Tshishimbi: Hili ndio tatizo la Eymael

Thursday July 30 2020

 

By Papy Tshishimbi

YANGA tumemaliza msimu kwa kumfukuza kocha wetu Luc Eymael ambaye alijikuta anapoteza kibarua chake saa chache baada ya kuiongoza timu kushika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Awali, nimshukuru Eymael kwa muda ambao nimefanya naye kazi hapa Yanga. Alikuja na matarajio yake kama ambavyo mwajiriwa yeyote ndani ya timu angekuwa na malengo, lakini kikubwa nayaona malengo ya timu kutangulizwa mbele ambayo ndio chanzo cha ajira zetu sote.

Kinachonisikitisha ni jinsi Eymael ameondoka hata kama angekuwa amefanya makubwa kiasi gani, lakini hatua ambayo imesababisha kuondolewa kwake haileti picha nzuri kwake kwa heshima ya kazi yake na hata huko atakakokwenda.

Hili ni somo lingine ambalo binadamu yeyote anapaswa kujifunza jinsi anavyotakiwa kuyafanyia kazi yale anayoyaona kama changamoto katika kazi yake.

Zipo njia ambazo Eymael angeweza kuzitumia katika kufikisha ujumbe ambao ulikuwa unamsumbua, lakini kwa sasa ni vigumu kumpa nafasi tena ya kuelezea kile alichotaka kukisema, kwa kuwa jamii imeshachukua hatua na kuchukizwa na kauli zake na hapo ndipo baraka za maamuzi haya ya klabu zinapokuja.

Leo acha nieleze kwa kifupi jinsi gani niliishi na Eymael ambaye alinikabidhi unahodha wangu kwenye timu na hatua ambayo imechukuliwa kwake.

Advertisement

Nakumbuka wakati fulani Eymael akiwa bado ni kocha mpya wa Yanga, niliwahi kumuonya juu ya jinsi ya kuchukua hatua katika yale ambayo anataka kuyatafutia ufumbuzi.

Siyo kwamba alikuwa ni kocha mwenye ukali katika mazingira ambayo hayakuhitaji kwake kuwa mkali.

Kumuonya kwangu kulikuwa na maana kwamba anatakiwa kujitofautisha na anapofanya kazi sehemu kama Tanzania, kuna nidhamu ya kufikisha kile unachotaka kukizungumza na kikubwa kocha inawezekana alifanya kazi na wachezaji wenye weledi ambao hawakuwa wanahitaji kuzungumza mara mbili lile analotaka lifanyiwe kazi.

Hapa ilikuwa tofauti hata kwa wachezaji. Alihitaji kuzungumza zaidi ili kuweza kueleweka katika kile anachotaka mtu abadilike, naona hakuelewa kipi ambacho namuonya nacho.

Binafsi sikuwahi kumuona kama ni kocha ambaye anaweza kuwa mkali katika mazingira ambayo hakuhitajika, lakini maamuzi yake ya wakati gani na wapi apeleke malalamiko yake na pia uvumilivu wake ulitakiwa uwaje hapo ndipo kulikuwa na changamoto.

Ukiangalia hatua yake ya kupoteza kazi naona kabisa kukosa kwake mafanikio kunaweza kukawa sababu kubwa ambayo ilizidi kupeleka msukumo wa kuondolewa kwake.

Katika timu yake haina kitu ambacho watu wangeweza kukitumia kama njia ya kuhitaji kumpa nafasi zaidi kila taji alilikosa ndani ya miezi sita ambayo alifanya kazi. Nikiangalia tangu ugonjwa wa Covid- 19 ulipoingia uliondoa utulivu mkubwa ambao ungemsaidia.

Hatua nyingine mbaya zaidi ni pale alipopoteza vibaya mbele ya Simba (kwa kufungwa 4-1).

Eymael alikuwa na changamoto katika uamuzi wake kuelekea mchezo ule na matokeo ya timu kupoteza vibaya kwa mabao 4-1 yalifuta hata ushindi wake wa kwanza dhidi ya wapinzani wetu.

Makocha wengine wanaokuja nyuma yake yapo ya kujifunza katika michezo kama hii hapa Yanga.

Muhimu sasa ni kuona kama klabu yapi ambayo tunaweza kujifunza na kuyachukua kama njia ya kujisahihisha baada ya kuondoka kwa Eymael na yale ambayo aliyasema katika ujumbe wake kama yapo ambayo yataonekana yanatakiwa kufanyiwa kazi katika changamoto ambazo alizitoa kwa klabu.

Ni muhimu kila ambalo linawezekana kufanyiwa kazi ni vyema likafanyiwa, ili msimu ujao na hata wanaokuja wasiwe katika hali ambayo wale wanaotoka walikumbana nayo na kuwakwamisha.

Yanga inahitaji mafanikio, hili halipingiki, lakini katika kupatikana mafanikio hayo ni lazima mazingira yawe safi ili mtu akose sababu ya kipi kinamkwamisha, tukijaribu kujifanyia tathmini sisi na wapinzani wetu tuko kwenye afya gani ya kupambana na wenzetu ambao nao wanajipanga kufanyia kazi upungufu wetu.

Mwisho nimwambie Eymael kwaheri. Mpira ni mchezo unaokutanisha watu mbalimbali na huenda tukakutana tena.

Muhimu ni kujifunza ulipoanguka sasa ili kesho huko uendako usikutane na utelezi uliokuangusha.

Daima Yanga itaendelea kuwapo tu wengi tunapita kama ulivyopita wewe.

Kila la heri kocha.

Advertisement