PASCAL TOKODI : Bachela anayetesa ndani ya Selina

Muktasari:

Mwanaspoti limezungumza naye ambapo, amefunguka mambo kibao wakati akiwa safarini kwenda kushiriki tamasha la Guinness Smooth Launch Party mjini Kisumu, Kenya.

Pascaliaono Lpesinoi Lenguro Tokodi ndio habari ya mjini kwa sasa. Supastaa huyu kutoka Kisamburu anatesa kwenye faini ya maigizo Afrika Mashariki kwa sasa.

Kutokana na ugumu wa kulitamka jina lake pamoja na urefu wake vilevile, tutamwita tu Pascal Tokodi jinsi anavyofahamika na wengi. Tokodi ni mmoja wa wasanii wenye vipaji vya ajabu.

Huyu ni mwigizaji akitamba kwenye tamthilia ya Selina, lakini pia ni mwanamuziki mtaalamu wa ngoma za kimapenzi.

Mwanaspoti limezungumza naye ambapo, amefunguka mambo kibao wakati akiwa safarini kwenda kushiriki tamasha la Guinness Smooth Launch Party mjini Kisumu, Kenya.

Yapata miaka mitatu iliyopita ulijishindia Dola 10,000 (Sh1 milioni) katika shindano la uimbaji kule Nigeria Teckno Own Stage, hizo hela mzee ulifanyia nini?

Tokodi: Mwana unajua sinaga mazoea ya kuzungumzia matumizi yangu, hivyo nitakuomba tuliweke hili pembeni kidogo ila naweza kusema niliifanyia matumizi mazuri kwa kuwekeza kwa mambo mbalimbali.

Wewe ni msanii mwenye kipaji, unaimba, unaigiza na hata unajihusisha na ucheshi, je ni kipi kingine kipya ambacho hatukijui kuhusu wewe?

Tokodi: Nimeanza kujihusisha na kuwa produsa wa filamu na sasa nimeanza kujifua kuwa mwelekezi wa filamu na matangazo na ni kitu ambacho nimekuwa nikifanya kwa takriban miaka miwili sasa.

Unaweza kusema kuna tofauti gani kati ya kuigiza na kuwa mwelekezi?

Tokodi: Wanasema ukitaka kuwa dereva mzuri basi jifunze kuendesha kila aina ya gari na ndicho ninachokifanya sababu napenda shughuli hizi. Hata hivyo kama kutakuwa na utofauti nafikiri bado sijagundua. Sipendi kufungiwa kwenye eneo moja tu, hapana.

Ni filamu ipi umeelekeza?

Tokodi: Kuna ‘Selina’, ‘Kalamu na Ndeng’a’, pia matangazo ya kibiashara ya kampuni mbalimbali kwa mfano lile tangazo la Safaricom ‘Nani ataniscratchia’ ni kazi yangu.

Series ya Kalamu na Ndeng’a alipigwa marufuku na Ezekiel Mutua hii ishu imefikia wapi na ni kwa nini ilitokea vile?

Tokodi: Maprodusa waliniomba nisilizungumzie ishu hii kwa sasa ila ni moja ya kati ya kazi kubwa niliyowahi kuhusishwa.

Unafikiri ni kwa nini Mutua aliamua kuipiga marufuku?

Tokodi: Siwezi kujua, labda tumuulize yeye si wajua tena ndiye bosi wa bodi ya filamu nchini sababu dhamira yangu ipo haina tatizo kabisa na kazi hiyo.

Muziki pia unafanya ila haonyeshi kujituma jinsi unavyofanya kwenye uigizaji?

Tokodi: Ni kweli na hii ni kwa sababu ya kuwa na ratiba ya kubana sana. Sio rahisi kupata muda wa kuingia studio kurekodi na kwa wakati huo kupata muda wa kushuti inabidi upande mmoja uuumie na hapa ni muziki wangu unaumia ila sio kwamba, nitaacha kuimba.

Hivyo utaendelea kuachia muziki kwa kusitasita?

Tokodi: Hapana nijitahidi kuongeza nguvu pia kwenye muziki wangu ili muweze kunizungumzia hata zaidi.

Una mke ama mchumba?

Tokodi: Hahaha! Hamna labda unitafutie lakini kwa sasa bado sijaamua kuingia kwenye maisha hayo. Navuta muda kidogo.

Mwigizaji Kone alikuwa mtu wako wa karibu kifo chake ni vipi?

Tokodi: Duh! Yule muungwana ni mmoja kati ya watu stadi niliowahi kufanya kazi nao. Isitoshe niliipenda hulka na nafasi yake. Naumia sana alitutoka mapema ila kilichonitesa hata zaidi ni kuona jinsi blogu zilivyoandika habari za uongo baada ya kifo chake. Sikuelewa ni kwa nini? Hata kama ndio kutafuta click baits jamani.

Unamisi nini kutoka kwake?

Tokodi: Wajua tukiigiza alichukua uhusika wa kakangu mkubwa na ikaishia kuwa hivyo katika maisha yetu.