pointi tisa itakapowakabili Man City licha ya kwamba ni mabingwa wa ligi hiyo kwa miaka miwili mfululizo.

Unatarajia upinzani mkali wa kwenye mechi hiyo kuanzia filimbi ya mwisho hadi ya mwisho. Hakika kipute hicho cha Anfield ni moja ya mechi zitakazokuwa tamu kuzitazama kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Ukikosa basi umepitwa na uhondo, licha ya Guardiola kuwa kwenye wakati mgumu kutokana na kuwa na shida kubwa kwenye mabeki wake, lakini pia akimpoteza kiungo wake mchezeshaji, David Silva kwa maumivu ya misuli.

Advertisement