JAMVI LA MWANASPOTI : Sio Mkwakwani tu, viwanja vingi havifai kutumika

Thursday April 18 2019

 

By Khatimu Naheka

Uliangalia ile mechi ya Coastal dhidi ya Simba jana Jumatano? Vipi macho yako yaliona kama yangu juu ya ubovu a sehemu ya kuchezea pale dimbani? Ndiyo, vile ndio viwanja vyetu ambavyo tunavitumia katika ligi ambayo tunahitaji wadhamini waje kuboresha soka letu.

Usiishie hapo utafute Uwanja wa Namfua pale Singida unakubali lig ichezwe kwenye uwanja kama huo? Usishangae hivyo ndiyo viwanja vilivyopitishwa kuchezewa ligi na viko vingi sana hapa kwetu.

Tumeshindwa kila kitu kuhusu soka na jinsi tunavyotakiwa kuliongoza hapa kwetu kila kitu ni ubabaishaji hakuna kitu kinachofanyika kwa weledi.

Hivi ndiyo viwanja ambavyo timu inapopoteza tena ikiwa na kocha wa kigeni kisha unaambiwa kazi ya kufundisha hawezi anatakiwa kuondoka tulete kocha mpya.

Hivi ndiyo viwanja ambavyo tunavitumia kupima ubora wa mchezaji kuwa huyu ni mchezaji sahihi kuzichezea klabu zetu na zipate mafanikio.

Klabu kubwa hapa nchini zinaleta kocha mpya alafu kabla ya kusaini mkataba anaonyeshwa uwanja wa Taifa na nyasi zake alafu anaenda kusaini akikubali kuwa ataipa mafanikio timu husika.

Advertisement

Bado hatujaanza kuishi soka linavyotaka kutokana na mambo ya kizamani bado yapo kwa kushindwa hata kusimamia kulea nyasio za uwanja ambao utatumika kuzipa timu mafanikio.

Ndiyo najua majibu yatakuwa mepesi kwamba wamiliki wa viwanja ni CCM ambao nao wamelala wakipambana na siasa zao huku wakivuna persa kupitia viwanja hivyo lakini hebu tujiulize wakati klabu inawasilisjha uwanja flani kuutumia kwenye ligi nani anapitisha na kubaliki hilo?

Hawaonikuwa viwanja hivyo havina ubora kabisa kuchezewa ligi?

Klabu zinaingiza fedha nyingi lakini fedha hizo zimekuwa haziendi kutumika katika kutunza viwanja hivyo na kuzipeleka katika matumizi mengine.

Hili sio la CCM tu kwa kuwa hata Mwenyekiti wao wa Taifa Rais John Pombe Magufuli ni juzi tu ametoka kuhoji juu ya matunzo ya viwanja hivyo kulingana na maingizo ya fedha zinapopatikana.

Uwanja ambao anatoka Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi na hata Rais wa TFF kuwa na sehemu ya kuchezea mbovu kiasi hiki hii ni ishara mbaya kwa maendeleo ya soka letu ni sawa na kulala na lundo la uchafu katika chumba chako.

TFF na hata bodi ya ligi inatakiwa kufika wakati kuzizuia klabu zinazochagua viwanja vibovu kutumia viwanja hivyo ili nao waweze kuwafuata wamiliki na kuwahamasisha juu ya kuboresha na kuvitunza viwanja.

Katika uwanja ambao hata danadana tatu za mpira kudunda sehemu moja na inashindikana alafu kuutumia kujua ubora wa mchezaji wa timu flani au kocha ni mashaka mazito ambayo lazima yaondolewe.

Kuchukua akocha wa kigeni tena kutoka Ulaya na kuwaleta nchini kisha kuwapima katika viwanja vya Mkwakwani na hata Namfua ni kuleta utani na kazi za watu na hata wao watatushangaa kwa aina ya akili zetu.

Yako mambo ambayo yanaendelea kuganda hapa kwetu lakini nchi nyingi zinakimbia na kuachana nayo wakati huku kwetu tukiaendelea kuishi nayo.

Kuna mambo sio ya kufumbia macho hasa tunapozungumzia maendeleo kwenye mchezo wa soka maana sio kuangalia tu timu zinacheza lakini hatuna mipango ya kufanya soka liwe endelevu na kuvutiwa wengine, ndio maana hata udhamini unakuwa mgumu kutokana na mazingira ambayo sio rafiki.

Advertisement