Seth Bosco amefariki dunia siku, saa aliyofariki Kanumba

Saturday December 7 2019

Seth Bosco -amefariki dunia -siku- saa -aliyofariki-Kanumba-Flora -Mutogoa-nyota wa filamu - Tanzania

 

By Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Flora Mutogoa ambaye ni mama wa aliyekuwa nyota wa filamu nchini Tanzania marehemu Steven Kanumba amesema Seth Bosco amefariki siku na saa aliyofariki kaka yake.

Flora ameyasema hayo leo Jumamosi Desemba 7, 2019 nyumbani kwake Kimara Temboni jijini Dar es Salaam nchini Tanzania alipokuwa akizungumzia kifo cha Bosco kilichotokea usiku wa kuamkia leo.

Amesema anasikitika kuwapoteza watoto wake hao wakiwa na umri mdogo ambapo Kanumba alifariki Aprili 6, 2019 akiwa na miaka 28 na Bosco amekutwa na mauti akiwa na miaka 32.

"Watoto hawa niliowalea mwenyewe wamefariki saa zinazofanana kwani hata Kanumba alifariki saa sita usiku wa kuamkia Jumamosi.”

"Hii inaonyesha namna gani undugu wao ulikuwa wa kushibana na wa kweli," amesema mama Kanumba.

Kutokana na msiba huo amewaomba wasanii na wadau mbalimbali kumshika mkono kama walivyofanywa wakati wa msiba wa Kanumba.

Advertisement

“Ukizingatia kuwa  Bosco ni msanii mwenzao na mtoto wao hivyo ni vema wakamsindikiza katika safari yake hii ya mwisho,” amesema

Pia, amebainisha kuwa angetamani kumsafirisha mtoto wake huyo kwenda kuzikiwa Bukoba mkoani Kagera ambapo ndio nyumbani kwao na  kwa mujibu wa mila zao zinataka hivyo, lakini kutokana na kutokuwa na uwezo mpaka sasa hivi hajajua atamzika wapi.

Advertisement