P Square wameamua kucheza Simba na Yanga

Sunday September 30 2018

 

By LUQMAN MALOTU

LEO mishale ya alasiri kinawaka “Kwa Mchina”, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ni Simba na Yanga. Mechi ambayo ina ukubwa usiolinganishwa ni michezo mingine ya timu za mji mmoja (derby), kokote Afrika. Kwa Tanzania, hakuna shughuli kubwa kupita Simba na Yanga. Iko hivyo, klabu hizi zinashughulisha watu.

Simba na Yanga ndizo ambazo zinakaribia kuigawa Tanzania pande mbili sawa. Inaweza kuwa kuwa asilimia 50 kwa 50 kupata 100, au chini kidogo lakini haivuki chini ya asilimia 90. Mgawanyo huu wa asilimia huwezi kuupata kokote duniani kwa klabu mbili kugawana mashabiki kwa wastani YANGA

Lipo kundi fulani husema halishabikii Simba wala Yanga lakini zinapocheza hufurahi au kuumia kimyakimya kwa aina ya matokeo ambayo timu iliyo ndani ya mapenzi yao hupata. Naomba niseme kwa msisitizo; Simba na Yanga ni taasisi pacha na maisha ya Watanzania.

Upacha wa Simba na Yanga kwa maisha ya Watanzania haupatikani kokote duniani. Ni rahisi shabiki wa Barcelona kuwa mnazi wa Real Madrid au kinyume chake lakini siyo shabiki wa Simba kuipenda Yanga au kinyume chake.

Inawezekana mkereketwa wa Inter Milan kuishabikia AC Milan au kinyume chake lakini hali hiyo huwezi kuipata Simba na Yanga. Mechi ya Simba dhidi ya Yanga huwa na msisimko wa hali ya juu, na mguso wake haufanani na mahali popote duniani.

Mguso ambao naujengea hoja ni ule upacha wa Watanzania kwa timu zao mbili, Simba na Yanga. Nafahamu zitaibuka hoja kuhusu mchuano mkali wa wapinzani wa jadi nchini Argentina kati ya Boca Juniors dhidi ya River Plate (Superclasico).

Takwimu za zinaonyesha kuwa Boca Juniors na River Plate, zinabeba asilimia 70 ya mashabiki wote wa soka Argentina. Boca ikiwa na asilimia 40, River ikiwa na asilimia 33. Ukija Tanzania utakuta kuwa asilimia 100 ya mashabiki wa soka nchini wapo Simba na Yanga.

Nenda Uturuki wakute Fenerbahce dhidi ya Galatasaray (Intercontinental Derby), fika Scotland uwaone Celtic na Rangers (The Old Firm), ukikanyaga Serbia utawashuhudia Red Star Belgrade na Partizan Belgrade (The Eternal Derby), shusha maguu Uholanzi ukutane na Ajax dhidi ya Feyenoord (De Klassieker), bado vionjo vya Simba na Yanga vipo kipekee sana.

Hazinishtui Liverpool na Manchester United (North-West Derby) England wala Roma na Lazio (Derby della Capitale) Italia. Natambua ukali wa mahasimu wa Ugiriki, Olympiakos dhidi ya Panathinaikos (Derby of the Eternal Adversaries), Brazil kati ya Palmeiras dhidi ya Corinthians (Paulista Derby), ongezea El Clasico (Barcelona na Madrid) pamoja na Derby della Madonnina (Inter na AC Milana), bado nazipa thamani Simba na Yanga.

P SQUARE NI SIMBA NA YANGA

Anyways, ya Simba na Yanga tutayajua leo jua litakapozama, baada ya shughuli ya dakika 90. Hapa nawacheki vijana mapacha, wanaofanana sana, si tu kwa sura, bali hata maumbo, kimo, sauti zao na kipaji cha muziki. Hata hivyo, tofauti yao kubwa ipo kwenye tabia.

Mapacha hao ni vijana wawili wanaounda kundi la muziki la P Square. Ni Paul na Peter Okoye. Nyakati za maelewano yao waliibeba Pop ya Nigeria kwenye mabega yao na wakatawala soko la muziki Afrika. Ubabe wa muziki wa lingala, Soukous na Rhumba, ulimalizwa na majanki hao. Kwaito pia ilifunikwa.

Muziki hawaufanyi kwa kuungaunga. Walikaa darasani kuusomea. Hiyo ni sababu ya uhodari wao wa kuchezea vifaa na mpangilio bora wa sauti kwenye nyimbo zao. Utawakubali P Square wakifanya shoo kwa live band. Wanajua kutumia kila kifaa cha muziki kwa kiwango bora.

Hawakuibuka tu kuwa P Square. Miaka ya 1990 wakiwa vijana chini ya umri wa miaka 20, waliungana na wenzao watatu, M Clef a.k.a Itemoh, Michael na Melvin kuunda kundi lililoitwa MMMPP, likisimama kama herufi za mwanzo za majina yao ya kwanza. Baadaye walimpiga chini M Clef na kubadili jina kwa kupunguza M moja, hivyo kuwa MMPP.

Hapo haikuwa mwanzo, wala hawakuanza kuimba. Ukichaa wao wa muziki ulianzia kwenye mabreka. Wakawa wanamrudi Michael Jackson na mitindo yake ya ‘kusheki’, wakati huo walikiita Smooth Criminals. Pamoja na kusomea muziki, Paul na Peter ni wasomi wa Usimamizi wa Bishara, shahada zao walizichukulia Chuo Kikuu cha Abuja.

Mwanzoni mwa miaka 2000, waliamua kusimama wenyewe wawili, hasa baada ya washkaji zao kutawanyika kwa sababu za masomo. Walianza kujiita Double P, baadaye P&P, wakaona michosho na kujitambulisha kama Da Pees, lakini mwisho P Square lilisimama.

Mwaka 2002 wakaingiza alabamu yao ya kwanza sokoni yenye kuitwa Last Nite, mwaka 2005 wakatoboa ya pili yenye jina Get Squared. Mwaka 2007, walifanya balaa kubwa katika albamu yenye jina Game Over. Inatajwa kufikia mauzo ya nakala 8 milioni. Midude kama Do Me, No One Like You, Roll It, Ifunanya na More Than A Friend, zilibamba si kitoto.

Ni kweli albamu zilizotangulia zilitisha, lakini hii ilikuwa funga kazi. Nakala 8 Milioni zinafungisha tela mpaka mastaa wakubwa Marekani. Kanye West na ufaza wake wote hajawahi kuingiza mzigo sokoni ukauza nakala 4 milioni. Majanki wa Nigeria ‘walitupiamo’ 8 Milioni.

Baada ya hapo zikawa shoo kubwakubwa. Afrika walitumbuiza kwenye viwanja vikubwa vya soka. Walipoenda Ulaya na Marekani, sharti lao kwa shoo ni kwamba pamoja na mkwanja mzuri, lakini lazima onesho lifikishe mauzo ya tiketi 5000, chini ya hapo hawakupanda jukwaani.

Ungewagusa kwa onesho moja, fedha zao zilianzia Dola 250,000 (zaidi ya Sh570 milioni) kupanda juu. Lebo yao, Square Records, ilimudu kuwaingiza studio na Akon, Rick Ross pamoja na T.I kisha kutoa kolabo zilizotia fora kama Chop My Money, Beautiful Onyinye na EjeAJo.

DIMBA LAO SASA

Wana pesa nyingi. Magari ya kifahari na mijengo ghali Nigeria na Marekani kuliko mastaa wengi wa Ulaya na Marekani. Mwanzoni walinunua mjengo mkali na wakawa wanaishi wote. Mwaka 2015 walitangaza kumwagana. Peter ndiye alikinukisha kwa kuiondoa familia yake katika nyumba yao na kutaka iuzwe kila mtu afe na chake. Mwaka 2016 baada ya mazungumzo, wakirejea pamoja, wakatoa ngoma kali kama Bank Alert na Nobody Ugy. Mwaka 2017, Peter akatangaza tena kuvunjika kwa kundi lao kwa kile anachodai kuwa Paul hamheshimu pamoja na familia yake. Akasema pia kwamba Paul huwa anamtukana.

Nyuma ya stori ni kuwa Paul ni mchapakazi, Peter ni bishoo mpenda bata kwa sana. Sasa Paul huamua kumhimiza Peter azingatie muda na uwajibikaji hasa katika ratiba za shoo na kurekodi.

Advertisement