Wamekimbiza, wana wafuasi wengi hadi raha

MCHEZAJI Cristiano Ronaldo ndiye binadamu mwenye wafuasi (followers) wengi zaidi duniani kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram akiwa nao milioni 239, akifuatiwa na mwimbaji Selena Gomez mwenye watu milioni 194. Pia Ronaldo anaongoza upande wa Facebook akiwa na watu milioni 123, akifuatiwa na mwimbaji Shakira mwenye wafuasi milioni 99.

Upande wa Twitter, Justin Bieber ndiye mwimbaji anayeongoza akiwa na watu milioni 112, akifuatiwa na mwimbaji Katy Perry mwenye watu milioni 108, hata hivyo wanatanguliwa na aliyekuwa Rais wa 44 wa Marekani, Barack Obama mwenye wafuasi milioni 123.

Lebo ya T-Series kutoka nchini India inayojihusisha na uandaaji wa muziki na filamu ndio inaongoza duniani kote kuwa na wafuatiliaji (subscribers) wengi kwenye mtandaoni wa YouTube ikiwa nao milioni 156. Mchekeshaji PewDiePie kutokea Sweden ndiye anayefuata akiwa na wafuatiliaji milioni 107.

Ni wazi wanamichezo, wanamuziki na waigizaji wamekuwa na nguvu kubwa ya ushawishi katika mitandao ya kijamii duniani kote kitu kinachosababisha kujizolea wafuasi lukuki.

Je, hapa Tanzania hali ipo vipi? Makala haya yanaangazia mastaa 10 Bongo kutoka kwenye filamu, muziki, michezo, urembo na media wenye wafuasi wengi kwenye mitandao hiyo (Instagram, Facebook, Twitter na YouTube).

Karibu.

1. Diamond Platnumz -

Mil. 10.8

Mwimbaji huyu pendwa wa WCB ndiye anaongoza Tanzania na Afrika Mashariki kufuatiliwa na watu wengi zaidi kwenye mitandao ya Instagram na YouTube.

Diamond anafuatiliwa na watu milioni 10.8 Instagram, Facebook milioni 2.9, Twitter 959,000 na YouTube milioni 4.2.

2. Millard Ayo - Mil. 8.2

Mtangazaji huyu wa Clouds FM ndiye binadamu pekee kutokea Tanzania kuwa na wafuasi zaidi ya milioni 1 kwenye mitandao yote minne. Hivi majuzi alitambulika na YouTube kama mwanahabari wa kwanza Afrika kwa video zake kwenye mtandao huo kutazamwa (views) zaidi ya mara bilioni 1.

Millard ana watu milioni 8.2 wanaomfutilia Instagram, Facebook watu milioni 2.5, Twitter milioni 1.1 na YouTube milioni 3.

3. Wema Sepetu - Mil. 7.8

Mrembo huyo aliyenyakuwa taji la Miss Tanzania mwaka 2006 ndiye mwanamke anayeongoza Tanzania kuwa watu wengi zaidi kwenye ukurasa wake wa Instagram, ila kwa ukanda wa Afrika Mashariki anazidiwa na Zari The Bosslady mwenye watu milioni 8.3.

Wema ana watu milioni 7.8, Facebook watu 643,000 Twitter watu 464,000 na YouTube watu 177,000.

4. Harmonize - Mil. 6.2

Mwimbaji huyo wa Konde Music Worldwide alikuwa na nafasi ya kuwa juu zaidi kama angeongeza ubunifu wa kimaudhui katika mitandao ya Twitter na Facebook, jina lake ni kubwa zaidi ukilinganisha namba alizonazo kwenye mitandao hiyo.

Konde Boy ana watu Milioni 6.2 Instagram, Facebook watu 379,000, Twitter watu 101,000 na YouTube watu Milioni 2.

5. Rayvanny - Mil. 5.2

Huyu naye alikuwa na fursa ya kupaa zaidi kama angeutumia vema mtandao wa Twitter, uzito wa jina lake na muziki wake haulingani namba alizonazo kwenye mtandao huo.

Ray ana watu Milioni 5.2 Instagram, Facebook watu 529,000, Twitter watu 94,000 na YouTube watu Milioni 2.

6. Vanessa Mdee - Mil. 6.8

Mwimbaji huyu aliyetangaza kuachana kabisa na muziki wa Bongo Fleva, ameikuza chapa yake sana hasa mtandaoni, hajaishia kwenye kurasa za mitandao ya kijamii bali ana hadi tovuti kwa ajili kumuelezea zaidi yeye na kazi zake.

Cash Madame ana watu milioni 6.8 Instagram, Facebook watu 233, 000, Twitter watu 392,000 na YouTube watu 258,000.

7. Alikiba - Mil. 5.9

Huyu ni staa ambaye daima analinganishwa na Diamond Platnumz kwa kila jambo, ikiwamo wafuasi. Lakini Kiba si mtu wa kujitangaza sana, ndio maana amezidiwa kwenye wafuasi wa mitandaoni huku pia akiwa chini kutokana na kutoitumia YouTube channel yake ya awali yenye jina lake na kuanzisha nyingine inayotumia jina la Kings Music Records.

King Kiba ana wafuasi milioni 5.9 Instagram, Facebok watu 465,000, Twitter watu 543,000 na YouTube watu 699,000.

8. Idris Sultan - Mil. 5.9

Kabla ya kuanza uchekeshaji, Idris alikuwa maarufu zaidi mtandaoni baada ya kushinda Big Brother Africa Hotshots 2014 na kujinyakulia kitita cha Sh. 514 milioni.

Kwa sasa, host huyo wa shoo ya kusaka vipaji vya kuimba ya Bongo Star Search (BSS) msimu wa 11, ana wafuasi milioni 5.9 Instagram, Facebook watu 335,000, Twitter watu 636,000 na YouTube watu 92,000.

9. Lady Jaydee - Mil. 4.8

Mwimbaji huyo ndiye msanii wa kike Tanzania katika filamu na muziki kuwa na watu wengi zaidi kwenye mtandao wa Facebook, mwaka 2014 alikuwa msanii wa kwanza nchini kufikisha watu 300,000 kwenye mtandao huo.

Jide ana watu milioni 4.8 Instagram, Facebook watu 849,000, Twitter watu 609,000 na YouTube watu 71,000.

10. Masanja Mkandamizaji - Mil. 4.6

Pia Masanja na Lady Jaydee amefungana kwa upande wa wastani, ila Masanja amedondokea kwenye nafasi hii kutokana YouTube channel kuwa na matumizi mengine nje ya sanaa, hivyo ana nafasi kubwa ya kuongeza watu.

Msanja aliyebamba na kundi la Orijino Komedi, kwa sasa Instagram ana watu Milioni 4.6, Facebook watu 746,000, Twitter watu 729,000 na YouTube watu 133,000.

Muhimu: Kuna Mastaa kama Jacqueline Wolper, Linah, Zamaradi Mketema, Elizabeth Michael Lulu n.k wanaonekana kuwa na wafuatialiji wengi Instagram kuliko hata baadhi ya niliyowaweka kwenye chati hii lakini wameshindwa kuingia kutokana na kutokuwepo au kutotumia moja ya ile mitandao hiyo minne niliyoitaja hapo awali.

Pia namba za wanaowafuatilia mastaa hawa zinaongezeka kila muda, hata hivyo haiwezi kuathiri mtiririko mzima kwa kiasi kikubwa.