MTAA WA KATI : Juventus inavyoonyesha bure sio gharama

Wednesday October 30 2019

 

By Said Pendeza

KIPIGWE hapo. Man United na Juventus kipi kitatokea. Kwenye karatasi ni rahisi sana kutabiri matokeo ya mechi hiyo.

Hata ikitokea Juve inacheza na Arsenal ni rahisi kutabiri kwa kuzitazama timu hizo mbili kwenye karatasi. Ikipigwa mechi ya Juve na Liverpool. Juve na Real Madrid, Barcelona, PSG ua Bayern Munich, utasema patachimbika.

Utakuwa na ugumu kidogo wa kutabiri upande upi utaibuka na ushindi.

Lakini, Juventus ni tofauti kabisa na timu zote hizo. Zenyewe zinautazama mchezo wa soka na thamani ya wachezaji katika jicho la peke yao kabisa.

Ni staili kali inayowapa faida ya kulitawala soka la Italia na Ulaya. Kwa misimu kadhaa ya hivi karibuni imekuwa ikitinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Bahati tu ndicho kitu kinachoifanya ishindwe kubeba taji hilo. Lakini, mpira inaupiga.

Tofauti ya Juventus na vigogo wengine wote hao ni matumizi ya pesa.

Advertisement

Arsenal inatumia pesa kwenye kusajili, Man United ndio kabisa sawa na Bayern Munich, Real Madrid, PSG, Barcelona na vigogo wengine wanafikiria kwenye kutumia pesa zaidi kupata mafanikio.

Lakini Juventus imebeba ubingwa wa Serie A kwa misimu minane mfululizo, ukitazama kwenye safu ya kiungo ya timu hiyo, imejaa wachezaji kibao wa bure.

Inachokifanya Juve ni kufuatilia tu mikataba ya wachezaji wa timu nyingine, ikiona kuna yule inayomhitaji kwenye timu yao, inawahi haraka kumsainisha mkataba wa awali na kumbeba bure kabisa. Cheki kwenye dirisha lililopita, imewanasa bure Aaron Ramsey na Adrien Rabiot.

Lakini huko nyuma iliwanasa viungo matata kabisa bila ya kulipa chochote kama Andrea Pirlo, Paul Pogba, Emre Can na Sami Khedira kwa kuwataja kwa uchache. Mastaa wote hao walionekana wamechoka na hawafai kabisa huko walikotoka, lakini walipotua Juventus wamekuwa wenye faida kubwa.

Hapo hujawataja wachezaji wengine kama Dani Alves, aliyeonekana hana kitu huko Barcelona.

Kwa sasa imetegesha ndoano yake kwa Christian Eriksen. Tottenham Hotspur isipomshawishi kusaini dili jipya hadi kufikia Januari, basi mabosi wa Juventus wameshajiandaa kwenda kumsainisha mkataba wa awali staa huyo akakipige kwenye timu yao mwishoni mwa msimu.

Hiki ndicho kitu ambacho Juventus imekuwa ikikifanya kwa mafanikio. Man United kwa sasa inasumbukia ubingwa wa Ligi Kuu England,sawa na ilivyo kwa Arsenal na Liverpool licha ya kutumia pesa nyingi. Juventus imeweka vyema karata zake na kunasa wachezaji wa bure wakali na kuzitesa Inter, AC Milan na Napoli, ambazo zimekuwa zikitumia pesa nyingi kusajili.

Kuna ulazima wa vigogo wa soka kufikiria kuiga mtindo huo wa Juventus hasa katika kipindi hiki cha mdororo wa kiuchumi duniani pamoja na kuepuka suala la kubanwa na Uefa kwenye masuala ya usawa wa kipato na matumizi kwenye klabu.

Jambo hilo linaifanya Juventus kuwa salama, kwani kitu ambacho inakifanya ni kulipa tu mishahara mikubwa wachezaji wake. Zaidi ya hapo, imekuwa tu ikipata huduma bora kabisa kutoka kwa wachezaji wa bure na kuwaletea faida.

Ilitoa pesa zake kumsajili Cristiano Ronaldo na beki Matthijs de Ligt kwa ajili ya kufukuzia taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Itafanya hivyo kwa Kylian Mbappe kuboresha zaidi kikosi chake. Lakini zaidi ya hapo, itatumia muda mwingi kuwanasa wachezaji wa bure, ambao wamekuwa na faida kubwa kwenye timu. Suala la kujifunza hapo ni hili, Juventus inafanyaje kushinda dili matata za wachezaji wa bure? Kitu hicho kinaonekana hakipewi nafasi kwenye timu nyingi za Ligi Kuu England. Liverpool kwa sasa inafaidi tu huduma bora ya bure kutoka kwa beki wa kati Joel Matip.

Norwich City inaye pia Teemu Pukki, kumbe hilo ni eneo ambalo timu zingeweza kulichangamkia kama fursa katika kupunguza matumizi makubwa ya pesa kama wanavyofanya Man United na Man City.

PSG nayo ilinasa huduma ya Ander Herrera bure na anapiga mzigo. Kumbe kuna cha kujifunza kwenye kuiga staili hiyo ya Juventus na kufuatilia wachezaji wakali wanaomaliza mikataba yao ili kuwanasa bure kuboresha vikosi vyao. Vyabure vitamu.

Advertisement