Wasanii waliogeukia biashara ikawatoa na kuwapoteza

KUMEKUWEPO na madongo mengi kwa wasanii ambao wamekuwa wakitegemea muziki katika kuendesha maisha yao ya kila siku na inapofika wamechuja kwenye soko hali zao huwa taabani.

Hii imeshuhudiwa hata kwa baadhi yao kushindwa kumudu gharama za matibabu na kujikuta wakitembezewa bakuli na wasanii wenzao kuomba msaada kwa jamii iweze kuwasaidia.

Kwa wale ambao hawataki aibu hiyo wamekuwa wakiugua kimyakimya ilimradi kulinda heshima zao na kutotaka kuonekana mbele ya macho ya watu kwamba wamefulia.

Pia, ni kutokana na kuchuja huko wengine wameshindwa kuhimili hali za kimaisha na kujikuta wanaingia katika matumizi ya dawa za kulevya kwa kinachodaiwa ni kujipa moyo kwamba wanapunguza msongo wa mawazo wakati ukweli ni kwamba wanajimaliza kiafya na kiakili, na baadhi yao kuishia magerezani.

Ni kutokana na hilo, hivi karibuni baadhi ya wasanii wamejiongeza na kuanzisha biashara mbalimbali na kutokana na majina ambayo tayari wanayo mitaani, na wapo ambao wamejikuta wakipiga pesa za maana tu.

Katika makala hii itawaorodhesha wachache waliochukua uamuzi huo na kujikuta wanatoboa, na pia itaeleza walioshia njiani.

Shilole

Jina lake halisi ni Zuwena Mohamed. Akiwa msanii aliyepata jina kupitia uigizaji filamu na baadaye kubadili gia na kuingia

katika muziki, aliamua kuanzisha biashara ya chakula.

Katika biashara yake hiyo aliyoianzisha kama masihara nyumbani kwake alipokuwa akitembelewa na wageni, alikuwa akiwapikia na wao wakiondoka kwenda kusimulia msosi wake ulivyo bomba.

Taratibu walimshauri kwa nini asiwe anapika na kuuza na kukubaliana na ushauti huo, ambapo anaeleza alianza na mtaji wa Sh50, 000 na kadri alivyozidi kupata wateja ndipo alipopata wazo la kufungua mgahawa na kuupa jina la Shishi Food, ambapo Shishi ni kifupi cha Shilole.

Biashara hiyo imejikuta ikimfungulia milango mbalimbali msanii huyo ambaye hivi karibuni amekuwa gumzo zaidi baada ya kutokea mgogoro katika ndoa yake na kujikuta analamba madili kibao ikiwemo ubalozi wa bidhaa mbalimbali.

Pia, amekuwa akialikwa katika makongamano mbalimbali ya kinamama ambako hutoa ushuhuda wa maisha aliyoyapitia hadi kufika kuwa na mgahawa huo, ambao awali ulikuwa eneo la Morocco na baadaye kauhamishia Kinondoni.

Shishi amekuwa shuhuda mzuri kwa kinamama kama moja ya njia ya kuwapa moyo wanawake ambao wameonyesha kukata tamaa ya maisha au kuwafanya wasonge mbele zaidi katika hatua ambazo baadhi yao wapo kwa sasa.

Hamisa Mobeto

Mwanamitindo Hamisa Mobeto kutokana na kipaji chake cha kuwa mwanamitindo alijikuta akiwavutia watu kutokana na nguo ambazo alikuwa anajishonea na kwenda nazo katika hafla mbalimbali.

Kuulizwa mara kwa mara nani fundi wake, kulimpa wazo la kwa nini asianzishe kampuni ya mavazi na hapo ndipo alipokuja na Mobeto Styles, ambapo amekuwa akiwashonea nguo watu mbalimbali wakiwemo mastaa wa nchini na nje ya nchi.

Mojawapo wa mastaa ambao ameshawashonea nguo ni pamoja na msanii Diamond Platnumz, nguo ambazo alivaa siku ya uzinduzi wa EP ya Zuchu uliofanyika Aprili, mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City.

Jaquiline Wolper

Msanii huyu aliyejizolea umaarufu kupitia fani ya filamu, ni moja ya mastaa wa kike wanaopenda kupendeza na kutaka kuonekana tofauti anapotokelezea mbele za macho ya watu.

Jambo hilo lilimsukuma na kufungua kampuni ya mavazi aliyoipa jina la Wolperstylish, ambayo awali ofisi zake zilikuwa eneo la Mkwajuni huko Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, mwaka jana aliamua kuhama eneo hilo na kwenda Tandale - uswahilini kuuza vijora - biashara ambayo anasema imekuwa ikimlipa zaidi kuliko alivyokuwa Mkwajuni na pia amefungua duka la vitenge eneo la Sinza.

Aunt Ezekiel

Aunt Ezekiel ambaye mbali ya kufanya biashara ya pochi eneo la Kariakoo, pia amefungua baa aliyoipa jina la Lux. Baa hiyo iliyopo eneo la Kijitonyama imekuwa ikiwakarimu mastaa mbalimbali kwenye shughuli zao za sanaa na pia ni hivi karibuni ilikuwa moja ya wadhamini wa shughuli ya msanii Kusah aliyoipa jina la ‘Private affair with Kusah’.

Jux

Alianzia kwenye uanamitindo na baadaye kujikita kwenye muziki. Alianzisha kampuni yake ya mavazi aliyoipa jina la African Boy.

Kampuni hiyo inatengeneza mavazi ya aina mbalimbali zikiwemo fulana, viatu, kofia na kava za simu.

Nandy

Huyu ni mmoja wa wasanii wa kike wanaofanya vizuri kwenye muziki wa Bongo fleva tangu alipoachia kibao chake cha Nagusagusa miaka miaka minne iliyopita.

Julai, mwaka huu, msanii huyo anayejiita African Princess alifungua duka la nguo za harusi alilolipa jina la Nandy Bridal lililopo eneo la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.

Malkia Karen

Huyu ni mtoto wa mtangazaji maarufu wa redio, Gardiner G Habash. Licha ya kuwa na muda mfupi tangu aingie kwenye soko la muziki, hivi sasa amekuwa mjasiriamali wa juisi ya miwa aliyoipa jina la Malkia Caneblast na ameshafungua vieneo kibao vya kuuzia juisi hiyo.

Pia amekuwa akitoa huduma ya kuwapelekea watu juisi hiyo majumbani mwao.

Rose Ndauka

Ni mmoja wa wasanii wa mwanzo waliopata majina kupitia filamu, huku filamu ya kwanza kumtambulisha vyema katika soko hilo ikiwa ni Swahiba aliyocheza sambamba na wasanii Rich Rich na Jacob Steven.

Mbali ya kuigiza, Rose anamiliki saluni ya kike na ya kiume iliyopo eneo ya Sinza, Afrika Sana.

Wakati hao tuliowataja biashara zao zikiwa bado zinaendelea, baadhi wameonekana kupotea akiwemo mrembo wa zamani wa Tanzania, Wema Sepetu ambaye mwaka 2017 alitambulisha lipstick yake ya ‘Kiss by Wema’.

Mpaka sasa bado haijajulikana hasa sababu ya kutoendelea na biashara hiyo japokuwa huko nyuma ziliwahi kuzuka tetesi kwamba hazikuthibitishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa Tanzania. Hata hivyo, hakuwahi kulizungumzia hili.

Diamond Platnumz

Huyu ni kama kachangulia upande wa biashara - anakubalika sana, kwani mpaka sasa mbali ya kumiliki lebo ya Wasafi, pia anamiliki kituo cha redio na televisheni za Wasafi.

Pia ni hivi karibuni alionyesha hoteli yake ambayo bado haijajulikana lini itaanza kazi.

Hata hivyo, moja ya bidhaa ya msanii huyo iliyoadimika sokoni ni pafyumu ya Chibu aliyoitambulisha mwishoni mwa mwaka 2017.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo katika moja ya mikutano ya waandishi wa habari, Diamond alisema kulitokea makosa katika utengenezaji wake na kwamba ilikuwa inafanyiwa marekebisho kabla ya kurudishwa tena sokoni.

Ali Kiba

Ni mmoja wa wasanii wakubwa wa muziki wa kizazi kipya. Mbali ya kumiliki lebo ya Kings Music ambayo mpaka sasa ina wasanii wanne akiwemo yeye, mwaka juzi alitambulisha kinywaji chake cha ‘Mo Fire’.

Kinywaji hicho alikitambusha rasmi siku ya sherehe ya ndoa yake iliyofanyika Hoteli ya Serena.

Hata hivyo, kinywaji hicho kilionekana maeneo machache jijini Dar es Salaam na baada ya hapo ikawa kimya.

Siku alipoulizwa na wandishi kuhusu suala hilo, alisema walisimama kwa muda kutokana na sababu ambazo hakuwahi kuzitaja na kuahidi kuwa kitarudi muda si mrefu, lakini mpaka sasa kimya.

Wasanii wengine wenye biashara ni Irene Paul anayeuza mafuta ya nywele asili, Shamsa Ford anauza

vijora, MwanaFA mwenye pafyumu ya fyN, Whozu ana duka la nguo na Vanessa Mdee aliyetangaza kuacha muziki siku za karibuni alikuwa na bidhaa ya viatu vyake vya shule.

Ukiangalia bishara walizonazo wasanii hao ni wazi kuwa iwapo watazisimamia vyema, hata muziki au filamu vikija kuwatupa mkono wataweza kuishi maisha mazuri na pengine kutimiza hata ndoto za maisha yako kupitia shughuli hizo.