JAMVI LA KISPOTI : Chama, Mnguto huu ni wakati sahihi kuachia ngazi

Thursday February 6 2020

Chama, Mnguto huu ni wakati sahihi kuachia ngazi, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Kuu Tanzania Bara, Chama cha Soka cha WaamuzI,

 

By Khatimu Naheka

Gumzo kubwa sasa ama tatizo kubwa linalozungumziwa na eoyote anayefuatilia Ligi Kuu Tanzania Bara na hata Ligi Daraja la Kwanza ni makosa ya wazi ya maamuzi katika mechi mbalimbali.

Kila unapopita katika maeneo mbalimbali ukikuta wanazungumzia soka, basi haitamalizika dakika moja kama hutasikia malalamiko ya waamuzi.

Hata ukikuta shabiki anashangilia timu yake imeshinda akimaliza furaha yake atawageukia waamuzi - kama sio kukubali walimbeba, basi atalalamika na lake - huu ndio umekuwa wimbo mzuri sasa kuimbwa.

Wimbo huu unazidi kushika kasi, makosa ya waamuzi yamekuwa ni mengi kuliko kupungua na kadri ya muda unavyosogea haionekani dalili ya kupungua na sasa yameongezeka.

Hilo si tatizo kubwa sana, lakini kinachosikitisha wakubwa wenye mamlaka ya mpira bado hawajaliona hilo kama tatizo. Wako katika usingizi mzito na hata ukiwaamsha na kuwauliza watakujibu jibu rahisi tu kwamba waamuzi nao ni binadamu wanafanya makosa, kisha baada ya jibu hilo watarudi kuvuta shuka na kuendelea kulala.

Ndiyo. Mpira wetu umefikia hapo nafikiri hatua muhimu sasa ni kusubiri kuona bingwa ambaye anatokana na makosa ya waamuzi katika mechi mbalimbali.

Advertisement

Nasema kauli hii kwa sababu sasa timu zimekuwa zikipata pointi tatu za ushindi kwa kutumia makosa ya wazi ya waamuzi wanaosimamia mechi na si timu kuonyesha uwezo wa kucheza kandanda safi na kisha ishinde.

Badala ya timu kupambana kutafuta pointi tatu, hali imekuwa kwamba timu inakuja uwanjani kusubiri makosa ya waamuzi ili wapate ushindi. Huu ni udhafu mkubwa.

Ajabu ni kwamba wapo watu ambao wanahusika kuwafanyia mchujo waamuzi hawa na hata kuwapitisha, lakini mpaka sasa wako kimya na hakuna anayethubutu kuwajibika.

Mpira wa nchi yetu unapitia wakati mgumu, lakini bado kuna mtu ataitwa mwenyekiti wa Chama cha Soka cha Waamuzi kisha ataitika.

Sioni kama kuna ulazima wa kuendelea kumuona mtu kama mzee wetu Athuman Chama akiendelea kuongoza jopo la waamuzi wakati huu ambao waamuzi wake wanaonekana wazi wameshindwa kufanya kazi ipasavyo.

Sio tu mzee Chama, lakini pia kwa matatizo yanayoendelea sioni kwa nini mzee wangu Steven Mnguto ambaye licha ya kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, pia anaiongoza Kamati ya Saa 72 ambayo nayo imeshindwa kuchukua maamuzi magumu dhidi ya waamuzi.

Namwamini sana Mzee Mnguto, lakini kwa hatua ambayo makosa haya yamefikia ni lazima alipaswa kuwajibika na si kusubiri kuandamwa kutokana na kazi ambayo klabu zilimwamini ameishindwa na badala yake sasa klabu zinaumia.

Nawamulika hawa wawili kutokana na nafasi zao hizo mbili - zote zimeshindwa kutoa mwarobaini au hata kupunguza maradhi ya waamuzi ambao wanaendelea kuzipa pointi tatu timu ambazo hazistahili.

Sasa hali imefikia hata timu ambayo imeshinda au kunufaika na makosa ya waamuzi wenyewe wanashangaa kwa nini wamependelewa kwa maamuzi ya namna hiyo.

Hali kama hii inapotokea kisha ukamsikia Mnguto akinukuliwa akisema tulisahau kuipangia timu moja kucheza mechi zake na akiishangaa hiyo timu hata kwa nini nao wao hawakuikumbusha Bodi, ni lazima utagundua kwamba kuna saratani mbaya inauangamiza mpira wetu.

Naona kuna watu wanaongoza ofisi ambazo hazipo katika kiwango chao ambao hawataweza kulivusha soka letu badala ya kuzidi kulididimiza.

Makosa kama haya yatawachefua zaidi wadhamini ambao wanatoa fedha nyingi kugharamia klabu na badala yake wanakuja kuona nembo zao zinachafuliwa kwa makusudi huku hakuna hatua zinazochukuliwa kwa waamuzi.

Hili ni anguko kubwa ambalo hakuna anayepaswa kuendelea kulichekea zaidi ya kuwa mkali, wakati huu tukisubiri kuona tunapata bingwa au timu kushuka daraja ambazo hazikustahili.

Mnguto na Chama wanapaswa kuelewa kwamba wanazidi kudidimiza soka kutokana na kwamba, tunaweza kuona timu fulani imefanikiwa kuchukua ubingwa, lakini itakapotoka nje ya mipaka na kukutana na mabingwa halisi waliopigana vita ngumu ndipo pale tunapopata aibu ya kupokea vipigo vikali.

Lakini kumbe matatizo hayo tumeyatengeneza ndani mwetu katika usimamizi mbovu wa ligi na badala yake adhabu yake itakuja katika ushindani tuwapo katika uwakilishi huko nje ya mipaka ya taifa letu.

Advertisement