MTAA WA KATI : Hakuna namna, Liverpool anachukua ndoo

Muktasari:

Kwa kasi hii ya kikosi cha Klopp huoni ni wapi watafeli washindwe kwenda kumalizia mkia waliobakiza baada ya kula ng’ombe mzima. Kama itashinda mechi zake zote, Liverpool itamaliza Januari hii ikiwa imeweka pengo la pointi 19 na hapo kutakuwa na mechi 14 za kucheza.

LIVERPOOL kitu ambacho inapaswa kufanya kwa sasa ni kuanza tu maandalizi ya namna watakavyoshangilia ubingwa wao. Haionekani kuwa kuna namna yoyote timu hiyo ikashindwa kubeba taji lao la kwanza la Ligi Kuu England baada ya kulisubiri kwa miaka 30.

Kila kitu kinakwenda sawa kwa upande wa Kocha Jurgen Klopp. Januari ya mwaka huu 2020 ilipoingia, kulikuwa na mtego wa mechi mbili mbele yake, dhidi ya Jose Mourinho na Ole Gunnar Solskjaer ilidaiwa kwamba ingekuwa na kitu cha kuamua kuhusu hatima ya Liverpool kwenye mbio zao za ubingwa. Lakini, kote huko imeweza kuvuka vigingi hivyo na sasa Liverpool imeketi kileleni kwa tofauti ya pointi 16 na ina mchezo mmoja mkononi.

Kwenye mechi 22 ilizocheza, imeshinda 21 na hiyo moja ambayo hawakushinda, ilimalizika kwa sare. Haijapoteza.

Kwenye msimamo imekusanya pointi 64 na kama ikikila vyema kiporo chao dhidi ya West Ham United basi itakuwa imefikisha pointi 70 na hapo itakuwa imecheza mechi sawa na wenzao. Hapo kama itakuwa imeshinda mechi yake ya Jumatatu ugenini kwa Wolves.

Kwa kasi hii ya kikosi cha Klopp huoni ni wapi watafeli washindwe kwenda kumalizia mkia waliobakiza baada ya kula ng’ombe mzima. Kama itashinda mechi zake zote, Liverpool itamaliza Januari hii ikiwa imeweka pengo la pointi 19 na hapo kutakuwa na mechi 14 za kucheza.

Hapo kila timu itakuwa imecheza mechi 24. Mechi 14 ni sawa na pointi 42. Hapo ina maana ukitoa pointi 19 itakuwa pointi 23.

Pointi hizo 23 ni sawa na michezo minane tu. Hivyo, kwenye mechi hizo 14 zitakazokuwa zimebaki, Liverpool itahitaji kushinda mechi nane tu kutokea Febrauri hadi Mei kubeba taji lao la kwanza la Ligi Kuu England.

Lakini, matokeo hayo ni kama Man City inayowafukuzia kwenye nafasi ya pili kama itaendelea kushinda mechi zake zote zilizobaki. Man City kutoka sare au kupoteza mchezo wowote katika mechi zake zilizobaki, hapo itakuwa na maana kwamba imeipunguzia mechi za Liverpool kutangaza ubingwa wa ligi msimu huu.

Namba hizo ndizo zinazofanya Liverpool kuwa kwenye nafasi kubwa ya kubeba ubingwa.

Ni muujiza tu ndio utakaofanya Liverpool isinyakue ubingwa wa ligi hiyo msimu huu. Suala la kubeba taji pengine si kitu kinachofikiriwa tena huko Anfield.

Pengine kwa sasa wanachofikiria ni kujaribu kuvunja rekodi ya Arsenal ya kucheza msimu mzima wa Ligi Kuu England bila ya kupoteza mechi.

Ushindi dhidi ya Man United umewapa nguvu kubwa na shangwe zilikuwa kubwa baada ya Mohamed Salah kufunga bao la pili kwenye dakika za majeruhi.

Liverpool ilifahamu usumbufu wa Man United inapokutana nayo, ambapo kwenye mechi sita zilizokuwa zimepita kabla ya hiyo Jumapili, walikuwa wameibuka na ushindi mara moja tu dhidi ya wapinzani wao hao wa miaka mingi.

Lakini, sasa Mo Salah alipopiga chuma cha pili, kila kitu kilionekana kimekwenda sawa katika mbio zao za kuukaribia ubingwa.

Liverpool itaingia Februari ikicheza na Southampton Anfield, Norwich City ugenini kisha West Ham Anfiend, kisha itatoka kwenda Watford na baada ya hapo itarudi nyumbani kuikaribisha Bournemouth, halafu itawabili mahasimu wao Everton huko Goodison Park, kisha itacheza na Crystal Palace Anfield ndipo wataenda Etihad kuikabili Man City.

Kwa ratiba hiyo, kama Liverpool itaendelea kushinda kila mechi, Man City nayo ikshinde kila mechi, basi Liverpool itakwenda kutangaza ubingwa wake Etihad kama itamchapa Pep Guardiola na timu yake kwenye mchezo huo utakaopigwa Aprili 4. Vitu viwili, Guardiola ili asikumbane na aibu ya Klopp kwenda kutangaza ubingwa mbele ya mashabiki wake huko Etihad, basi anapaswa kupoteza au kutoa sare hapo kati kabla ya mechi hiyo huku aombe Liverpool waendelee kugawa dozi zao.

Hakuna namna, Liverpool ubingwa wa ligi ni wao msimu huu baada ya kushindwa kufanya hivyo msimu uliopita walipobwagwa kwa pointi moja na City.