TIMUA VUMBI : Aveva, Kaburu karibuni uraiani watu wa mpira

Thursday November 7 2019

 

By Mwanahiba Richard

NI siku 860 ambazo walitengana na familia zao, walitengana pia na familia ya soka ambayo kwa hakika waliipenda na waliitumikia kwa miaka mingi.

Evans Aveva na Geofrey Nyange ‘Kaburu’ ni miongoni mwa viongozi ambao waliitumikia Simba kwa miaka mingi tangu enzi na enzi nadhani ni kuanzia kipindi ambacho walijitambua kuwa wanapenda soka na timu wanayoipenda ni Simba SC.

Walipata kuwa viongozi wa klabu hiyo kwa nyakati tofauti hadi pale walipopatwa na matatizo ya kisheria ambapo Aveva alikuwa ni Rais huku Kaburu akiwa makamu wake.

Ni mengi waliyafanya wakiwa ndani ya Simba, ambayo kwa hakika pamoja na matatizo hayo yaliyowakuta inaaminika Wanasimba wanakumbuka nini walikifanya juu ya klabu yao, ingawa binadamu tuna kawaida ya kukumbuka mabaya zaidi kuliko mazuri ila Aveva na Kaburu walikuwa na mazuri mengi waliyoyafanya kwenye uongozi wao.

Walitengana na familia ya soka kwa tuhuma za utakatishaji pesa za usajili wa mshambuliaji Emmanuel Okwi raia wa Uganda aliposajiliwa na Etoile du Sahel ya Tunisia kiasi cha Dola 300,000 zaidi ya Sh 600 milioni.

Hivi karibuni Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwaondolea shitaka hilo la utakatishaji pesa na uhujumu uchumi makosa ambayo hayana dhamanana kubakiwa na kesi nyingine saba ambazo wanatakiwa kujibu ingawa hizo zina dhamana.

Advertisement

Juzi Jumanne, Aveva na Kaburu walipata dhamana ambapo sasa wapo nje kwa dhamana ya Sh 30 milioni kila mmoja wakisubiri kuendelea na kesi zao nyingine zinazowakabili.

Tangu wakiwa chini ya sheria wakisubiri hatima zao, kuna mambo mengi yamefanyika ndani ya timu yao pendwa ya Simba ambayo sasa wataanza kuyashuhudia na si kuyasikiliza kama ilivyokuwa hapo awali.

Tangu walipoondoka miaka miwili na zaidi timu yao ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo na sasa wanapambana ili kufikia rekodi ya Yanga ya kutwaa ubingwa huo mara tatu mfululizo.

Lakini, Simba iliweza kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita ambapo sasa ilitolewa hatua za awali kabisa hivyo imebaki kupambana kutetea ubingwa wake tu.

Simba ikiwa kwenye mchakato wa kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa klabu ambapo baada ya Aveva na Kaburu kushikiliwa na vyombo vya dola walifanikisha mchakato huo na sasa Simba haipo chini ya wanachama ni mali ya kampuni huku Mwekezaji, Mohamed Dewji ‘Mo Dewji’ ndiye aliyepita kwenye mchakato huo akiwa mwombaji pekee.

Simba sasa haina nafasi ya Rais kama ilivyokuwa wameiacha katiba yao, kuna mwenyekiti ingawa kwa kipindi walichokuwa nje ya familia hii alichaguliwa Swedy Mkwabi ambaye amejiuzulu nafasi hiyo akiwa hajamaliza hata mwaka mmoja madarakani.

Simba ya sasa inasimamiwa na Mkurugenzi Mtendaji, Senzo Mzingisa raia wa Afrika Kusini ambapo kipindi cha kina Aveva na Kaburu hakukuwa na mambo kama hayo, kwasababu ilikuwa ni klabu ya wanachama na sasa ni kampuni, hivyo kila kitu kinakwenda kisasa tu. Ule Uwanja wa Bunju waliouacha ukiwa unaelekea kutekelezwa sasa umejengwa viwanja viwili na tuliambiwa ungeanza kuutumia mwezi uliopita, Oktoba kwa ajili ya mazoezi ingawa hadi sasa bado.

Pia, wale wachezaji wa waliowasajili kina Aveva na Kaburu kama kina Okwi, Haruna Niyonzima, Emmanuel Mseja, Jamal Mwambeleko, Ally Shomary, Juma Liuzio, Salum Mbonde, Asante Kwasi, James Kotei, Nicholous Gyn, Shiza Kichuya, Mohamed Ibrahim, Paul Bukaba, Said Mohamed ‘Nduda’, Mwinyi Kazimoto wote hao hawapo kila mmoja ameenda kuangalia maisha sehemu nyingine.

Ila naamini ni furaha kubwa kwa Aveva na Kaburu kuendelea kuwoana wale nyota walioapigania kutoka Azam FC kama vile John Bocco, Shomary Kapombe, Aishi Manula na Erasto Nyoni wakiendelea kuwemo kundini. Mbali na hao kuna Yusuph Mlipili (Toto Africans), Mzamiru Yassin (Mtibwa Sugar).

Aveva na Kaburu bado wanawakuta vijana wao wapendwa ndani ya Simba Jonas Mkude, Said Ndemla pamoja na Ibrahim Ajibu ambaye amerudishwa kutokea Yanga, hao ni vijana waliolelewa Simba B. Yapo mengi ambayo Simba kwasasa wanajivunia yaliyofanywa kwa muda huu ambao Aveva na Kaburu walipokuwa nje ya familia ya soka, Simba ya sasa sio waliyoicha, ina mabadiliko makubwa sana.

Advertisement