MTAA WA KATI : Hadithi tamu halafu chungu kuhusu Harry Kane

Muktasari:

Jose Mourinho anasema Spurs si timu inayopenda kuuza wachezaji wake, lakini Daniel Levy ameonyesha miaka kadhaa iliyopita kwamba si mgumu wa kuuza nyota wake wa kiwango cha juu pia, akifanya hivyo kwa Luka Modric, Gareth Bale na Christian Eriksen. Hivyo pengine na sasa anaweza akampiga bei Kane, ambaye atakuwa amebakiza miaka miwili kwenye mkataba wake itakapofika Juni mwaka huu.

HARRY Kane na Tottenham Hotspur. Hadithi tamu na chungu inayorudi upya. Kuna utamu na uchungu wake. Spurs wanalifahamu hilo.

Uchungu ni kwamba Spurs haitakuwa na uwezo wa kuzizuia klabu kuhitaji saini ya straika huyo. Mbaya zaidi kwao, timu zinazomtaka mshambuliaji huyo zote zina uwezo wa kifedha na zina sababu ya kuhitaji saini yake.

Timu hizo ni Man United, Man City na Juventus. Hicho ndicho kinachowapa shida Spurs, Kane hataweza kugomea ofa za timu zote hizo huku akijua umri wake unakwenda na kufahamu kwamba anahitaji kuwa na medali kadhaa za ubingwa wa kuja kudhihirisha ubora wake kwenye soka na kuja kuonyesha wajukuu zake, atakapozeeka.

Hiyo ndiyo chungu inayowakabili Spurs. Ni chungu itakazozikabili Man United, Man City na Juventus kama mmoja wao atashinda vita hiyo au kama watakutana na ngumu kutoka kwa Kane mwenyewe au Spura ikagoma kumuuza.

Tamu itakuja kwa timu itakayofanikiwa kupata huduma yake na kwa Spurs pia, kwa sababu wataingiza pesa nyingi kwenye kumpiga bei staa huyo.

Jose Mourinho anasema Spurs si timu inayopenda kuuza wachezaji wake, lakini Daniel Levy ameonyesha miaka kadhaa iliyopita kwamba si mgumu wa kuuza nyota wake wa kiwango cha juu pia, akifanya hivyo kwa Luka Modric, Gareth Bale na Christian Eriksen. Hivyo pengine na sasa anaweza akampiga bei Kane, ambaye atakuwa amebakiza miaka miwili kwenye mkataba wake itakapofika Juni mwaka huu.

Suala la Kane kuachana na Spurs mwisho wa huu linaonekana kwenda kutimia. Kwanini Kane ataondoka? Umri wake umekwenda na Spurs haionekani kama itamfanya kuwa na furaha tena ya kuwa kwenye timu hiyo. Hakuna mataji na timu imekuwa si tishio tena. Kitu kingine ni kwamba anatafutwa na timu zenye uwezo wa kumpatia furaha na mataji. Anatafutwa na timu zinazomhitaji kwelikweli.

Man United hivi karibuni ilimsajili Bruno Fernandes, lakini wanahitaji wachezaji wengine kadhaa wa kiwango cha dunia kwenda kucheza na Mreno huyo. Kane na mastaa wengine wachache ni miongoni mwa wachezaji wanaohitajika Old Trafford. Uwepo wa Bruno utamfanya Kane kwenda kufunga mabao kama anavyotaka atakapotua Old Trafford.

Man City wanamhitaji pia. Pep Guardiola anafahamu wazi Sergio Aguero umri unamtupa mkono hivyo anahitaji mtu wa daraja lake. Hapa anamwona Kane kuwa anamfaa.

Juventus wao wanamhitaji Kane aende akashirikiane na Cristiano Ronaldo. Mabosi hao wa Turin wanaamini Ronaldo amekosa mtu kama Karim Benzema kwenye kikosi chao, hivyo wanamtazama Kane kama jibu la kumaliza tatizo hilo.

Benzema na Ronaldo walitengeneza kombinesheni matata sana Bernabeu, hivyo Juve wanaamini wakimleta Kane kwenye timu yao basi watamfanya Mreno wao kuwa moto zaidi. Kwenye mambo hayo huoni namna gani Kane ataendelea kubaki Spurs msimu ujao.

Kwenye kikosi hicho bosi si Mauricio Pochettino. Bosi ni Mourinho mwenye mfumo mgumu na mgeni kwa wachezaji wa timu hiyo baada miaka kadhaa ya kuwa chini ya Muargentina, Pochettino. Maisha yamebadilika sana. Bila shaka Spurs msimu ujao hawaonekani kama watacheza michuano ya Ulaya.

Hilo ni tatizo jingine ambalo linaweza kumsukuma Kane nje ya klabu hiyo akasake malisho yenye afya zaidi. Lakini, kingine bila shaka atahitaji kufuata nyayo za wakali kama Modric na Bale, ambao tangu walipotoka Spurs, wamekwenda kubeba mataji kibao kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya wakiwa na chama la Los Blancos.

Kwa Kane haitashangaza pia kama Barcelona, Real Madrid na Bayern Munich nazo zikaingia kwenye vita ya kusaka saini yake. Timu zote hizo zinahitaji huduma ya mtu kama Kane. Barca wanatafuta mbadala wa Luis Suarez.

Madrid wanafahamu Benzema jua limeanza kuzama na Bayern wanahitaji nguvu nyingine ya ziada ya kuja kumsaidia Robert Lewandowski kama ataendelea kubaki kwenye kikosi chao. Sawa wanamhitaji Timo Werner, lakini kama wakifahamu Kane anapatikana hawawezi kujiweka nyuma. Hizi ni sababu nyingi za Kane kuwa na nafasi finyu kubaki Spurs kuliko kuondoka. Spurs itawauma, lakini huo ndio ukweli.