Shamsa : Kapama wali kuku tu hasira kwisha aisee!

Saturday November 23 2019

Shamsa -Kapama -wali -kuku -hasira -mshambuliaji - Kagera Sugar-michezo blog-mwanasport-MwanaspotiSoka-timu-Kagera Sugar-

 

By Charity James

SHAMSA Nassoro ni mke halali wa mshambuliaji wa Kagera Sugar, Nasoro Kapama. Unaambiwa usimuone nyota huyo anapambana kufanya vizuri kwenye timu hiyo mkewe kafunguka kuwa yeye ndiye ‘alamu’ yake kwenye kila kitu kuhusiana na soka.

Kila mjanja ana mjanja wake, hivyo ndivyo unavyoweza kusema kwani Shamsa amefunguka kuwa kila jambo linalomhusu mumewe kuhusu soka, yeye ndiye amekuwa akipambana kuhakikisha linafanyika kwa wakati na vizuri. “Mimi kama mke nina msaada mkubwa sana kwake, kwani naweza kusema ndiye ‘alamu’ yake, kwa kila kitu nimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha anaamka kwa wakati kwenda mazoezini, kula, kumuomba Mungu kabla na baada ya mchezo ili aweze kufikia mafanikio,” anasema.

“Najivunia kwenye hilo na nimekuwa nikimpa nguvu, hata yeye anaamini kuwa nipo pamoja naye katika hali zote za shida na raha, amekuwa akipambana kuniridhisha ninayepambana kumuamusha na kumtakia mema kwenye kila kitu.”

NI MUME BORA

Kapama anafahamika kutokana na kutupia mipira kambani kutokana na nafasi anayoicheza, ambapo ameweza kujizolea umaarufu kupitia hilo, basi unaambiwa akiwa nyumbani mambo yake kwa mkewe ni tofauti na anavyochukuliwa.

“Mume wangu pamoja na kuonyesha ufundi uwanjani kwa ari ya juu, basi uchovu wake unaishia hukohuko, akiwa hapa majukumu yake ya kifamilia anatimiza kwa wakati bila ya visingizio,” anasema.

Advertisement

“Kila kinachofanywa na mwanaume aliyeingia katika majukumu ya ndoa huwa anakitimiza, hivyo anastahili kuitwa mume bora kwangu.”

WALI, KUKU HASIRA KWISHWA

Kila mwanamke aliye ndani ya ndoa ana staili yake ya kumtuliza mume wake pale anapokuwa katika wakati mbaya na hasira.

Kuna wanaowabembeleza waume zao kwa mahaba na wengine kwa kuwapa muda wa mapumziko ili wakiamka warudi kwenye ari zao za kawaida.

Basi unaambiwa Shamsa ameshamjulia mumewe akimuona tu amekasirika jikoni hakuzimiki moto, anawasha jiko na kuanza kumpikia vyakula anavyovipenda na kumuandalia ili aweze kurudi kwenye ari yake ya kawaida na amekuwa akifanikiwa kwenye hilo.

“Kapama ni mtu wa hasira sana akiwa kwenye hali hiyo, basi naandaa mchele, maharage na kuku, najua nikipika hivyo tu anarudi kwenye furaha yake ya kawaida na kusahau kabisa kilichotokea,” anasema.

JIKONI KAMA KAWA

Wanaume wengi wamekuwa wakiamini kuwa majukumu ya akina mama ni kupika na kufua ikiwa ni sambamba na majukumu mengine mengi ya nyumbani huku wanaume wakijiweka pembeni kuwa ni watu wa kupambana kusaka fedha.

Kwa Kapama hilo ni tofauti kwani mkewe Shamsa anathibitisha kuwa huwa hana ubaguzi kwenye majukumu, kila anachokiweza amekuwa akikifanya ikiwa ni kumpunguzia majukumu mke wake anapotaka kupumzika.

“Nafurahia ndoa yangu, mume wangu ni rafiki yangu, tunasaidiana majukumu mengi, hata mimi nimekuwa nikimsaidia kumfulia vifaa vyake vya kazi kama jezi, soksi na viatu, basi unaambiwa na yeye hataki kukubali akiwa na nafasi haoni shida kuingia jikoni ananisaidia kupika.”

Advertisement