JICHO LA MWEWE: Wanaotusumbua ni hawa wachezaji 15 tu wa kigeni

Monday April 27 2020
Jicho pic

ULE mjadala wa wachezaji wa kigeni umerudi tena.

Majuzi wamejadiliwa bungeni pale Dodoma. Idadi ipunguzwe au isipunguzwe? Imezungumzwa na waziri husika kama vile wachezaji wa kigeni ni wengi sana na wanabana nafasi za wazawa.

Wala sio mjadala mpana kama wanavyotaka kuufanya. Sikia. Kuna timu tatu tu ambazo zina uwezo wa kujaza nafasi zote 10 za wachezaji wa kigeni klabuni. Yanga, Simba na Azam. Zimewahi kufanya hivyo siku za nyuma.

Timu nyingine hazina uwezo huo. Mara nyingi hazina mpango huo. Tunapojadili kuhusu hizo nafasi kupunguzwa mara nyingi inashauriwa kila klabu iwe walau na wachezaji watano tu wa kigeni.

Hii ina maana kama Simba, Yanga na Azam zikibanwa hapo basi tutakuwa na wachezaji 15 tu wa kigeni katika hizo timu. Wachezaji 15 wengine ndio ambao watafungiwa milango.

Hizi klabu nyingine bila ya kujali kanuni wala sheria tayari hazitimizi hata hao wachezaji watano. Hatuna muda wa kuzijadili hapa. Timu kama Mtibwa haitaki hata kuwa na wachezaji wa kigeni. Kwingine wapo wawili au mmoja.

Advertisement

Hata hivyo, tunajadili kama vile kila timu ya Ligi Kuu ina wachezaji 10 wa kigeni ambao wanabana nafasi za wazawa. Sio kweli.

Kwamba wachezaji wa kizawa wanabanwa sana kuonyesha makali yao, sio kweli. Wangeweza kuonyesha makali yao katika klabu kibao ambazo hazina wachezaji wa kigeni.

Kwa mfano, kama zamani timu zetu kubwa tatu zingeamua kwenda na mwendo huu wa wachezaji wa kigeni, bado Pamba ingebakia na wachezaji wake wakali wazawa kina Fumo Felician, Kitwana Suleiman, Hamza Mponda, Abdala Bori na wengineo.

Coastal ingeweza kubakia na mafundi wake kina Idrisa Ngulungu, Juma Mgunda, Kassa Mussa, Razak Yusuph, Hussein Mwakuluzo, Ally Maumba na wengineo.

Leo wachezaji wa vipaji vya namna hii hawapo katika klabu kama Ndanda na ndio maana inakuwa rahisi kulaumu wageni ambao ukichunguza wala hawajaziba nafasi katika klabu kama hizi.

Ukweli ni tunajaribu kulinda viwango vya wachezaji wetu wakati huu wakiwa katika viwango duni. Mbona hawaonyeshi viwango hivyo katika klabu nyingine ambazo zina wazawa wengi?

Lakini hapo hapo tunafahamu tuna wachezaji kibao wazawa katika klabu kubwa ambao wamegoma kujituma.

Tuna tatizo la viongozi wa klabu hizi tatu kuleta baadhi ya wachezaji wa kigeni ambao hawana uwezo.

Hapa tunakubali. Lakini kuna wachezaji wengi tu wa kigeni ambao wamekuwa mfano mzuri katika soka letu kwa miaka nenda rudi.

Kama Kagere asingekuwepo si ajabu mfungaji bora wa Ligi yetu mpaka sasa angekuwa mzawa mwenye mabao 11 tu. Kaangalie katika chati ya wafungaji bora wa msimu huu ndipo utagundua hili. Kwa nini tunataka kulindana katika ubovu?

Hawa wachezaji wa kigeni wamekuja kwa wingi nchini kwetu baada ya wazawa kulegalega. Jaribu kujiuliza kama kuna mgeni ambaye angetamba katika kikosi cha Yanga yenye Mohammed Hussein, Edibily Lunyamila, Salvatory Edward, Yusuph Macho, Sekolojo Chambua na wengineo. Isingewezekana.

Kitu cha msingi ni wenye dhamana kutimiza wajibu wao. Hatuzalishi wachezaji wenye ubora.

Mbona Simba haileti mchezaji katika nafasi ya Mohamed Hussein ‘ Tshabalala’? Ukiona hivyo katika nafasi hiyo tulizalisha mchezaji aliye bora.

Wenye dhamana wanaleta kisingizio kwa wageni, lakini ukweli, hatuzalishi wachezaji bora na hata hao wachache bora tuliozalisha nao wana uvivu fulani hivi kulinganisha na wachezaji wa kigeni. Kwa nini Ibrahim Ajibu anashindwa kucheza pale Simba mbele ya kina Francis Kahata? Siamini kama ni kwa sababu za kisoka.

Nimeambiwa ligi ina wachezaji 76 tu wa kigeni. Ni kweli wachezaji hawa wanaziba nafasi za wazawa? Tusiwe na uvivu wa kufikiria. Tuna matatizo ya msingi zaidi ya hili la wachezaji wa kigeni. Tunataka kutumia kama kisingizio tu, lakini mpaka sasa hawajaziba nafasi za maana za wageni.

Tunaweza kuwaondoa hata wote kama tunataka, lakini tutabakia na ligi isiyo na ushindani kutokana na kuwalinda wachezaji wetu wazawa wenye viwango vibovu.

Kupanga ni kuchagua. Hata Waingereza waliwahi kutaka kudanganyana hivi lakini wakaamua kuchagua kuwa na ligi yenye ushindani.

Leo Harry Kane anacheza katika kikosi cha kwanza cha Tottenham kwa sababu anastahili na sio ameondolewa upinzani wa wachezaji wa kigeni katika nafasi yake.

Kina Raheem Sterling wamepambana kupata nafasi licha ya kuwepo kwa wakali wengi wa nje katika kikosi chake.

Turudi katika tatizo la msingi. Tatizo liliacha kutengeneza kina Benard Morrison wake. Hatujui kwa nini.

Unapogundua Morrison asingepata nafasi mbele ya Lunyamila au Thomas Kipese hapo ndipo unapojua tatizo sio wachezaji wa kigeni.

Tatizo ni sisi wenyewe na wachezaji wetu wa kizawa.

Advertisement