VIDEO: Wema Sepetu aomba radhi kwa ‘video zake chafu’

Thursday October 25 2018Mwigizaji Wema Sepetu

Mwigizaji Wema Sepetu 

By Rhobi Chacha

Mwigizaji Wema Sepetu, leo Oktoba 25 ameomba radhi akisema video na picha zake chafu zilizoenea mtandaoni zimesababisha usumbufu kwa mamlaka za Serikali na Watanzania kwa ujumla.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika nyumbani kwa mama yake, Sinza jijini Dar es Salaam, Miss Tanzania huyo wa mwaka 2006 amesema kuenea kwa picha na video hizo kumetokana na utoto.

Wema aliyeonekana kuwa mtulivu amesema: “Kuenea kwa picha hizo kumetokana na upumbavu na utoto wangu, ninawaahidi Watanzania kuwa hilo halitatokea tena naomba radhi kwenu wote.”

Huku akisoma maelezo hayo yaliyoandikwa katika karatasi mbili, Wema alisema hakuna mwingine wa kulaumiwa kwa kuenea kwa picha na video hizo lakini anaomba asamehewe kwa kitendo hicho.

Pembeni akiwa amesimamiwa na meneja wake, Martin Kadinda na rafiki yake Petit man, Wema alisoma karatasi hizo huku akionekana mwenye  huzuni na alipomaliza alisimama na kuondoka eneo hilo akiwaacha waandishi wa habari wakiwa na kiu ya kuuliza maswali zaidi.

Moja ya swali kuu kutoka kwa waandishi lilikuwa kufahamu ni nani aliyevujisha video na picha hizo katika mitandao ya kijamii.

Wema ni kama alilijibu swali hilo  katika maelezo yake aliposema, hamlaumu yeyote kwa kuvunja kwa picha hizo kwa kuwa ujinga wake ulisababisha zikawepo.

Advertisement