Stima mapenzi kama yote kwa Jasmini

Muktasari:

Wanafurahia miaka 13 ya ndoa yao tangu walipokutana 2006, Jasmini anasema alimkubali na kumpenda Stima na kazi yake, hivyo amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha anafanya kwenye bora.

MWANAUME akipata mwanamke mwelewa basi inakuwa rahisi kwake kuwajibika bila ‘stress’ ndivyo ilivyo kwa kiungo fundi wa JKT Tanzania, Jabiri Aziz ‘Stima’ kapata mrembo anayemuelewa na kumuunga mkono katika kazi yake ya soka.

Jasmini Ismail Mkupe ni mke wa Stima, wamejaliwa kupata watoto watatu wa kwanza wa kike anaitwa Njama (9) na mapacha kurwa ni Nadir, doto Nizar (5).

Anasimulia safari yao ya mapenzi yaliyoanza 2006 kwamba, nyumba yao ilikuwa jirani na kina Stima huku Magomeni jijini Dar es Salaam, hivyo walikuwa wanakutana kupiga stori mbili tatu zilizowazamisha kwenye penzi zito.

Anasema baada ya kuzoena walijikuta hakuna anayetaka kukaa mbali na mwenzake na muda wote wakawa wanapenda kukaa pamoja.

Wanafurahia miaka 13 ya ndoa yao tangu walipokutana 2006, Jasmini anasema alimkubali na kumpenda Stima na kazi yake, hivyo amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha anafanya kwenye bora.

“Nashindwa kusema ilikuwaje mpaka tukajikuta tunatengeneza mahusiano, kifupi sisi ni watu ambao, tunapendana kupita kiasi ndio maana mpaka leo tunaishi kwa furaha kama ndio tunaanza kutongozana leo,” anasema.

RATIBA YAKE NYUMBANI

Jasmini anasema mume wake anapokuwa mapumziko anasimamia ratiba yake ya mazoezi ni kuhakikisha hajibweteki na akirejea kwenye timu sio mzigo kwa kocha.

“Nafahamu kazi yake inakuwa ina miiko gani, asubuhi anakuwa anakwenda kufanya mazoezi Uwanja wa Makurumla uliopo Magomeni, jioni anaingia gmy nikiwa na muda namsimamia,” anasema.

Mbali na hilo anasema anajitahidi kuangalia mechi zake kupitia luninga kuona kiwango chake ili kikiwa chini anakuwa anamsaidia namna ya kukipandisha.

“Soka ndilo linafanya atutunze familia yake, siwezi kufanya mizaha na hilo, uzuri ni mwelewa na hapendi timu anayokuwepo ifanye vibaya.

“Timu ikifanya vibaya stresi zake zinahamia nyumbani kunakuwa hakuna furaha ndio maana naepuka vitu vya kumfanya acheze chini ya kiwango ili muda wote tuwe na shangwe,” anasema.

KITU KILICHOWAHI

KUMUUMIZA

Jasmini anasema hakumbuki Taifa Stars walicheza na timu gani ya nje kocha akiwa Mbrazil Marcio Marcel Maximo, anasema alikwenda uwanjani kumuunga mkono mume wake alikutana na kisanga kilichofanya moyo wake uvuje hasira.

Anasema huwa wanapewa tiketi za VIP lakini yeye akaamua kwenda kujichanganya na mashabiki ambapo, akakutana na dada mmoja ambaye Stima alikuwa akishika mpira anasema usiniumizie.

“Mara ya kwanza niliposikia usiniumizie nikajua ni kawaida tu labda anamfurahisha anavyocheza, nikasha-ngaa anaendelee anasema usiniumizie Stima wangu, roho iliniuma sikuwa na la kufanya zaidi ya kumsubiri amalize nirudi naye nyumbani.

“Sasa akawa ananiuliza mke wangu mbona leo huniambii kama nifanya hovyo ama vizuri na nakuona kama umekosa furaha, ndipo nikamwambia, alicheka sana maana mume wangu si mtu wa kununa nuna kaniambia utachukia mara ngapi na mambo ya mashabiki.

“Kanipa moyo kwamba tumeishi miaka mingapi usinijue nilivyo, nikajikuta naishiwa pozi na ghafla hasira zikaondoka kisha akaniambia ya uwanjani yabaki huko huko na tukiwa nyumbani ni mambo ya familia,” anasema.