Rashid staa wa mbao aliyenasa mke msikitini

Muktasari:

Achana na pasi zake za maudhi anazozipiga akiwa na timu yake ya Mbao FC, kiungo huyo anabainisha kuwa dini inaweza ikawa sababu ya yeye kumpata mwanamke huyo kiurahisi kwani ni mwanamke aliyetoka katika familia ya dini hivyo ingekuwa kazi kwake kumpata kama asingekuwa anaswali.

MAPENZI buana daah! Wakati wanandoa wengi wakifunguka kuwa walikutana shuleni, mitandaoni na wengine kazini, basi unaambiwa kiungo wa Mbao FC, Rajabu Rashid ameeleza kuwa ndoa yake ina baraka na anaamini itadumu kutokana na kukutana na mkewe Pilly Abdallah msikitini.

Hadi ukaona mwanamke au mwanaume ameingia kwenye ndoa sio jambo rahisi kama wengi wanavyochukulia lakini kwa upande wa Rajabu anabainisha kuwa tangu alipomuona mwanamke huyo muda wa kutoka msikitini, haikumpa muda hadi kumpata kwani alitumia wiki mbili tu hadi kupata mawasiliano na kuingia kwenye uhusiano.

Achana na pasi zake za maudhi anazozipiga akiwa na timu yake ya Mbao FC, kiungo huyo anabainisha kuwa dini inaweza ikawa sababu ya yeye kumpata mwanamke huyo kiurahisi kwani ni mwanamke aliyetoka katika familia ya dini hivyo ingekuwa kazi kwake kumpata kama asingekuwa anaswali.

KAMBI HAIMNYIMI USINGIZI

Kwenye maisha ya ndoa hakuna kitu kinampa mwanaume au mwanamke furaha hasa anapokuwakaribu na mke/mume karibu na kuishi pamoja kwa kushirikiana katika kila jambo basi unaambiwa kwa kiungo wa Mbao yeye umbali na mkewe hasa akiwa kambini wala haumpi shida.

“Pilly ni wa kwangu. Ni kweli muda mwingi nakuwa kambini lakini hilo halinipi shida kwani ni mali yangu na mimi nipo kazini kutafuta hivyo nikirudi namkuta na nakaa naye wakati wote,” anasema.

“Suala la mimi kuwa kambini haliwezi kuwa kikwazo nimeoa natambua kuna kukaa kambini hata wanaofanya majukumu mengine mbali na soka siamini kama muda wote wanashinda na wake zao ni lazima wanatoka na kwenda kwenye majukumu yao kama kawaida hivyo hilo halininyimi usingizi na mke wangu anatambua majukumu yangu huwa ananivumilia na kunisubiri,” anasema.

MLINZI WA NDOA

Wachezaji wengi walio katika ndo ni muda mchache sana wanautumia kukaa na wake zao kutokana na majukumu yao ya kuwa na safari nyingi kwenda kucheza soka mikoani na hata wakiwa katika mikoa yao basi wanaingia kambini basi unaambiwa huwa wanapata shida sana hivyo njia kubwa wanayoitumia ili kujenga ukaribu na wake zao ni simu.

“Nampenda sana mke wangu na nina wivu naye hadi najikuta nakosa uaminifu kwake hivyo nikiwa mbali naye basi huwa namsisitiza sana kuwa karibu na simu kwani kila ninapopata wakati wa kuishika kitu cha kwanza kukifanya ni kumpigia. mawasiliano hayajawahi kukauka,” anasema.

“Akitaka kunikwaza nisimpate hewani au nimpigie asipokee basi ajiandae kunipa maelezo ambayo naweza nikayaelewa, napenda kuwasaliana naye sana na yeye mwenyewe analitambua hilo hivyo simu inaweza ikawa na siri kubwa ya ndoa yangu na mke wangu,” anasema.

KUFUA KULIFANYA AOE

Wachezaji hasa wasiokuwa katika ndoa wana shida kubwa sana zinazowasumbua kulingana na majukumu yao, unaambiwa wanapika wenyewe, kufua kuweka nyumba katika mazingira ya usafi hapo bado wanadaiwa mazoezi. Hayo yalikuwa yakimnyima raha Rajabu na ndipo alipochukua uamuzi wa kuingia kwenye ndoa.

“Hakuna kitu nafurahia sasa kama kupunguziwa majukumu na mke wangu ambaye nimedumu naye sasa mwaka mmoja na miezi nane, amekuwa akinisaidia vitu vingi sana ukiachana na ushauri wake wa kuona mimi nakuwa mpambanaji uwanjani amekuwa akinifulia, kupika vitu hivyo vilikuwa vinanikwaza,” anasema.

“Wachezaji wengi wanaamini ndoa inashusha viwango hilo napingana nalo na linawapotosha na kujikuta wanachelewa kuoa. Ukitaka kufurahia soka oa upunguziwe majukumu, utafurahi sana unacheza bila mawazo ya kufua soksi, jezi wala kufikiria namna ya kupata chakula,” anasema Rajabu.

PITISHA MUDA WA KULA MTOTO UDUNDWE

Raha ya ndoa upate mtoto buana unaambiwa mtoto anabaraka zake kwenye familia Rajabu anabainisha kuwa tangu wameanza uhusiano na mkewe Pilly wamejaaliwa kupata mtoto mmoja ambaye amekuwa faraja kwao na kujikuta wanafurahia maisha yao.

“Nampenda sana mwanangu muda wote natamani kuona yupo kwenye furaha ata nikiwa nyumbani basi huwa napambana kuhakikisha anakula kwa wakati anakuwa msafi muda wote hivyo ukitaka kunikwaza mcheleweshe kumuandalia chakula tutapigana,” anasema kiungo huyo.